Home / News / Ujumbe wa Benki ya Dunia Wahitimisha Ziara yake kwa Mahakama: Waisifu Mahakama kwa maboresho

Ujumbe wa Benki ya Dunia Wahitimisha Ziara yake kwa Mahakama: Waisifu Mahakama kwa maboresho

Na Mary Gwera

Mtaalamu Mwandamizi wa Maboresho ya Utumishi wa Umma kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Waleed Malik amesifu Mahakama ya Tanzania kwa kasi nzuri inayoenda nayo katika utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama pamoja na Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015/16-2019/2010) wa Mahakama.

Bw. Malik aliyasema hayo mapema Desemba 11 ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Kitengo cha Usimamizi wa Mradi wa Maboresho ya Mahakama (JDU), katika kikao cha Majumuisho baada ya ziara ya Ujumbe Benki ya Dunia (WB) na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.

“Kufuatia  ziara tuliyofanya  ya kukagua na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama, tumeona mnaendelea vizuri na ninapenda kuwapongeza kwa ushirikiano wenu, kwani Mahakama ni moja kati ya Taasisi zinazokwenda vizuri katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia,” alieleza Bw. Waleed.

Mbali na Pongezi, Bw. Waleed aliwasihi Viongozi wa Mahakama kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuwapa mafunzo Watumishi wake juu ya matumizi ya TEHAMA yatakayowezesha maboresho yanayofanyika kutekelezeka vizuri.

“Ni muhimu kuwapa mafunzo ya TEHAMA Watumishi wa Kada mbalimbali wa Mahakama ili Mifumo ya Kiielektroniki itakayowekwa iweze kutumiwa na Watumishi bila shida yoyote,” aliongeza Mtaalam huyo kutoka Benki ya Dunia.

Aliongeza pia juu ya umuhimu wa kuimarisha mawasiliano/utoaji taarifa kwa jamii ili wananchi waweze kujua juu ya maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Akiongea kwa niaba ya Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mtendaji Mahakama ya Rufani, Bw. Sollanus Nyimbi aliahidi kufanyia kazi maelekezo na changamoto zilizoibuliwa kutoka ujumbe wa Benki ya Dunia ili kuendana na matakwa ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama.

“Tunashukuru kwa pongezi, lakini pia tunaahidi kufanyia kazi yale yote mliyoyaibua lengo likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki nchini,” alisema Bw. Nyimbi.

Ujumbe wa Benki ya Dunia uliwasili  nchini Desemba 04, lengo likiwa ni kukagua utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama pamoja na Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015/16-2019/2010) wa Mahakama.

Ujumbe huo pia ulipata wasaa wa kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilichojengwa eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kawe pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni.