Post Details

UTEUZI WENU NI SAHIHI MSIWE NA WASIWASI; JAJI MKUU

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma amewahakikishia Majaji Wateule kuwa uteuzi wao ni sahihi na hivyo wawe tayari kufanya kazi na Mahakama mara baada ya kuapishwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na Majaji hao alipokutana nao mapema leo Mei 17, 2021, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa uteuzi wa Majaji hao walioteuliwa ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais baada ya kujiridhisha.

“Napenda kuwahakikishia kwamba mara baada ya kuapishwa ninyi ni Majaji kamili, kwa sababu mnafahamu mchakato mliopitia ambao kwa bahati mbaya watu wengi sana hawajui mchakato upi tumepitia hadi kuwapata Wahe. Majaji, kwa bahati mbaya huko nje kwenye mitandao kuna dhana kwamba Majaji wanapatikana kirahisirahisi ili hali tunapitia michakato mbalimbali ya kujiridhisha tofauti na nchi nyingine,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma aliwahakikishia Majaji hao kuwa majina yao ni miongoni mwa majina bora yaliyoteuliwa hivyo kuwataka kupuuza baadhi ya maneno yanayoelekezwa kwa baadhi yao na kujielekeza kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao kuungana na Mahakama kufanya kazi kwa kuzingatia nguzo tatu (3) ambazo Mhimili huo umejiwekea ambazo ni Utawala bora na Uwajibikaji, Usimamizi wa rasilimali na Kuimarisha ushirikiano na wadau ili kufikia dhima ya Mahakama ya kutoka haki sawa kwa wote na kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Majaji Wateule, Jaji Mteule wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revokatti alimuhakikishia Mhe. Jaji Mkuu na Viongozi wengine wa Mahakama walioambatana na Mhe. Jaji Mkuu kuwa watafanya kazi ya kazi ya utoaji haki kwa ufanisi ili kuendeleza jitihada za maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Jumla ya Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani saba (7) na wa Mahakama Kuu 21 wanatarajiwa kuapishwa leo Mei 17, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Comments (0)

Leave a Comment