Post Details

ASKOFU MALASUSA ATEMBELEA KITUO JUMUISHI TEMEKE

Published By:magreth.kinabo

Asisitiza Watanzania kuandika wosia

  • Jaji Mfawidhi asema Viongozi wa Dini muhimu katika kufanikisha haki

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Baba Dkt. Alex Malasusa, jana jioni tarehe 21 Mei, 2024 alitembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam, kujifunza mambo mbalimbali na kujionea jinsi kinavyofanya kazi.

Baba Askofu Malasusa aliwasili katika Mahakama hiyo majira ya saa tisa alasili na kupokelewa na Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa. Wakati wa maapokezi hayo, alikuwepo pia Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Frank Moshi na Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Bi. Mary Shirima.

Baada ya kuwasili mahakamani hapo, Baba Askofu Malasusa,  ambaye aliambatana na Wachungaji na Wakuu wa Majimbo wa Kanda za Kanisa hilo takribani 31, alipitishwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo chumba maalum cha akina mama cha kunyonyeshea watoto, Mahakama ya Watoto, ofisi ya utoaji msaada wa kisheria na ofisi ya ustawi wa jamii.

Ugeni huo pia ulipata maelezo mafupi jinsi Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi unavyofanya kazi na namna unavyoharakisha utoaji haki kwa wananchi kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa wazi kushiriki kwenye uwasilishaji wa mada mbalimbali.

Moja ya mada hizo ilihusu uendeshaji wa mashauri ya ndoa na mirathi katika Kituo iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. John Msafiri na mchango wa Viongozi wa Dini katika masuala ya mirathi na ndoa iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi, Mhe. Loveness Mwakyambiki.

Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kituo hicho. Mhe. Gladys Barthy, Mhe. Asina Omary na Mhe. Sharmillah Sarwatt, walihudhuria zoezi la uwasilishaji wa mada hizo na kushiriki kikamilifu katika kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na Viongozi hao wa dini wakati wa mjadala. 

Akizungumza kabla ya uwasilishaji wa mada hizo, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa shughuli za utoaji haki katika kituo hicho haziwezi kufanyika bila ushiriki wa Viongozi wa Dini kupitia Taasisi mbalimbali zilizoundwa kisheria. 

“Hii inaonesha umuhimu wenu katika zoezi la utoaji haki, hivyo napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati katika kufanikisha jitihada za utoaji haki katika kituo chetu. Ninyi ni wadau muhimu katika shughuli zetu kwani mmebeba dhamira kuu ya kusimamia imani za wanajamii,” alisema.

Mhe. Mnyukwa alibainisha kuwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971, sura ya 29 inatambua ndoa zilizofungwa katika Taasisi za Dini na pia katika mirathi Mahakama inazingatia imani ya marehemu katika kushughulikia mirathi. 

Katika muktadha huo, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa masuala ya mirathi na ndoa yana mahusiano makubwa na imani, hivyo ushiriki wa Viongozi wa Dini hauepukiki katika kushughulikia mashauri hayo mahakamani. 

“Kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024, Kituo kilitoa jumla ya hati za talaka 444. Idadi hii  inadhihirisha wazi kuwa Viongozi wa Dini mnalo jukumu kubwa katika  kuisaidia jamii katika eneo hili,” alisema. 

Mhe. Mnyukwa aliwaambia Viongozi hao kuwa Mahakama hukosa mamlaka ya kusikiliza shauri la mirathi inapokosekana fomu Na. 3 ambayo inatolewa na Bodi za Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa zilizoundwa na Taasisi za Serikali na Dini. 

Alisema pia kuwa Mahakama huamua sheria ipi itumike katika shauri la mirathi kwa kuzingatia imani ya dini ya marehemu, hivyo hayo yote yanaonesha nafasi kubwa waliyonayo Viongozi wa Dini katika usikilizaji wa mashauri ya mirathi na ndoa mahakamani.

“Wakati wa kubadilishana mawazo baina yetu, tutaweza kuainisha changamoto na ushiriki wa Viongozi wa Dini katika mashauri ya ndoa na mirathi, ni matumaini yangu kuwa mtatushauri namna bora ya kuondokana na changamoto hizo ili kuinua hali ya utoaji haki kwa wakati,” Jaji Mfawidhi alisema.

Baada ya uwasilishaji wa mada hizo, Viongozi hao wa dini walipata nafasi ya kuuliza maswali na kutoa maoni mbalimbali namna ya kuboresha utendaji na ushauri wa kuangalia upya mwongozo wa mafundisho ya ndoa katika kanisa, hasa baada ya kugundua kuwa chanzo kikubwa cha ndoa kuvunjika ni uzinzi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yake, Baba Askofu Malasusa alieleza kufurahishwa na namna Kituo hicho kinavyofanya kazi na maboresho makubwa ambayo yamefanywa na Mahakama ya Tanzania katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa wananchi.

Aliomba ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na Viongozi wa Dini katika nyanja mbalimbali uendelee, kwani amegundua wanafanya kazi moja katika maeneo mengi kupitia njia tofauti.

“Tulipofika hapa na kuanza kukutana na wale wanaotoa msaada kisheria na maafisa ustawi wa jamii, wanasheria, Mahakimu na Majaji tumeona kuna mambo mengi sana yanakwenda pamoja. Hata hii hoja ya ndoa na talaka tuliyokuwa tunaijadili hapa sisi imetugusa sana. Hivyo, tunahitaji kukutana mara kwa mara ili tuifanye kazi hii vizuri,” alisema.

Baba Askofu Malasusa alitumia fursa hiyo kuziomba mamlaka zinazotengeneza sheria kufanya maboresho ili kupunguza utoaji wa talaka Tanzania. “Nina hakika talaka zisizokuwa na sababu zipo nyingi sana, leo ndiyo nimeshangaa kwamba mtu anaamua hata kwenda kujiunga na dini au thehebu nyingine ili kumfanya mwenzake amuache,” alisema.

Aidha, alisisitiza Watanzania kuandika wosia na akaiomba Mahakama kutoa semina na mafundisho mbalimbali ili kuondoa dhana potovu zilizopo kuhusu suala hilo.

“Sisi Waafrika kuandika wosia ni kama kujichulia au kwamba upo tayari kuondoka, kumbe ni utaratibu tu na mimi nina hakika Mahakama itakuwa mahali kwenye kesi za jinai na tutawapunguzi kazi Mahakimu na Majaji kama Watanzania wengi tutaandika wosia …

“Sisi tupo tayari na mimi nitaongea na Viongozi wenzangu wa dini wote, Waislam na mathehebu ya Kikristo kuona namna gani tunaweza kuhamasisha waumini waliochini yetu wawetayari kuandika wosia,” alisema.

 Ziara ya Askofu Mkuu Malasusa katika Kituo hicho ni matokeo ya juhudi zilizofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipoenda kufungua Kituo cha Msaada wa Kisheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam. 

Baba Askofu Malasusa alimshukuru Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Mama Shirima kwa kuwa kiungo muhimu na kufanikisha ziara hiyo.

 

Comments (0)

Leave a Comment