Post Details

JAJI MKUU AWATAKA WATUMISHI KUTENDA HAKI BILA UBAGUZI

Published By:LYDIA CHURI

  • Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye awashauri kusimamia Misingi ya Maadili

Na Lydia Churi- Mahakama, Iringa

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama kutenda haki kwa watu wote wote pasipo kuangalia hali ya kiuchumi ama kijamii ya Mtanzania anayefika mahakamani kutafuta haki.

Akizungumza kwenye Mkutano kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Iringa, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo aliwaambia watumishi hao kuwa Katiba ya nchi imeupa Mhimili wa Mahakama imani kubwa ya kusimamia suala la utoaji haki hivyo hawana budi kutekeleza jukumu hilo kwa kufuata sheria.

“Tunalo jukumu kubwa la kusimamia haki na Katiba ya nchi inatutaka kutochelewesha upatikanaji wa haki pasipokuwa na sababu za msingi, hivyo mnapotekeleza wajibu wenu vizuri mnaipa uhai Katiba” alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu alisema suala la utoaji haki ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo inazingatia uwepo kwa amani katika jamii, hivyo endapo watumishi wa Mahakama watatekeleza wajibu huo kikamilifu watatoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.  

Alisema Majaji na Mahakimu wanapotoa maamuzi ya kesi kwa wakati wataiwezesha Mahakama kuchangia katika kujenga uchumi wa Taifa kwani wananchi watapata muda zaidi wa kufanya shughuli za uzalishaji. “Tusisahau kuwa tunapotoa haki kwa wakati tunachangia maendeleo ya Taifa letu”, alisisitiza.

Kuhusu matumizi ya Tehama, Jaji Mkuu alisema Mahakama imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye Tehama hivyo ipo haja ya kwenda mbele zaidi katika matumizi hayo ili kuendana na karne ya 21 ya Mapinduzi ya nne ya viwanda. Aliongeza kuwa matumizi ya Tehama yataongeza uwazi, ufanisi na kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.

Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof. Adelardus Kilangi amewashauri watumishi wote wa Mahakama nchini kufanya kazi zao kwa kusimamia misingi ya maadili yanayotarajiwa kwao.

“Tufahamu kuwa kila wakati jamii inatutazama, inaangalia tunavyofanya kazi hivyo fanyeni kazi kwa kuzingatia weledi, ufahamu na kuzingatia maadili na miiko yote iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria, kanuni, taratibu na hata mapokeo”, alisema Mwanasheria Mkuu.

Alisema endapo watumishi wa Mahakama watafanya kazi kwa kuzingatia maadili, watatoa mchango mzuri katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla na kuchangia kuwa na jamii iliyo tulivu.

Kiongozi huyo pia ametoa wito kwa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za mikoa na wilaya kuongozwa na maadili zinapofanya kazi yake.

Wajumbe wa Tume hiyo leo wameanza ziara katika Mkoa wa Iringa na baadaye mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa Mahakama.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume hii iliundwa kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama.

Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji, kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.

Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.

 

Comments (0)

Leave a Comment