Home / News / Toeni huduma bila kujikweza au kujitukuza

Toeni huduma bila kujikweza au kujitukuza

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wote nchini wametakiwa kujishusha pindi wanapotoa huduma za utoaji haki kwa wananchi wanaofika Mahakamani ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Mhimili huo yanayoendelea.

Akifungua kikao kazi cha Watendaji na Wataalamu wa Mahakama kutathmini Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka  Mitano (2015/16- 2019/20) na Utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Utoaji huduma za Mahakama unaofanyika mjini Arusha, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Watumishi hao kuacha tabia binafsi ikiwemo kujikweza zinazoweza kuwa kikwazo katika maboresho ndani ya mhimili huo.

“Kila mmoja ni kiongozi na ni lazima tujishushe wote tulingane kwa lengo moja la maboresho ndani ya Mhimili wa Mahakama”, alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Akitoa mfano wa kujishusha na kutojitukuza, Jaji Mkuu alimnukuu Mwandishi wa kitabu kiitwacho “The Making of Tanganyika”, Judith Listowel ambaye anazungumzia kutojitukuza kwa Mwalimu wakati wa Harakati za kupigania Uhuru. Kwa mujibu wa kitabu hicho, Mwalimu Nyerere alijiuliza ni kwa namna gani angeweza kutumikia nchi yake kwa uaminifu na weledi bila kujidai na kujitukuza yeye binafsi.

Akizungumzia Maboresho, Jaji Mkuu alisema mafanikio ya maboresho yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano ndani ya Mhimili wa Mahakama na pia ushirikiano wa wadau na wananchi ambao wako nje ya Mhimili huo.

Alisema Mradi wa Maboresho ya Mahakama unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia unatajwa  kuwa mfano katika bara la Afrika na kwamba mradi huu unatumiwa na Benki ya Dunia kama mfano wa Mhimili kuwa na uwezo wa ndani wa kufanya maboresho ya huduma ya utoaji haki.

Aliwataka watumishi wa Mahakama kuwa darasa zuri la Mradi wa Maboresho ya huduma kwa nchi nyingine za bara la Afrika kwa kuwa nchi hizo zinasubiri mafanikio ya Mradi huo ili nazo zianzishe kwenye nchi zao.

Aidha, Jaji Mkuu amesema kiongozi yeyote wa Mahakama atakayechelewesha upatikanaji wa nakala za hukumu atachukuliwa hatua za kinidhamu. Akiwa kwenye ziara ya kikazi Mahakama Kuu kanda ya Tabora hivi karibuni, Jaji Mkuu aliwaagiza Mahakimu wote nchini kutoa bure nakala hizo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga amewataka Watendaji na Wataalamu wengine wa Mahakama kufanya kazi kwa ushirikiano lengo likiwa kujenga Taasisi imara.

“Mahakama ina jukumu kubwa la kufanya maboresho katika kazi zake za kila siku, hivyo ni vyema kushirikiana ili kufikia azma” alisema Mtendaji Mkuu.

Aidha; Mtendaji Mkuu alisema kuwa suala la maboresho ya Mahakama linatakiwa kueleweka kwa Watendaji na Watumishi wote wa Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani.

Kikao kazi hicho kilichofunguliwa rasmi na Mhe Jaji Mkuu mapema Machi 08, kimehusisha Wakurugenzi, Manaibu Wasajili, Mahakimu pamoja  Watendaji wa Mahakama nchini kimelenga kufanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020) pamoja na Mradi wa maboresho ya Huduma za Mahakama.