Post Details

MAHAKAMA YA TANZANIA YAIPONGEZA ZANZIBAR KUPATA MKOPO WA KUTEKELEZA MIRADI YA MABORESHO

Published By:innocent.kansha

Na. Innocent Kansha- Mahakama

Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Angelo Rumisha, amesema kwamba Mahakama ya Tanzania imepokea kwa furaha kuona Mahakama ya Zanzibar imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mradi wa Maboresho wenye lengo la kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Akizungumza na ujumbe wa Maafisa kutoka Zanzibar uliongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim, hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mhe. Dkt. Rumisha alisema kwamba, Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania kipo tayari kushirikiana na Kitengo cha maboresho ya Mahakama ya Zanzibar katika kuhakikisha kinatekeleza majukumu yake.

“Tuwahakikishie kuendelea kutoa ushirikiano mara zote wa kubadilishana taarifa zote muhimu kwa kubadilishana uzoefu, kutatua changamoto za utekelezaji endapo zitatokea na kwamba milango ipo wazi muda wote mtakapohitaji msaada wetu,” alisema Mhe. Dkt. Rumisha.

Mahakama ya Zanzibar kama ilivyo kwa Mahakama ya Tanzania imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Maboresho utakaojulikana kwa jina la Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar ‘Zanzibar Judiciary Modernisation Project’ (Zi-JUMP) mradi huo umeidhinishwa na Benki ya Dunia mnamo tarehe 10 Mei, 2024 na unatarijiwa kuanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2024 hadi tarehe 1 Julai, 2029. Mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miaka 5.

Akizungumza wakati wa mafunzo mafupi ya kubalishana uzoefu juu ya utekelezaji wa mradi wa maboresho yalifanyika kwa siku mbili Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim alitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Mahakama ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa na Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania kwa kuwapatia uzoefu mkubwa na kuahidi kufanyia kazi uzoefu huo ili kuhakikisha kwamba wanafikia malengo ya Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Zanzibar.

Aidha, Mhe. Ibrahim alimwomba Mkuu wa kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU) kuendelea kuwapa ushirikiano na uzoefu zaidi pale watakapohitaji kwa kuwa wanatambua kazi kubwa iliyopo mbele yao.

Vilevile, Maafisa hao wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama kutoka Zanzibar wakiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama Zanzibar Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim walipata wasaa wa walitembelea Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya kushiriki katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maboresho iliyofanywa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete aliyoifanya hivi karibuni na kupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi hiyo.

Baada ya ziara hiyo ujumbe kutoka Zanzibar uliwasili katika Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU) kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kusimamia Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho ya Mahakama ‘Citizen- Centric Judicial Modernisation and Justice Sevice Delivery Project’ unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, kwakuwa Kitengo hicho hadi sasa kina uzoefu wa miaka 8 ya kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho ya Mahakama.

Aidha, ujumbe huo pamoja na mambo mengi ulipitisha kwenye mafunzo mbalimbali ikiwemo namna bora ya kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho.

Maeneo mengine waliyojifunza ni kuhusu majukumu ya kitengo cha maboresho ya Mahakama Tanzania (JDU) na majukumu ya watumishi wa Kitengo hicho.

Vilevile, ujumbe huo ulijifunza kuhusu namna ya kuandaa maandiko dhana ‘concept notes’, menejimenti ya masuala ya manunuzi, uandaaji mipango kazi, na masuala ya usimamizi wa fedha za mradi ‘Financial Management’.

Comments (0)

Leave a Comment