Home / Job / TANGAZO: YAH: NAFASI ZA KAZI YA UDALALI

TANGAZO: YAH: NAFASI ZA KAZI YA UDALALI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAMAHAKAMA

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI

Mahakama ya Tanzania inapenda kuutangazia umma kwamba kuna nafasi za kazi za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama watakaofanya kazi katika Mikoa mbalimbali Tanzania Bara. Kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na ya 6 ya Kanuni za Madalaliwa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na. 363 za Mwaka 2017(The Court Brokers and Process Servers (Appointment Remuneration and Discipline) Rules, GN No. 363 of 2017), Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kuteua Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wenye sifa kama zilivyoainishwa hapa chini.

 1. Dalali wa Mahakama.
 • Sifa za Waombaji.

Mwombajiwa kazi yaUdalali wa Mahakama anapaswa kuwana sifa zifuatazo:-

 • Raia na Mkazi wa Tanzania mwenye umri wa utu uzima.
 • Mkurugenzi wa Kampuni iliyosajiliwa Tanzania au Mwendesha Mnada Mshirika katika Taasisi ambayo imesajiliwa na kupewa Leseni chini ya Sheria ya Waendesha Minada (The Auctioneers Act No. 6 Of 1928 Cap. 227).
 • Awe na Elimu ya Kidato cha Nne na kuendelea na awe na uwezo kuzungumza Kingereza na Kiswahili kwa ufasaha.
 • Awe amehudhuria mafunzo ya majukumu ya Madalali wa Mahakama yanayotolewa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) na kutunukiwa Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence).
 • Awe anafahamu kikamilifu Kanuni za utekelezaji kama zilivyoainishwa na Sheria ya mwenendo wa Madai na Sheria nyingine husika.
 • Awe ni mtu mwenye tabia njema na Muadilifu wa kiwango cha juu.
 • Awe ni mtumwenye msimamo mzuri wa kifedha.
 • Awe na Kituo au ghala la kutosha kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa kwa ajili ya usalama.
 • Awe amelipa ada ya maombi ya kiwango cha Shilingi 250,000/= ambayo haitarejeshwa.

 

 • Kazi za Kufanya.

Kutekeleza tuzo na amri za Mahakama zilizotolewa ndani ya mamlaka yake ambazo zinajumuisha:-

 • Kukamata na kuuza mali za Mshindwa tuzo (Judgment Debtor). Aidha, utekelezaji huo wa amri au tuzo zinazotolewa na Mahakama lazima uzingatie Sheria ya mwenendo wa Madai na Sheria nyingine husika.
 • Kutekeleza amri za kuondosha mali, vitu au watu (Eviction Orders).
 • Kutekeleza amri nyingine zozote zitolewazo na Mahakama.
 • Kuandaa na kuwasilisha taaarifa ya namna utekelezaji ulivyofanyika kwa Mahakama iliyotoa amri.
 • Kutekeleza maelekezo mengine yoyote yatakayotolewa na Mahakama.
 • Ada, gharama na posho za Madalali wa Mahakama.

Ada, gharama na posho atakayolipwa Dalali wa Mahakama kutokana na kazi atakayofanya ni kama zilivyoainishwa katika Kanuni ya 27 na 28 ya Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 363 la mwaka 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment Remuneration and Discipline) Rules, GN No. 363 of 2017).

 1. Msambaza Nyaraka za Mahakama.
 • Sifa za Waombaji.
 • Raia na Mkazi wa Tanzania mwenye umri wa utu uzima.
 • Awe ana Leseni na kwamba tayari kujisajili kwa ajili ya kupata Leseni ya kufanya kazi ya Msambaza Nyaraka za Mahakama.
 • Awe na Elimu ya Kidato cha Nne na kuendelea na awe na uwezo wa kuzungumza Kingereza na Kiswahili fasaha.
 • Awe amehudhuria mafunzo ya majukumu ya Msambaza Nyaraka za Mahakama yanayotolewa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) na kutunukiwa Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence).
 • Awe anafahamu kikamilifu Kanuni za Usambazaji Nyaraka za Mahakama kama zilivyoainishwa na Sheria ya mwenendo wa Madai na Sheria nyingine husika.
 • Awe amelipa ada ya maombi ya kiwango cha Shilingi 30,000/= ambayo haitarejeshwa.

 

 • Kazi za kufanya.

Kusambaza nyaraka za Mahakama zinazotokana na mwenendo wa Mashauri na zinazotolewa nje ya mwenendo wa Mashauri ambazo zinajumuisha:-

 • Wito wa kuitwa Shaurini, taarifa, nakala za Hukumu, nakala za Maamuzi, tuzo au amri.
 • Taarifa ya uteuzi wa Dalali wa Mahakama.
 • Nyaraka nyingine zozote zitakazotolewa na Mahakama.

 

 • Ada, gharama na posho za Wasambaza Nyaraka za Mahakama.

Ada, gharama na posho atakazolipwa Msambaza Nyaraka za Mahakama ni kama zilivyoainishwa katika Kanuni ya 30 na 31 ya Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 363 la Mwaka 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment Remuneration and Discipline) Rules, GN No. 363 of 2017).

