Post Details

WATUMISHI MAHAKAMA WAASWA KUFANYA KAZI KWA UPENDO NA USHIRIKIANO

Published By:magreth.kinabo

 

Na Francisca Swai – Mahakama Musoma.

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, wameaswa kufanya kazi kwa heshima, upendo, umoja na kwa kuzingatia utu wa mtu kabla ya kuangalia wadhifa wake.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Kamazima Idd, aliwaasa watumishi hao, katika kikao cha makabidhiano ya ofisi kati ya Bw. Festo Chonya Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma anayehama na Bw. Leonard Maufi Mtendaji anayehamia Kanda ya Musoma, yaliyofanyika tarehe 5 Machi,2024.

“Watumishi wote  tufanye kazi kwa heshima, upendo, umoja, ushirikiano, kwa kujali utu wa mtu,kabla ya kuangalia wadhifa wake na siku zote tuzingatie njia ya mazungumzo kama sehemu nzuri ya kufikia muafaka katika mambo mbalimbali kama alivyokuwa akifanya Bw. Chonya.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma  Mhe. Fahamu Mtulya alimpongeza Bw. Festo Chonya kwa kazi nzuri aliyoifanya Musoma ya kutekeleza majukumu yake kwa misingi ya haki na kuunganisha watumishi kufanya kazi kwa umoja jambo lililochangia kwa Mahakama hiyo kuwa ya pili kitaifa kwa kasi nzuri ya umalizaji wa mashauri.

Kwa upande wake Bw. Festo Chonya, Mtendaji anayehama Kanda ya Musoma, aliwashukuru viongozi, watumishi na wadau wa Kanda hiyo kwa upendo na ushirikiano mkubwa waliompa wakati wote alipokuwa Musoma. Pia aliwaasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa misingi uadilifu, weledi na uwajibikaji.

Aidha, Mtendaji mpya wa Kanda ya Musoma Bw. Leonard Maufi, aliwashukuru viongozi na watumishi kwa mapokezi mazuri na kuwaomba ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kila siku ili kuweza kufikia malengo yanayotarajiwa na Mahakama ya Tanzania.

Watumishi wote kwa pamoja waliohudhuria kikao hicho cha makabidhiano kilichohudhuriwa na viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma walikubaliana kuendelea kufanya kazi kwa upendo, umoja na ushirikiano ili kuhakikisha lengo kuu la utoaji haki sawa kwa wote na kwa wakati linafikiwa kama inavyotarajiwa.

 

Comments (0)

Leave a Comment