Post Details

HUDUMA ZAIMARIKA JENGO JIPYA LA MAHAKAMA YA WILAYA YA KILWA

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Kilwa Masoko

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Kilwa Mhe. Frank Michael Lukosi amesema kujengwa kwa jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Kilwa kumerahisisha utendaji kazi wa Mahakama hiyo ambapo hivi sasa mashauri yanamalizika kwa wakati.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama leo wilayani humo, Mhe. Lukosi amesema kuna mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za kimahakama baada ya kuanza kutumika kwa jengo jipya la Mahakama ya wilaya ambapo awali Mahakama ilikuwa ikitumia jengo lililoazimwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya lililokuwa na nafasi finyu kwa ajili ya kutolea huduma.

“Tulikuwa tukipeana zamu kutoa huduma kutokana na kuwa na vyumba vichache, tulikuwa tukipata shida ya mtandao (internet) na wakati huo huo mashauri yalikuwa yakichelewa kuanza na hivyo kuchelewa kukamilizika”, alisema Hakimu huyo.

Alisema jengo jipya linakidhi idadi ya vyumba vya Mahakimu, watumishi wengine pamoja na vyumba kwa ajili ya Mawakili na waendesha mashtaka. Aliongeza kuwa kutokana na jengo hilo kuunganishwa kwenye mkongo wa taifa wa Mawasiliano hivi sasa wanapata mtandao vizuri na kazi ya kuingiza mashauri kwenye mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri wa Mahakama (JSDS 2) inafanyika kwa ufasaha.

Akizungumzia mashauri yanayosajiliwa na Mahakama ya wilaya ya Kilwa, Mhe. Lukosi amesema mwaka jana kulikuwa na mashauri mengi yaliyosajiliwa lakini mwaka huu mashauri ni machache (52) kutokana na kutokea kwa tatizo la mafuriko pamoja na uwepo wa ugonjwa wa Covid 19 nchini.

Kwa mujibu wa Hakimu huyo, wilaya ya Kilwa inaongoza kwa kuwa na mashauri mengi ya jinai yanayohusiana na ubakaji, mimba za utotoni na mashauri ya Ndoa.

Wakati huo huo, Katibu Tawala (DAS) wa wilaya ya Kilwa Bw. Haji Mbaruku Balozi amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kujenga jengo la Mahakama linaloendana na hadhi ya Mhimili wa Mahakama ambapo hivi sasa wananchi wanapata haki zao kwa wakati.

Alisema licha ya kujengwa kwa jengo hilo wilayani humo, bado Mahakama inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa baadhi ya majengo ya Mahakama za Mwanzo wilayani humo.      

Bw. Balozi pia aliishukuru Serikali kwa kuyaingiza mabaraza ya Ardhi ndani ya  mfumo wa Mahakama ambapo alisema wananchi waliokuwa wakikosa haki zao wakati mabaraza hayo yalipokuwa nje ya mfumo wa Mahakama sasa watapata haki zao.

Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kilwa lilizinduliwa rasmi mwezi Januari mwaka huu na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Mahakama ya Tanzania inaendelea na ujenzi wa majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini.

Comments (0)

Leave a Comment