Post Details

HAITOSHI KUWA NA SHERIA KAMA HAZIWANUFAISHI WANANCHI

Published By:LYDIA CHURI

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema haitoshi kwa nchi kuwa na sheria katika vitabu endapo sheria hizo hazieleweki, hazistawishi na haziboreshi maisha ya wananchi.

Akizungumza baada ya Matembezi ya kuzindua wiki ya Sheria ambayo hutumika kutoa elimu ya sheria leo jijini Dodoma, Jaji Mkuu amesema ubora wa sheria siyo maandishi yaliyomo kwenye sheria husika bali ni sheria kuwa na malengo yenye manufaa kwa wananchi.

Alisema pamoja na sheria za Tanzania kuwa na malengo maalum bado sheria hizo zinatakiwa kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo ni kuboresha hali ya maisha ya watanzania, kuweka mazingira ya amani, usalama na umoja na kujenga utawala bora.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, malengo mengine ni pamoja na kuwezesha jamii iliyoelimika vyema na inayojifunza pamoja na kujenga uchumi imara unaokabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.  

Alisema Kauli Mbiu ya Wiki ya Sheria mwaka huu (Uwekezaji na biashara:jukumu la Mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji) inawataka wote waliopewa jukumu la kutunga sheria (Bunge), kutekeleza sheria (Serikali)  na jukumu la utoaji haki (Mahakama) kujiuliza endapo wananchi walio wengi ambao ni maskini watanufaika vipi na sheria au taratibu za kimahakama.

“Taratibu za kisheria zinapaswa kuwa na msukumo wa kimapinduzi ili kuwawezesha wananchi kupanda kutoka katika hali duni walizonazo na kufikia mizani sawa na watanzania wenye uwezo wa kiuchumi”, alisema Prof. Juma.

Alisema maonesho ya wiki ya sheria hayana budi kutumika tambua vizuizi na vikwazo vyote vya Sheria na taratibu za utoaji haki vikiwemo vizuizi na vikwazo dhidi ya haki kwa wanyonge. Aliongeza kuwa vikwazo hivi havianzii mahakamani ingawa Mahakama ndio sehemu ya mwisho inapotafutwa haki

“Misingi ya kupata haki lazima ianze mapema wakati wa kutunga Sheria kwa kubeba dhana ya kuwawezesha wananchi walio masikini, Bunge linapotunga sheria lijiridhishe kuwa uwezeshaji ni kiini muhimu katika sheria husika”, alisisitiza.

Akizungumzia umuhimu wa elimu ya sheria kwa wananchi, Jaji Mkuu alisema Mahakama haiwezi kufanikiwa katika kutekeleza jukumu lake la utoaji haki  bila ya wananchi kufahamu Sheria na Kanuni zinazoongoza taratibu za kimahakama. Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ili kupata elimu ya masuala ya kisheria.

Wiki ya Sheria ambayo huambatana na utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi imezinduliwa rasmi leo kwa matembezi yaliyoongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai. Matembezi hayo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wadau wa sekta ya sheria nchini.

 

Comments (0)

Leave a Comment