Home / Latest News / MAHAKAMA, TPSF KUWA NA JUKWAA LA PAMOJA KUJADILI CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA

MAHAKAMA, TPSF KUWA NA JUKWAA LA PAMOJA KUJADILI CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA

Na Mary Gwera, Mahakama

Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imepanga kuwa na Jukwaa la pamoja kujadili masuala ya msingi ya biashara yenye lengo la kukuza uchumi wa Taifa.

Akizungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma Novemba 12, Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bw. Salum Shamte alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kukubali pendekezo la kuwa na Jukwaa hilo.

“Jukwaa hili ambalo tumependekeza kufanyika mara nne (4) kwa mwaka litasaidia TPSF na Mahakama ya Tanzania kujadili changamoto kwani kuna Mashauri ya Kibiashara ambayo kimsingi yakimalizwa mapema biashara zitaendelea na hatimaye uchumi utakua,” alisema Bw. Shamte.

Mbali na Jukwaa, Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF pamoja na Wajumbe wa Bodi wa Taasisi hiyo ambao walimtembelea Mhe. Jaji Mkuu kwa lengo la kujitambulisha, aligusia pia juu ya ucheleweshaji wa baadhi ya Mashauri ya Kibiashara Mahakamani.

“Napenda kupongeza jitihada zinazofanywa na Mahakama katika kuendelea na maboresho ya huduma zake, hata hivyo napenda kugusia baadhi ya mashauri ya biashara yanayochukua muda mrefu, hivyo Mhe. Jaji Mkuu tunaomba uliangalie hili kwa jicho ya kipekee,” alieleza Mwenyekiti huyo wa TPSF.

Kwa ujumla ujumbe huo uligusia masuala kadhaa yote yakiwa na lengo la kuboresha na kukuza Sekta ya biashara na uwekezaji nchini ambayo Mahakama pia ina mchango katika kufanikisha hili.

Kwa upande wake Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati ambaye alizungumza kwa niaba ya Mhe. Jaji Mkuu aliujuza ujumbe huo juu ya maboresho mbalimbali ambayo Mahakama inaendelea kuyaboresha mojawapo ikiwa ni matumizi ya TEHAMA.

“Kwa sasa, Mahakama ya Tanzania ina baadhi ya mifumo mbalimbali inayofanya kazi, kama Mfumo wa Utunzaji Takwimu kwa njia ya Kielektroniki (JSDS), ‘e-filling’ na kadhalika, na mingine ipo katika hatua za mwisho kukamilika na pia tutawashirikisha mifumo hii ili muweze kupata uelewa zaidi wa namna inavyofanya kazi,” alisema Mhe. Revocati.

Kwa upande mwingine, Mhe. Msajili Mkuu aliutoa hofu ujumbe huo juu ya kasi ya Mahakama katika kushughulikia mashauri yanayoletwa Mahakamani huku akieleza juu ya Mikakati ya Mahakama katika kukabiliana na mlundikano wa mashauri kwa kila ngazi ya Mahakama.

“Mahakama za Mwanzo tumepanga kesi zisizidi miezi sita (6), Mahakama za Wilaya/Mkoa kesi zisizidi mwaka mmoja na kwa upande wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu kesi zisizidi umri wa miaka miwili (2) Mahakamani,” alifafanua Mhe. Revocati kwa niaba ya Mhe. Jaji Mkuu.