Home / News / Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama wasaini mikataba ya kazi

Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama wasaini mikataba ya kazi

1Wakuu Wa Idara na Vitengo wa Mahakama ya Tanzania leo  wamesaini Mikataba ya Kazi kwa ajili utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama.

Zoezi hili fupi la utiaji sahihi limefanyika mapema leo Februari 24, katika Ukumbi wa Maktaba wa Mahakama ya Rufani (T) ikishuhudiwa na Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama.

Katika muendelezo wa utekelezaji wa Mpango Mkakati huo, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kufikia malengo yaliyowekwa katika mpango huo wenye lengo kuu la kuboresha huduma ya upatikanaji haki nchini.

Zoezi hilo maalum la utiaji sahihi Mikataba ya kazi limefanyika kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wanaosimamia utekelezaji wa malengo ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania 2015-2020.

Akizungumzia zoezi hili muhimu, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Utekelezaji wa Shughuli za Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama, Mhe. Zahra Maruma alisema kuwa Mahakama imejiwekea mfumo wa utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho kwa Mfumo wa Matokeo Makubwa sasa, (BRN).

“Zoezi lililofanyika leo linalenga katika upimaji wa Viashiria muhimu tulivyokubaliana katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama,” alieleza Mhe. Maruma.

Wakuu wa Idara na Vitengo waliokabidhiwa Mikataba hiyo ni Msajili-Mahakama ya Rufani (T), Msajili-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mkurugenzi wa Utawala, Menejimenti ya Rasilimali Watu, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri, Mkurugenzi Msaidizi- Ukaguzi, Maadili na Malalamiko na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano.

Wengine ni Kitengo cha Usimamizi wa Majengo na Idara ya TEHAMA.

Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama vilizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, Septemba 21, 2016.