Post Details

MAHAKAMA SPORTS JABALI, LIMESHINDIKANA

Published By:LYDIA CHURI

  • Yatinga fainali kwa mkwara baada ya kuwakaangiza TPDC

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 27 April, 2022 imetinga fainali kwenye mchezo wa kuvuta kamba wanaume na wanawake katika mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa baada ya kuwapa kipigo kitakatifu TPDC.

Mashindano yaliyozikutanisha timu hizo yalianza majira ya saa moja asubuhi, ambapo TPDC walionekana kuukamia mchezo huku wakihamasishana ili kulisabaratisha Jabali la Mahakama. Hata hivyo juhudi zao hazikuzaa matunda mara baada ya kuangukia pua na kujikaanga kwenye mafuta yao wenyewe.

Ilikuwa Mahakama Sports wanawake waliokuwa wa kwanza kuingia katika mchezo dhidi ya TPDC wanawake ambao ulionekana kuwa mgumu, huku timu zote mbili zikisomana mbinu za uchezaji. Hatimaye Mahakama Sports walifanikiwa kuwango’a wapinzani wao kwenye mzunguko huo.

Mzunguko wa pili haukuwa rahisi kwa timu zote mbili ambapo Mahakama Sports walionyesha ubabe walionao dhidi ya wapinzani wao. Hata hivyo, TPDC walifanikiwa kuchomoza baada ya Mahakama Sports kutereza na kudondoka, hivyo kuwapa nafasi wapinzani wao kuvuta kamba haraka haraka na kupata pointi moja.

Iliwalazimu waamuzi kuchezesha mzunguko wa tatu ili kupata mshindi. Mahakama Sports walitulia, wakajipanga na kwa kutumia mbinu za kimchezo walizokuwa wamefundishwa na Mwalimu Spear Mbwembwe walicharuka kama nyuki na wakafanikiwa kuwakaanga TPDC, ambao hawakuamini macho yao.

Mchezo wa wanaume ulianza kwa ushindani mkubwa huku TPDC wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo walipokutana na Mahakama Sports wanaume wakati wa makundi. Hivyo, TPDC walikamia mchezo huo kwa nia ya kulipiza kisasi.

Hata hivyo, usemi wa Wahenga kuwa Jabali ni Jabali tu uliendelea kujidhihirisha baada ya TPDC kutolewa kamasi na Mahakama Sports wanaume katika mizunguko yote miwili. Ingawa TPDC walijaribu kujitutumua kwa kubadilisha mbinu za uchezaji, juhudi hizo ziligonga mwamba na kuliacha Jabali likiondoka na kamba, huku wao wakiangukia pua bila kitegemea.

Baada ya kumalizika kwa michezo hiyo miwili, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewashukuru kwa mara nyingine tena wachezaji wote kwa mafanikio makubwa ambayo wameyafikia hadi sasa, hususani kufika fainali katika mchezo huo.

 “Ingawa wenzetu walikuwa wametukamia, lakini tumewaonyesha sisi ni nani. Sasa tuna kazi moja tu, nayo nikutembeza vichapo na kubeba makombe yote. Uwezo huo tunao, nia tunayo, twendeni tukamalizie kazi iliyotuleta. Sisi ni Jabali ambalo limeshindikana na halitikisiki,” alisema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mbwembwe amewakumbusha vijana wake kuwa hawana kitu kingine zaidi ya kuzoa makombe yote katika mchezo huo. “Wembe ni ule ule, wameutaka wenyewe na wanataka kuuchezea, lazima uwakate, watake wasitake,” alisema.

Baadaye, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso, ambaye pia ni mlezi wa Timu hiyo, alitembelea kambi ya Mahakama Sports ambapo amewapongeza wanamichezo wote kwa kuendelea kuiheshimisha Mahakama kwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

“Nizipongeze timu zote mbili kwa ushindi huu mlioupata leo. Nimewaona uwanjani mlivyokuwa mnapambana. Ingawa mchezo wa kamba ni kama dakika tano hivi, lakini shughuli yake ni zaidi ya dakika 90. Mmefanya kazi kubwa na hongereni sana. Nizidi kuwatia moyo, tumalizie huu ushindi,” alisema.

Mkurugenzi huyo pia aliwafikishia wachezaji hao salamu kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye ametoa pongezi za dhati kwa mafanikio waliyoyapata na anafuatilia kwa karibu mashindano hayo.

“Kama mlivyoanza mwanzo, endeleeni na jitihada hizo hizo, tumalize vizuri, tuondoke na ushindi na tukawakabidhi viongozi wetu vikombe. Nina uhakika tutachukua makombe yote,” alisema. Kwa upande wao, wachezaji wa timu zote mbili wamemhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa watapambana kwa nguvu zao zote ili kuibuka washindi.

Kikosi kilichoanza kwa upande wa Mahakama Sports wanawake wakiongozwa na mama Mchawi Mwanansolo kilihusisha Stephania Bishobe, Zahara Selemani, Rebecca Mwakabuba, Hadija Mkuvi, Beatrice Dibogo, Jamila Kisusu, Judith Sarakikya, Saraphina Mkumbo, Melina Mwinuka na Namweta Mcharo. Waliokaa benchi walikuwa Mwanabibi Bakari, Lucy Mbwaga, Zuhura Hamza, Scholastica Shemtoi na Josephine Aidani.

Walioanza kwa upande wa Mahakama Sports wanaume chini ya Rajab Mwariko walikuwa Leonard Kazimzuri, Cletus Yuda, Seleman Dimoso, Patrick Nundwe, Denis Chipeta, Frank Lutego, Ashel Chaula, Abdul Mbaraka, Mushi Martin na Moris Magogo. Waliokaa benchi walikuwa Chilemba Chikawe, Issa Kabandika, Philipo Ferdinand, Emmanuel Seshahu na Fred Ndimbo. 

Michezo mingine ya nusu fainali kwa upande wa wanawake iliwakutanisha Uchukuzi ambao waliwatoa kwenye mashindano Tamisemi. Kwa upande wa wanaume, Uchukuzi pia waliwapigisha kwata Mambo ya Ndani. Kwa maana hiyo, Mahakama Sports itakutana na Uchukuzi kwenye fainali.

Mahakama Sports iliingia robo fainali baada ya kushinda mechi zake zote kwenye hatua ya makundi. Mahakama Sports wanaume walimenyana na TPDC na Tanesco, ambao waliingia mitini kwa kuhofia kipigo, huku Mahakama Sports wanawake ikiwatambia Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana na Mahakama Sports ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanansolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa na Tiba Teresia Mogani.

Comments (0)

Leave a Comment