Home / Latest News / PROF. KABUDI AAHIDI KUKISAIDIA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO

PROF. KABUDI AAHIDI KUKISAIDIA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO

Na Ibrahim Mdachi, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameahidi kukisaidia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuwa anatambua mchango wake katika utoaji mafunzo ya Sheria nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria  ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Mahafali ya 18 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Novemba 23 alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa Chuo hiki katika kutoa mafunzo ya sheria kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada na katika kutoa mafunzo endelevu katika fani mbalimbali za sheria.

“Ninaahidi kutimiza wajibu wangu kwa kutoa msaada pale mtakapohitaji na nitakapoona sina budi nitatoa msaada huo hata kama hamjaleta rasmi hitaji lenu kwangu.” Alisema Prof. Kabudi.

Akiendelea kuhutubia hadhara ya Wahitimu, Watumishi wa Chuo na Mahakama Wazazi na Walezi wa wahitimu, Prof. Kabudi aliongeza kuwa wahitimu wa chuo hiki wamekuwa mfano kwa jamii kwa uadilifu na maadili kutokana na malezi wanayopata chini ya usimamizi wa Mahakama ya Tanzania.

Alipongeza Uongozi wa Chuo kwa jitihada unazozifanya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na namna unavyoweza kuzikabili na kuweza kutekeleza jukumu lake la utoaji wa mafunzo sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Sambamba na hayo aliwaasa na kuwasisitizia Wahitimu na juu ya kujiendeleza katika fani ya Sheria ambayo huhitaji kusoma kwani sheria na kanuni hubadilika kila mara na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Mhe. Prof Kabudi aliwataka Wahitimu hao kuendelea kusoma vitabu kwa wingi kwani itawasaidia katika utendaji kazi wao wa kila siku.

 Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji, Prof. Paul Kihwelo alisema kuwa Chuo kimeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa Watumishi wa Mahakama ili kuwajengea uwezo zaidi.

“Kwa kutambua umuhimu wake kwa Mahakama ya Tanzania pamoja na kuwajengea uwezo wa utafiti watumishi wake, Chuo kimeendesha mafunzo yaliyowajumuisha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata mkoani Tabora ili kuwajengea uwezo wa namna wanavyopaswa kusikiliza mashauri katika ngazi zao,” alieleza Mkuu huo wa Chuo. 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika alitaja miongoni mwa mafanikio ya Chuo kuwa ni kuboresha utendaji kazi wa Kurugenzi ya Mafunzo Endelevu ya Kimahakama. 

“Nichukue fursa hii tena kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chuo kutoa shukrani za pekee kwa Mhe. Jaji Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano wanaotoa kwa Uongozi wa Chuo, kutoa kipaumbele kwa shughuli za Chuo hususani kutenga fedha za mafunzo kwa maafisa wa mahakama na wasaidizi wao na kuamua kuwa mafunzo yote ya watumishi wa mahakama yaratibiwe na Chuo,” alieleza Mwenyekiti.

Aliongeza kuwa katika utoaji wa elimu bora  chuoni hapo, Chuo kwa sasa kina jumla ya Wanataaluma (Wahadhiri) Ishirini na Tatu (23) ambao wameendelezwa na kuwezesha Chuo kupata mafanikio ya kitaaluma yaliyotajwa. Miongoni mwa Wanataaluma hao, watano (5) wana Shahada ya Uzamivu na kumi na nane (18) wana Shahada ya Uzamili. Kwa sasa kati ya hao 18 wenye Shahada za Uzamili wawili wanafanya Shahada ya Uzamivu na wapo katika hatua nzuri.

Katika Mahafali hayo, Mhe. Waziri alizindua Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chuo hicho, Mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Mafunzo ‘Training Management Information System (TMIS)’ na Klabu ya utunzaji mazingira ijulikanayo kama ‘IJA Green Club’.