Post Details

MIUNDOMINU YA MAJENGO IWE KIELELEZO CHA HUDUMA BORA KWA WANANCHI: JAJI KIONGOZI

Published By:faustine.kapama

Na Waandishi wetu-Mahakama -Katavi

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ametoa wito kwa watumishi kuhakikisha uboreshaji wa miundominu ya majengo ya Mahakama inakuwa kielelezo cha huduma bora kwa wananchi.

Mhe Siyani ametoa wito huo leo tarehe 18 Januari, 2023 katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi wakati wa uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi Lindi, Songwe na Katavi.

Alisema uzuri wa muonekano na ubora wa miundombinu unatarajiwa kuwa uendane  na wajibu ambao Watanzania wamekasimu kwa Mahakama.

“Msiwaangushe Watanzania kwa kuendekeza ubinafsi, rushwa na upendeleo. Haya ni magonjwa ambayo tiba yake ya kwanza na kamili inapaswa kutoka miongoni mwenu wenyewe,” alisisitiza.

Alisema kuwa watumishi wa Mahakama wanapotumia majengo hayo wakumbuke kwamba yanatokana na kodi za Watanzania ambao watakuja kutafuta haki mbele yao.

Mhe. Siyani aliwataka watumishi watakaohudumu katika majengo hayo kuyatunza ili yadumu na wanatakiwa kuchapa zaidi kazi ili wajenge imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.

Jaji Kiongozi alisema uzinduzi wa Mahakama hizo tatu za Hakimu Mkazi Katavi, Songwe na Lindi ni matokeo ya uwezeshwaji unaoendelea kufanywa na Serikali pamoja na usimamizi na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu unaofanywa na watumishi wa Mahakama.

“Naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutenga fedha zinazowezesha maboresho makubwa yanayoendelea mahakamani na kipekee, nimshukuru sana Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka misingi mizuri inayoiwezesha Mahakama kujenga miundombinu yake na hivyo kuwa na mazingira mazuri yanayoiwezesha kutimiza wajibu wake,”alisema.

Alisema lengo la Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa huduma inazopaswa kuzitoa zinawafikia wananchi katika kila Mkoa.

Comments (0)

Leave a Comment