Home / News / Taasisi ya Waamuzi Tanzania

Taasisi ya Waamuzi Tanzania

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.  Mohamed   Chande Othman, amewataka  wajumbe wa Taasisi ya Waamuzi Tanzania, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma  yao ili kuhakikisha kwamba migogoro ya masuala ya ujenzi na biashara inashughulikiwa kwa wakati na nidhamu.

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania  wakati akifungua mkutano mkuu wa saba  wa Taasisi ya Waamuzi Tanzania uliofanyika jana jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mkutano wa Luther House.

Katika mkutano huo, aliwaagiza  wajumbe wa taasisi hiyo, kuhakikisha migogoro ya kibiashara katika Mahakama ya Biashara inapatiwa ufumbuzi kwa muda  muafaka kwa kuwa kufanya hiyo kutawezesha  mazingira ya uwekezaji kuendelea kuwa  rafiki na salama  nchini.

Taasisi-Maamuzi

Pia aliwataka wajumbe wa taasisi hiyo wanapofanya kazi hizo kuzingatia suala  la utoaji haki kwa pande zote mbili.

“Suala la  kuzingatia maadili ni visiyokwisha tutaendelea kupambana nalo ili tuweze kuwa na waamuzi wachache wenye maadili, alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Waamuzi Tanzania, Kesogukewele Msita alizitaja   changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali.

Taasisi hiyo ina wajumbe 168 ambao ni mawakili wanasheria, wengine wanatoka Mahakama  mbalimbali, Majaji, Wahandisi na wapima  ramani na wasanifu majengo.

Aliongeza kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wameshughulikia migogoro 9 na kwa kipindi cha mwaka huu wamepokea migogoro 32 ambayo iko katika hatua mbalimbali. Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka  1999.

Katika mkutano mambo yaliyojadiliwa ni Mpango Mkakati wa taasisi hiyo wa  mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 na  kufanyika kwa uchaguzi  wa wajumbe wa kamati tendaji.

Wajumbe hao

Aidha katika   hata nyingine Mhe. Jaji Mkuu amesema kwamba rasimu ya kwanza  ya kanuni ya Sheria ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imeshasambazwa kwa wadau ambao ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Waendesha Mashitaka nchini(DPP), Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Chama cha Wanasheria(TLS na Chama cha Wanasheria Wanawake  Tanzania (TAWLA) ili waweze kutoa maoni yao na wamepewa muda wa wiki moja.

Aliongeza kwamba wataichapisha katika gazeti la Serikali na utaratibu wa ufunguaji wa Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Alisema vyombo vya habari vitaalikwa siku itakapokamilika ili chombo hicho kiweze kufanya kazi.

Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza vita ya rushwa na uhujumu uchumi ni ya kila Mtanzania, si ya Mahakama pekee kwa kuwa ni chombo chenye majukumu ya kusimamia sheria.

Taasisi-Maamuzi2

Alifafanua  kwamba  Mahakama hiyo itakapoanza kutakwepo na ujipimaji wa utendaji kazi wake baada ya miezi sita au mwaka kwa ajili ya  kuangalia uendeshaji wake, ili tuweze kuendesha katika mikoa mingine kama kutakuwa na kesi  zinazohusiana na masuala hayo, mfano kwenye mikoa ya Arusha na Mwanza.

Mwisho.