tz_coa
The United Republic Of Tanzania
The Judiciary Of Tanzania
Timely And Accessible Justice To All
Post Details
JAJI KIONGOZI AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA MAHAKAMA KAZI
Post Media
post-media

Na INNOCENT KANSHA - Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani leo tarehe 23 Aprili, 2025 amefungua Kongamano la mafunzo ya Usalama Mahala pa Kazi kati ya Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Taasisi ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) pamoja taasisi za kiserikali ambazo ni wadau wa Mahakama Kazi.  

Kongamano la mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa jengo la OSHA limebeba Kauli mbiu maalum kwa ajili ya kutafakari na kubadilishana uzoefu juu ya “Nafasi ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) Mahali pa Kazi (Mapinduzi na Fursa)”

“Kwa kuwa nyinyi ni wadau wa utoaji haki na huduma katika sekta mbalimbali, mafunzo haya ni muhimu sana kwenu. Matumizi ya akili unde yamedhihirika kuleta mafaniko na ufanisi katika sekta mbalimbali duniani. Tanzania sio kisiwa na hivyo hatuwezi kubaki nyuma. Ni lazima nchi yetu iendane na mabadiliko chanya ya kiteknolojia na utendaji yanayotokea kote ulimwenguni. Mafunzo haya yanatoa fursa ya kupiga hatua muhimu katika safari ya uboreshaji wa mifumo na utendaji kazi wetu,”. amesisitiza Jaji Kiongozi Mhe. Dkt. Siyani.

Jaji Siyani amendelea kwa kusema, akili unde ni matokeo ya kuongezeka kwa utafiti na kukua kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kiasi cha kuwezesha kutengenezwa kwa mifumo yenye utambuzi wa mambo mfano wa binadamu. Viwango vya usahihi vinavyozidi kuongezeka kadri ya mifumo hiyo inavyotumiwa na muda mfupi ambao mifumo hiyo inatumia kutekeleza kazi mbalimbali, vinaongeza hamasa na kuonyesha umuhimu wa matumizi yake. 

Mhe. Dkt. Siyani ameongeza kuwa, matumizi ya akili unde yanazaa fursa na changamoto mbalimbali kupitia mafunzo washiriki watapata nafasi ya kupitia faida na hasara za matumizi ya akili unde. Faida za matumizi ya akili unde ni nyingi na kama nilivyotangulia kusema ni pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kurahisha tatifi mbalimbali, kutafsiri lugha, kupunguza makosa ya kibinadamu, pamoja na kuokoa muda na gharama.

“Aidha, akili unde inaweza kuwapa wafanyakazi muda zaidi wa kufikiria mambo yenye tija kubwa zaidi kwa taasisi na kutunza kumbukumbu muhimu kazini, mambo yanayoweza kukuza ugunduzi na ushindani,” amesema Mhe. Dkt. Siyani.

Aidha, Jaji Kiongozi ameongeza kuwa, akili unde haikuja na faida pekee bali pia, inazo changamoto zake. Moja ya changamoto hizo ni hofu ya watu kudhani kuwa watapoteza kazi zao ikiwa akili unde itaachwa kuendelea kukua na kufanya kazi ambazo kimsingi zinafanywa na binadamu. Hofu nyingine ni kupotea kwa usiri na uwezekano wa taarifa muhimu kudukuliwa.

“Ni muhimu kujua kuwa katika dunia yetu ya sasa matumizi ya akili unde hayakwepeki. Iko haja ya kujadili na kuhakikisha kwamba kila mmoja anajiongezea thamani kama mfanyakazi ili kufikia viwango na kufanya kazi ambazo haziwezi kufanywa na akili unde, lakini pia kuhakikisha kuwa mifumo yetu imewekewa ulinzi wa kutosha kudhibiti matumizi mabaya ya akili unde kwa ajili ya udukuzi wa taarifa,” amesema Jaji Siyani.

Vilevile, Mhe. Dkt. Siyani amesema kwamba, uzoefu watakaoupata washiriki wa mafunzo hayo, utawapa jukumu la kuhakikisha kuwa matumizi ya akili unde yanawasaidia kuboresha utendaji kazi kama mtu mmoja mmoja na ufanisi wa taasisi. Ni matumaini ya Mahakama na taasisi zingine zinazoshiriki mafunzo ya akili unde yatawapa pia ujuzi wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na maendeleo ya teknolojia katika utendaji kazi.  

Aidha, Jaji Kiongozi akatoa rai kwa washiriki wa mafunzo kutumia nafasi ya mafunzo hayo ipasavyo kubadilishana uzoefu, kujielimisha, na kutoa maoni ya namna ya kuboresha utendaji wa kazi, lakini pia sheria na sera zinazosimamia matumizi ya akili unde pamoja na usalama na afya kwa watumishi kwa ajili ya kulinda maslahi ya wafanyakazi.

Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo Mhe. Dkt. Siyani  ameushukuru uongozi wa OSHA kwa kutambua uhitaji wa mafunzo hayo kwa watumishi wa umma na kukubali kuwezesha kufanyika kwake kwa mara ya pili jijini Dodoma.

“Ni rai yangu kuwa ushirikiano huu baina ya OSHA kama mdau wa Mahakama uendelezwe ili kuwapa watumishi wa umma wakiwemo wale wa Mahakama fursa ya kupata elimu na kubadilishana uzoefu kupitia mijadala mbalimbali itakayoongeza tija kazini...

Aliwashukuru wafanyakazi wa Mahakama na wa Taasisi nyingine za umma kwa kutenga muda na kuja kushiriki mafunzo haya muhimu. Ni matarajio yangu kuwa baada ya mafunzo haya, washiriki watarejea katika maeneo yao ya kazi wakiwa na maarifa mapya yatakayowasaidia kuongeza tija, kuboresha utoaji wa haki na huduma bora kwa wananchi,” ameongeza Jaji Siyani.