Post Details

MAHAKAMA KUU ARUSHA YAFANIKIWA KUSIKILIZA NA KUMALIZA MASHAURI  YA UGAIDI

Published By:magreth.kinabo

  

Na Magreth Kinabo – Mahakama

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha imetimiza malengo iliyojiwekea na kutekeleza maelekezo ya Mhe. Jaji Kiongozi ya kusikiliza na kumaliza mashauri yote ya ugaidi yaliyofunguliwa katika masjala hiyo.

Mashauri ni yale ambayo yalikuw na muda mrefu na hivyo kuwekewa mikakati ya kuyasikiliza na kuyamaliza ndani ya kipindi cha mwaka 2023 mara tu baada ya upelelezi wa mashauri hayo kukamilika. Mikakati hiyo ililenga kuhakikisha mashauri hayo yapatayo Matano yanasikilizwa na kufanyia uamuzi ilipofika Desemba 2023 jambo ambalo lilifanikiwa.  

Hayo yamesemwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga, wakati akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg. Gerard Chami, ambaye amefanya ziara ya kikazi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha hivi karibuni kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu shughuli zinazofanyika na mafanikio yaliyopatikana toka kuanzishwa kwa kituo Jumuishi cha utoaji Haki Arusha.  

“Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha iliweka mikakati ya kuondoa kero ya mashauri ya muda mrefu ya ugaidi ifikapo 30 Desemba 2023. Hili tulifanikiw kwa kusikiliza mashauri yote matano, ambapo mashauri matatu washtakiwa wameachiwa huru na mashauri mawili washtakiwa wametiwa hatiani na kufungwa. Hayo yalikuwa ni malengo ya kanda na hiyo ni kabla ya maelekezo ya Mhe. Jaji Kiongozi aliyoyatoa nchi nzima kuhusiana na usikilizaji wa Mashauri ya Ugaidi,” alisema Jaji Tiganga.

Jaji Tiganga pia alisema fanikio lingine katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei 2024, Mahakama hiyo imefanikiwa kufunga vifaa vya Mfumo wa Unukuzi na Utafsiri (Transcription and Translation System) (TTS) wa mwenendo wa usikilizwaji wa mashauri katika vyumba faragha (Chember Courts) vinne vya Majaji kwa gharama zake wezeshi za ndani, mbali na vile vifaa vilivyofungwa katika Mahakama za wazi nne zilizoko katika jengo hilo la IJC ambavyo vilifungwa kwa gharama na fedha kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

“Hii imefanya sasa Majaji wote saba wanaweza kwa wakati mmoja wakasikiliza mashauri kwa kutumia mfumo huu wa unukuzi wa utafsiri bila kusubiriana na hivyo kuwapunguzia adha ya kuchapa na kuandika kwa mkono,” alisisitiza.  

Aliongeza kwamba kufungwa kwa vifaa hivyo katika vyumba faragha  kumewezesha Waheshimiwa Majaji kusikiliza mashauri bila ya kuandika kama ilivyokua awali ambapo waliwajibika kusikiliza na kuandika kwa wakati mmoja hivyo jitihada hizo za kanda zimeunga mkono juhudi za viongozi wakuu wa Mahakama na Serikali katika kuharakisha utoaji haki na uamuzi unaofanywa na Mahakama kwa wakati kwa wadau wote wanaopata huduma za Mahakama katika eneo la mashauri.

Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Elia Mrema, alisema vifaa hivyo vya unukuzi na tafsiri vinafanya kazi vizuri ya kutafsiri lugha ya Kiswahili kwenda Kiingereza na Kingereza kwenda Kiswahili.

Mhe. Mrema alitaja faida nyingine ya kutumia mifumo huo wa unukuzi na tafsiri kuwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya shajara/makaratasi (stationaries) na kuwezesha mashauri mengi zaidi kumalizika kwa haraka na haki stahili kutolewa kwa wahusika wa pande zote katika shauri husika.

“Tumefanikiwa pia kutoa elimu kwa umma kwa kila siku ya Jumanne na Alhamisi, ambapo Wananchi wanapata nafasi ya kusikiliza mada husika ya siku hiyo kisha huuliza maswali na kutoa kero zao na kutafutiwa ufumbuzi papo hapo,” alisema Naibu Msajili huyo.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya, alisema uwepo wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kwa Wananchi katika Mkoa huo wa Arusha umepunguza gharama za uendeshaji, usafiri na kuongeza uwazi na uwajibikaji zaidi kwenye huduma za Mahakama ya Tanzania.

Kituo hicho kwa mwaka 2021 kilihudumia jumla ya wateja 83,425, mwaka 2022  wateja 80,640 na mwaka 2023 wateja 62,500, hii ilitokana na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri jambo ambalo haliwalazimishi wateja kufika mahakamani.  

Comments (0)

Leave a Comment