Na INNOCENT KANSHA, SALUM TAWANI-Mahakama, Kondoa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa amewaongoza watumishi wa Mahakama na Wananchi mjini Kondoa katika safari ya mwisho ya Jaji Mwanaisha Athuman Kwariko ambaye amezikwa kwenye makaburi ya familia Bicha Wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma leo tarehe 30 Desemba 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa, amesema kuwa Jaji Kwariko alikuwa mtendaji mzuri na ni miongoni mwa majaji wanawake wachache wa Mahakama ya Rufani ambaye ameonyesha uwezo mkubwa kiutendaji kazi akiwa katika nafasi hiyo, hivyo kutangulia kwake mbele za haki Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amehuzunika sana kupata taarifa za msiba huo pia Taifa limepata pengo katika nafasi yake ya ujaji wa Mahakama ya Rufani.
“Marehemu Kwariko alikuwa Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania aliteuliwa na Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mwaka 2021, Tume hiyo inafanya kazi kwa karibu zaidi na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali. Utendaji wa kazi wa Mhe. Kwariko kama Kamishna wa Tume hiyo kulingana na kama Mwenyekiti wa Tume hiyo alivyoelezea, sisi kama Ofisi tumeguswa na msiba huu mzito na kwa hiyo tunaungana na Mhe. Rais kutoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania, kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na familia kwa ujumla,’’ amesema Waziri Mkuu.
Naye, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa salamu za pole kufuatia kifo hicho, alimuelezea Marehemu Kwariko kama mtumishi wa Umma aliyetekeleza majukumu yake kwa kuwajali wengine, kwa uaminifu na kwa bidii ya hali ya juu na kwamba, mchango wake kwa Taifa hautasahaulika kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya.
“Kuna wakati Rais wa Marekani Abraham Lincoln aliwahi kusema, ubora wa maisha siyo miaka ambayo unaishi duniani ubora wa maisha ni yale unayowafanyia binadamu wenzako ndiyo watu wanakukumbuka zaidi unaweza kukaa miaka kumi au ishirini lakini unaweza kufanya mambo makubwa zaidi ya wale waliojaaliwa uhai mrefu kwa hiyo sisi tunamshukuru Mungu kwa uhai wa Mhe. Kwariko umetusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kuhudumia wananchi hasa katika kutoa haki bila ya upendeleo,’’ amesema Mhe. Prof. Juma.
Vilevile, Jaji kwariko alikuwa Kiongozi katika ngazi ya Familia, Muhimili wa Mahakama na pia kwenye Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania, hivyo basi maeneo yote aliyofanya kazi yanagusa maisha ya mtanzania na ndiyo maana huu ni wakati wa kumshukuru Mwenyezi Mungu akumbuke yote mema ambayo Mhe. Kwariko aliyafanya kwasababu daftari la Mwenyezi Mungu halisahu kitu.
“Binadamu kiuhalisia anaweza kusahau mema lakini daftari la Mwenyezi Mungu halisahau na tunamuombea mema mengine ambayo tumeyasahau aweze kuyajumuisha kwenye daftari lake. Unaweza ukawa binadamu na usiwe na utu, lakini Mhe. Kwariko alikuwa na ubidamu na hii inatokana na salaam mbalimbali ambazo nimekuwa nikizipokea zinazoonyesha kwamba alikuwa na ubinadamu na utu,’’ amesema Jaji Mkuu.
Aidha, Mwenyekeiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania Mhe. Jacobs Mwambegele, amesema kuwa, walikuwa wanamuhitaji sana Jaji Kwariko katika kipindi hiki cha uboreshwaji wa daftari la Kudumu la wapiga Kura kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tume Huru ya Uchaguzi tumempoteza Marehemu Kamishna Kwariko wakati tukiwa katika mzunguko wa nane wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na tukisubiri kuingia katika mzunguko wa tisa utakaohusisha mikoa minne ya Rukwa, Songwe, Njombe na Ruvuma, ilichukua muda kutafakari vipi msiba huu kwa mwenzetu ambae alikuwa nasi bega kwa bega wakati wa Majukumu tunayotekeleza, alitoa ushirikiano mkubwa ambao ndiyo umetufikisha hapa, alihakikisha kuwa, Majukumu ya Tume yanatekelezwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa,’’ amesema mwenyekiti Mwambegele.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Mhe. Barke Mbaraka Sehel, amesema kuwa, Mhe. Kwariko alikuwa mwachama mzuri na hai hivyo Chama kinatoa pole kwa ndugu na jamaa wote na ifahamike kuwa mauti kwa binadamu ni fumbo kubwa ila ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu, kilichobaki ni kumuombea Dua ili kujiandaa na siku ya mwisho kila mmoja wetu atakapoitwa.
Katika mazishi hayo Viongozi mbalimbali wa Mahakama walihudhuria wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Watendaji wa Mahakama, Mahakimu wa ngazi mbalimbali pamoja na Watumishi wa Kada mbalimbali.