Post Details

JAJI MFAWIDHI DODOMA AHIMIZA HUDUMA BORA MAHAKAMANI

Published By:faustine.kapama

Na Arapha Rusheke, Mahakama-Dodoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu amewahimiza watumishi wa Mahakama kutimiza wajibu wao kikamilifu, ikiwemo kutoa huduma bora za haki stahiki kwa wananchi.

Mhe. Mdemu ametoa wito huo leo tarehe 28 Aprili, 2023 alipokuwa anafungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi katika Kanda hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa wilayani Kongwa.

“Pamoja na kuwa Mahakama inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ya kuboresha utoaji wa huduma za haki, bado huduma hizi zinahitaji tuziboreshe kila siku, wananchi walio wengi wanahitaji kupata huduma kwa kiwango stahiki,” amesema. 

Mhe. Mdemu ameeleza kuwa Mahakama inalo jukumu la kuwaelimisha wananchi na wadau ili wafahamu vizuri taratibu na miongozo inayohusika katika kupata huduma sahihi zinazotolewa mahakamani.

Amewakumbusha wajumbe wa Baraza hilo kuwa ili utumishi wa kila mmoja uweze kuheshimika ni wajibu kama watumishi wa Mahakama kufanya kilicho sahihi, ikiwemo kuzingatia weledi, kuwa waadilifu na kuwajibika ipasavyo.

Jaji Mfawidhi amebainisha kuwa watumishi wa umma ni waajiriwa wa wananchi, hivyo kwa nafasi zao wanatakiwa kuwatumikia na kila mmoja kufanya kilicho sahihi, kwa ufanisi na kwa wakati.

“Kwa hiyo, wito wangu kwa watumishi wa Mahakama ni kwamba kila mmoja atimize wajibu wake wa kutoa huduma bora,” alisema katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na wajumbe kutoka Singida na Dodoma na viongozi wa TUGHE.

Mhe. Mdemu amesisitiza kuwa maadili ni kitu muhimu cha kuzingatia katika utendaji wa kazi kwa kuzingatia hivi sasa Mahakama inafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha watumishi wanazingatia maadili yanayosimamia utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao. 

Hivyo, amesema, kuna umuhimu wa kila mtumishi kuonyesha juhudi za utendaji kazi kwa kufuata kanuni za maadili, ambazo zikifuatwa kwa ukamilifu watumishi watatoa huduma bora na inayostahili kwa wananchi ambao ndio waajiri wao.

Jaji Mfawidhi alitumia nafasi hiyo kuipongeza Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania Kanda ya Dodoma kwa kutekeleza takwa la kisheria ambao chimbuko lake ni tamko la Rais (Tamko Na 1 la mwaka 1970) na sheria nyingine za kazi zinazohimiza kuwashirikisha wafanyakazi katika kufanya maamuzi mbalimbali kupitia Mabaraza ya Wafanyakazi.

Amesema Mabaraza ya Wafanyakazi yameundwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za Mahakama na taasisi kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali watu, utekelezaji wa majukumu, kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi na maslahi na kusimamia haki na ustawi sehemu za kazi. 

“Mabaraza kama vyombo vya ushauri na usimamizi yana wajibu wa kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo chanya ya utendaji kazi yenye tija, staha na upendo. Nawashukuru sana wote waliowezesha baraza hili likafanyika,” amesema.

Naye Katibu wa TUGHE Mkoa, Bw Samweli Nyungwa, akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa Baraza la Kanda ni bunge la kanda, hivyo wajumbe wajue umuhimu wa baraza hilo kwani linawapa nafasi watumishi kuweza kueleza na kutatuliwa shida zao mbalimbali.

Mabaraza ya Wafanyakazi yapo kwa mjibu wa sheria na yanaongozwa na sheria kadha wa kadha ikiwemo Kanuni za Majadiliano katika Utumishi wa Umma za Mwaka,2005 na Kanuni za uendeshaji wa Mikutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania, 2018.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Comments (0)

Leave a Comment