Home / Latest News / TANGAZO LA KUHUISHA VYETI VYA UDALALI WA MAHAKAMA

TANGAZO LA KUHUISHA VYETI VYA UDALALI WA MAHAKAMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAHAKAMA

TANGAZO LA KUHUISHA VYETI VYA UDALALI WA MAHAKAMA

A. UTANGULIZI
Mahakama ya Tanzania inapenda kuutangazia umma kuwa Madalali wote wa Mahakama walioteuliwa kufanya kazi za Udalali wa Mahakama katika Mikoa mbalimbali Tanzania Bara Vyeti vyao vya Udalali wa Mahakama kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (6) ya Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na. 363 za Mwaka 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN No. 363 of 2017), vitafikia ukomo tarehe 31 Januari, 2019. Hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni hizo (Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na. 363 za Mwaka 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN No. 363 of 2017), Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kuhuisha Vyeti vya Madalali wa Mahakama. Kwa hiyo, kwa kuzingatia Kanuni tajwa hapo juu Madalali wote wa Mahakama wanapaswa kuhuisha Vyeti vyao katika kipindi cha miezi mitatu (3) kabla ya kufikia ukomo wake.

B. SIFA ZA DALALI WA MAHAKAMA
Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama haitahuisha Cheti cha Dalali wa Mahakama endapo atakuwa ameshindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Kanuni ili kuhuisha Cheti cha Udalali wa Mahakama na pia ikithibitika kuwa amekiuka taratibu na maadili ya utendaji kazi ya Udalali wa Mahakama na kukutwa na sifa kama zilivyoainishwa katika Kanuni ya 13 (1) ya Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na. 363 za Mwaka 2017 (The Court Brokers and Process Servers (Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN No. 363 of 2017).

C. NAMNA YA KUFANYA MAOMBI
Barua zote za maombi ya kuhuisha Vyeti vya Udalali wa Mahakama zitumwe kwa Katibu wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama ambaye ni Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi katika Mkoa husika. Aidha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ana wajibu wa kukagua ofisi ya Dalali, Yadi pamoja na Ghala la Mwombaji na kuandaa taarifa ya siri ya kazi ya Udalali wa Mahakama itakayoainisha pamoja na mambo mengine; utendaji kazi, uwezo wa kufanya kazi, nidhamu, maadili na mwenendo wa Dalali wa Mahakama na kuiwasilisha kwa Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania.

Barua ya maombi ya Udalali wa Mahakama iambatishwe na:-
(i) Kivuli cha Cheti cha Dalali wa Mahakama kinachoisha muda wake.
(ii) Ufupisho wa taarifa za mwombaji (CV). (Taarifa isiwe na “Referees” ambaye ni ndugu, jamaa au rafiki mwenye uhusiano wa karibu na mwombaji).
(iii) Kivuli cha Cheti cha kuzaliwa au kitambulisho cha Uraia.
(iv) Picha mbili za rangi (Passport size) zilizopigwa hivi karibuni.
(v) Fomu ya Maombi ya Udalali (Fomu Na. 6) iliyojazwa kikamilifu.
(vi) Fomu ya Wadhamini wawili wa Muombaji (Fomu Na. 5) yenye jumla ya kiwango cha udhamini kisichopungua Milioni mia nne (400,000,000/=).
(vii) Leseni ya Biashara kutoka katika Halmashauri ya Jiji, Mji au Manispaa.
(viii) Barua ya utambulisho juu ya tabia ya Mwombaji kutoka kwa watu wanaoaminiwa. (Barua isiandikwe na ndugu, jamaa au rafiki mwenye uhusiano wa karibu na mwombaji).
(ix) Nakala ya hati ya Bima ya moto, majanga na wizi ambayo ni hai kwa mujibu wa Sheria au ahadi ya maandishi ya kukata Bima hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Dalali wa Mahakama.
(x) Nakala ya Cheti cha usajili wa Kampuni ambayo Mwombaji ataitumia katika kazi ya Udalali wa Mahakama au Leseni ya Udalali wa Kawaida (Auctioneers’ General License).
(xi) MEMART (Memorandum and Articles of Association) ya Kampuni itakayotumika katika kazi ya Udalali.
(xii) Nakala ya uthibitisho wa malipo ya Kodi (TIN).
(xiii) Taarifa ya Benki ya miezi kumi na miwili (12) ya hivi karibuni inayoonesha uwezo wa Kifedha wa Kampuni itakayotumika au uwezo wa Mwombaji.
(xiv) Hati ya kubadilisha jina (Deed Poll) iwapo kuna tofauti ya majina katika nyaraka zitakazotumika katika maombi ya Mwombaji.
(xv) Uthibitisho wa umiliki wa Ofisi, yadi na ghala la kuhifadhia bidhaa/vitu au mkataba wa upangishaji.

D. MAELEZO MUHIMU
Fomu zote za maombi ya Udalali wa Mahakama na Wadhamini wake zinapatikana katika Ofisi zote za Mahakamu Wakazi Wafawidhi wa Mikoa, Tanzania Bara na Ofisi ya Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania, DAR ES SALAAM.

Maombi yote ya kuhuisha Vyeti vya Udalali wa Mahakama yatashughulikiwa ndani ya miezi miwili (2) tokea tarehe ya kuwasilisha maombi. Aidha, Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania kabla ya kuwasilisha maombi kwa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama atatoa orodha ya Madalali wote wa Mahakama walioomba kuhuisha Vyeti vyao katika Magazeti yanayosomwa kwa wingi hapa Nchini na katika tovuti ya Mahakama (www.judiciary.go.tz) ili kupata maoni kutoka kwa wateja, wadau na wananchi kwa ujumla juu ya utendaji kazi, uwezo wa Dalali kiutendaji, nidhamu, maadili na mwenendo wa Dalali wa Mahakama. Maoni yanaweza kutumwa kupitia anuani ya baruapepe (hcmainregistrydsm@judiciary.go.tz) au kwa anuani ya Posta – Ofisi ya Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mwombaji wa kuhuisha Cheti cha Udalali wa Mahakama atakayefanikiwa kuhuisha Cheti chake atapaswa kulipa ada ya kiasi cha Shilingi laki mbili (Tsh. 200,000/=) ikiwa ni gharama ya malipo ya Cheti cha Udalali wa Mahakama.

Mwombaji wa kuhuisha Cheti cha Udalali wa Mahakama anapaswa kuandaa nakala tatu (3) na kutuma maombi yake kwa njia ya Posta (E.M.S) au kwa Mkono na kuwasilishwa kwa Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania, 22 Barabara ya Kivukoni, S.L.P 9004, 11496 DAR ES SALAAM.

Imetolewa na:-

M.J. Chaba
Kny: MSAJILI
MAHAKAMA KUU YA TANZANIA