Post Details

MATARAJIO YA WANANCHI NI MAKUBWA: MSAJILI MAHAKAMA KUU

Published By:faustine.kapama

Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma

Mafunzo ya huduma kwa mteja kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika yameingia siku ya pili leo tarehe 6 Disemba, 2022 huku Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akiwataka washiriki hao kutoa huduma bora kwa wananchi wanapotekeleza majukumu yao mahali pa kazi.

Akiwasilisha mada kuhusu Wajibu na Majukumu ya Watumishi katika Mahakama za Chini, Mhe. Sarwatt aliwaambia washiriki hao wa mafunzo kuwa matarajio ya wananchi ni makubwa, hivyo wanahitaji kutimiza wajibu wao kwa kiwango kitakachowafanya wajisikie wapo mahala salama au peponi.

“Tunajua hakuna miongoni mwetu anayejua peponi kuna nini, lakini itoshe tu kusema tunategemea hali ya juu ya maadili kutoka kwenu. Hata kama tuna changamoto zetu, bado hazitupi kibali cha kumhudumia vibaya mwananchi. Tunahitaji kutoa huduma bora kwa mwananchi, na hili ndilo tegemeo letu,” alisema.

Msajili wa Mahakama Kuu huyo aliwaeleza watumishi hao sababu kadhaa za kujengwa Mahakama watakazohudumu kwa muundo kama unavyoonekama, ikiwemo kuandaa njia ya kupata haki kwa wote kama Mahakama inavyotarajia, kuwa na mtindo mpya wa kufanya kazi kwa uwazi na matumizi ya teknolojia.

“Labda niwaambie ndugu zangu, kwa namna tunavyokwenda kwa sasa, matumizi ya teknolojia katika shughuli za kimahakama hayana mbadala, ukipenda utatumia na usipopenda utatumia. Anzeni kutumia teknolojia kuendesha shughuli za Mahakama mkifika kwenye vituo vyenu vya kazi, hili halina mjadala,” Mhe. Sarwatt alisisitiza.

Naye Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama, Bw. Jumanne Muna, akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa Huduma kwa Mteja, aliwaomba washiriki hao wa mafunzo kutambua kuwa wanalojukumu kubwa la kutangaza mema ya Mahakama kupitia huduma wanazozitoa kwa wamanchi.

Akiwasilisha mada hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick, Bw. Muna alieleza kuwa watumishi wakitoa huduma bora kwa wananchi watapeleka taswila njema kwa jamii na jamii itatambua kuwa mahakamani ni mahala salama kuliko pengine katika muktadha mzima wa utoaji wa haki nchini.

“Mahakama ni sehemu ya kutoa huduma. Lazima kama sisi watumishi tujiulize tunatoa huduma za namna gani na kwa wakati gani. Lazima tujue huduma wanazohitaji wateja wetu. Wateja wetu wanamatarajio makubwa sana kutoka kwetu. Kwa hiyo, inatulazimu sasa kuwahudumia vizuri kwa vile bila wao hatutakuwa na stahiki yoyote ya kuendelea kuwa sehemu zetu za kazi,” alisema.

Bw. Muna amewakumbusha watumishi hao baadhi ya huduma ambazo wanapaswa kuzitoa kwa wateja, ikiwemo kutoa kalenda ya shughuli za Mahakama; kutoa ratiba ya kusikiliza mashauri; kupokea, kusajili na kusikiliza mashauri; kutayarisha na kusoma uamuzi; kutoa na kuthibitisha nyaraka mbalimbali za kimahakama na kutekeleza, kukaza hukumu, amri na uamuzi wa Mahakama.

“Hatuna budi kutekeleza majukumu ya Mahakama na kuhakikisha kuwa tunazingatia viwango vilivyobainishwa na kutoa huduma kwa ubora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya mteja. Tuna jukumu la kuijenga taswira ya Mahakama na kurudisha imani kwa wananchi,” alisema.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.

Comments (0)

Leave a Comment