tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
MAHAKAMA YA KENYA YAENDELEA KUJIFUNZA; YAIPA KONGOLE MAHAKAMA YA TANZANIA KWA MABORESHO LUKUKI
Post Media
post-media

·       Mada mbalimbali zatolewa

·       Wavutiwa zaidi na maboresho mengi ya TEHAMA nchini hususani uanzishwaji wa 'Judiciary Virtual Situation Room'

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Ujumbe wa watumishi wa Mahakama kutoka nchini Kenya waliopo katika ziara ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho ya huduma za utoaji haki umevutiwa na kupongeza hatua kubwa ya maboresho yaliyopo ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Ikiwa ni siku ya tatu ya ziara ya ujumbe huo leo tarehe 21 Mei, 2025 wamepata fursa ya kutembelea Chumba cha Kusimamia na kuratibu Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakama ya Tanzania (Judiciary Virtual Situation Room) ambapo wamejifunza namna kinavyofanya kazi.

Akitoa taarifa kuhusu namna chumba hicho kinavyofanya kazi, Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock amesema, chumba hicho kinatoa taarifa muhimu za Mahakama ikiwemo taarifa ya idadi ya mashauri yaliyofunguliwa kwa muda husika, mashauri yaliyoamuliwa na kadhalika.

“Uwemo wa chumba hiki na mifumo mingine ya TEHAMA ni dhamira ya dhati waliyo nayo viongozi wetu kuhusu matumizi ya teknolojia, kupitia chumba hiki watumiaji wanaweza kupewa mahitaji yao kwa mujibu wa majukumu yao,” ameeleza Bw. Kalege.

Baada ya kufanya wasilisho kuhusu Chumba hivyo, wajumbe kutoka Mahakama ya Kenya walipata fursa ya kuuliza maswali pamoja na kujadiliana na watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuona jinsi gani na wao wanaweza kuanzisha chumba kama hicho katika Mahakama yao.

Akiwasilisha mada kuhusu Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama (Call Centre), Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Aloyce Katemana amesema Kituo hicho kilianzishwa tarehe 01 Machi, 2022 kwa malengo ya kuimarisha imani ya wananchi na ushirikishwaji wa wadau, kuongeza uwazi juu ya huduma zinazotolewa na Mahakama, kuongeza uwajibikaji wa mfanyakazi wa Mahakama, kuwawezesha wananchi kuzifikia kwa rahisi habari za Mahakama na kwa gharama ya chini.

Mhe. Katemana amesema kuwa, kituo hicho kinapokea aina mbalimbali ya mirejesho kutoka kwa wananchi na wadau kupitia namba ya bure ya 0800750247 huku akitaja mirejesho hiyo kuwa ni pamoja na maoni, malalamiko, maswali na pongezi juu ya huduma za Mahakama.

Naye Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania, Bi. Evetha Mboya amesema kuwa, kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kuanzisha njia nyingine ya kuwasiliana na wananchi ‘WhatsApp Chatbot’ ambayo itamuwezesha mwananchi mwenye shida yote ya Mahakama au taratibu za kisheria kuuliza swali lake na kujibiwa papo hapo kupitia ‘WhatsApp’.

Aidha, mada nyingine iliyotolewa ilihusu ‘Tathmini ya Utendaji kazi kwa Maafisa wa Mahakama kwa utoaji huduma za haki’ ambayo ilitolewa iliwasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Divisheni ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Karol Mashauri.

Mhe. Mashauri amesema kwamba, Miongoni mwa mageuzi ambayo Mahakama ya Tanzania imefanya ni pamoja na uanzishwaji wa Kurugenzi ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi, Mrejesho kwa Umma na Maadili 2014 ambapo moja ya majukumu ya kurugenzi hiyo ni  kufuatilia upimaji wa utendaji wa Maafisa wa Mahakama.

Ameongeza kuwa, Mahakama imeweka viwango vya utendakazi, vya ubora na kiasi ili kupima na kutathmini utenda kazi halisi wa Maafisa wa Mahakama kulingana na mchango wao katika malengo yake.

“Kabla ya tathmini ya utendakazi ya 2015 ilikuwa ikifanywa kwa kuzingatia fomu za siri za utendaji wa kibinafsi. Mbinu hiyo ilikosa uwajibikaji na uwazi kwani mthamini hakujua vigezo vilivyotumika wala matokeo ya tathmini,” ameeleza Mhe. Mashauri na kuongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwaka 2015 Mahakama ilipitisha Mfumo wa Tathmini ya Utendaji Kazi kwa Maofisa wa Mahakama (JOPRAS) kama nyenzo muhimu katika tathmini ya utendaji kazi wa maafisa wa Mahakama.

Wasilisho lingine limetolewa kuhusu Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania (Judiciary Square) na Msanifu Majengo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Aikamiriam Kileo ambapo ameueleza ujumbe huo kuwa, jengo hilo lina mita za mraba 63,244 na lina jumla ya sakafu tisa na mbawa (wings) tatu.

Amesema usanifu wa kimahakama ‘Juditecture’ umezingatiwa katika jengo hilo ambapo amefafanua kuwa neno “Judi”- ikiashiria utawala, uwajibikaji na utoaji haki kwa wakati, "Tec"- inaashiria teknolojia ya hali ya juu ambayo imejumuishwa katika muundo wa jumla wa jengo na "Ture" -inaashiria usanifu na dhana ya kubuni ambayo imetumika kujenga jengo.

Ameongeza kuwa, jengo hilo lina jumla ya vyumba tisa vya Mahakama, kumbi ambazo zimeundwa kuchukua hadi watu 100, 60 hadi 70, huku chumba cha Mahakama kilicho katika sehemu ya kati kinaweza kuchukua zaidi ya watu 30.

Akiongezea katika wasilisho hilo, Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso amewaonesha wageni hayo miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo Mahakama imejenga kwa kutumia fedha za ndani. Miradi hiyo ni pamoja na nyumba 48 za makazi ya Majaji, ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu na miradi mingine.

Baada ya kupata mawasilisho hayo, wajumbe hao kwa nyakati tofauti wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa jitihada kubwa za maboresho ambayo imefanya na kuahidi kutekeleza waliyojifunza ili kuboresha huduma za utoaji haki nchini Kenya.

Aidha, kabla ya kupata mawasilisho hayo, Watumishi hao kutoka Mahakama ya Kenya walianza kwa kutembelea Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na kufurahishwa na uzuri wa ofisi hiyo.