Barua zote za maombi ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama zitumwe/ziwasilishwe kwa Katibu wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kupitia kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi (Mkoa) ambapo ndio Mkoa ambao Dalali wa Mahakakama au Msambaza Nyaraka za Mahakama anapotarajia kufanyia kazi. Aidha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi (Mkoa) ana wajibu wa kuwasilisha taarifa ya siri ya Mwombaji kazi ya Dalali wa Mahakama na Msambazaji Nyaraka za Mahakama kwa Katibu wa Kamati wa Uteuzi na Nidhamu ambaye ni Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania.

Barua ya maombi ya Dalali wa Mahakama iambatishwe na:-

 • Kivuli cha Cheti cha Elimu ya Kidato cha Nne na kuendelea.
 • Kivuli cha Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence) cha majukumu ya Dalali wa Mahakama kilichotolewa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA).
 • Ufupisho wa taarifa za mwombaji (CV).
 • Kivuli cha Cheti cha kuzaliwa au kitambulisho cha Uraia.
 • Picha mbili za rangi (Passport size) zilizopigwa hivi karibuni.
 • Barua ya utambulisho ya Benki kuhusu Akaunti ya Mwombaji.
 • Fomu ya Maombi ya Udalali (Fomu Na. 3) iliyojazwa kikamilifu.
 • Fomu ya Wadhamini wawili wa Muombaji (Fomu Na. 5) yenye jumla ya kiwango cha udhamini kisichopungua Milioni mia nne (400,000,000/=).
 • Leseni ya Biashara kutoka katika Halmashauri ya Jiji, Mji au Manispaa.
 • Barua ya utambulisho juu ya tabia ya Mwombaji kutoka kwa watu wanaoaminiwa.
 • Nakala ya hati ya Bima ya moto, majanga na wizi ambayo ni hai kwa mujibu wa Sheria au ahadi ya maandishi ya kukata Bima hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Dalali wa Mahakama.
 • Nakala ya Cheti cha usajili wa Kampuni ambayo Mwombaji ataitumia katika kazi ya Udalaliwa Mahakama au Leseni ya Udalali wa Kawaida (Auctioneers’ General License).
 • MEMART (Memorandum and Articles of Association) ya Kampuni itakayotumika katika kazi ya Udalali.
 • Nakala ya uthibitisho wa malipo ya Kodi (TIN).
 • Taarifa ya Benki ya miezi kumi na miwili (12) ya hivi karibuni inayoonesha uwezo wa Kifedha wa Kampuni itakayotumika au uwezo wa Mwombaji.
 • Hati ya kubadilisha jina (Deed Poll) iwapo kuna tofauti ya majina katika nyaraka zitakazotumika katika maombi ya Mwombaji.
 • Uthibitisho wa umiliki wa Ofisi, yadi na ghala la kuhifadhia bidhaa au mkataba wa upangishaji.

Barua ya maombi ya Msambaza Nyaraka za Mahakama iambatanishwe na:-

 • Kivuli cha Cheti cha Elimu ya Kidato cha Nne na kuendelea.
 • Kivuli cha Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence) cha majukumu ya Msambaza Nyaraka za Mahakama kilichotolewa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA).
 • Ufupisho wa taarifa za mwombaji (CV).
 • Kivuli cha Cheti cha kuzaliwa au kitambulisho cha Uraia.
 • Picha mbili za rangi (Passport size) zilizopigwa hivi karibuni.
 • Fomu ya Maombi ya Msambaza Nyaraka za Mahakama (Fomu Na. 4) iliyojazwa kikamilifu.
 • Leseni ya Biashara kutoka katika Halmashauri ya Jiji, Mji au Manispaa au ahadi ya kuwa tayari kukata Leseni hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Msambaza Nyaraka za Mahakama.
 • Fomu ya Wadhamini wawili wa Muombaji (Fomu Na. 5) yenye jumla kiwango cha udhamini kisichopungua Milioni mia nne (400,000,000/=).
 • Nakala ya uthibitisho wa malipo ya Kodi(TIN).
 • Hati ya kubadilisha jina (Deed Poll) iwapo kuna tofauti ya majina katika nyaraka zitakazotumika katika maombi ya Mwombaji.

Fomu zote za maombi ya Udalali wa Mahakama na Wadhamini wake na Wasambaza Nyaraka za Mahakama zinapatikana katika Ofisi zote za Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi (Mkoa) Tanzania Bara na Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, DAR ES SALAAM.

Mwisho wa kupokea maombi ni tarehe 27/07/2018 saa 9:30 alasiri.

Mwombaji wa nafasi ya Dalali wa Mahakama na Msambaza Nyaraka za Mahakama aandaye nakala tatu (3) na atume maombi yake kwa njia ya Posta (E.M.S) au kwa Mkono na kuwasilishwa kwa Katibu, Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, Mahakama Kuu, S.L.P 9004, DAR ES SALAAM.

Imetolewa na:-

 

KATIBU

KAMATI YA UTEUZI NA NIDHAMU YA

MADALALI WA MAHAKAMA

NA WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA