Home / News / Rais Dkt. John Magufuli amuapisha Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania

Rais Dkt. John Magufuli amuapisha Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania

Na Lydia Churi-Mahakama

1Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli amemtaka Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya watanzania na kupambana na vitendo vya Rushwa.

Akizungumza wakati wa kumuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania leo Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amemtaka kiongozi huyo kufanya kazi kwa bidii licha ya changamoto zilizopo ndani ya Mhimili wa Mahakama kwa kuwa Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na Mhimili huo.

“Mungu amekuchagua, katumikie watu kwa kuongozwa na maslahi ya wananchi”, alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa tatizo la rushwa ni kubwa na liko katika kila chombo cha serikali hivyo alimtaka kiongozi huyo kupambana nalo.

2

Rais alisema pamoja na kuwepo kwa Majaji wengi ambao ni watendaji wazuri, ameamua kumchagua Prof. Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuwa dhimira yake imemkubali kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kupambana na vitendo vya Rushwa.

Akielezea sababu ya kuchelewa kuteua Jaji Mkuu, Mhe. Raisa alisema alijipa muda ili ateue mtu atakayekaa muda mrefu kwenye nafasi hiyo na siyo mtu aliyebakisha muda mchache kustaafu Utumishi wa Mahakama. Hata hivyo, Mhe. Rais alisema Ibara ya 118 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu kidogo cha 4 inampa Mamlaka ya kuteua Kaimu Jaji Mkuu kabla ya kumteua Jaji Mkuu.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema hakuna mgongano baina ya mihimili yote mitatu ya dola kwa kuwa yote inafanya kazi ya kuboresha maslahi ya wananchi wa Tanzania na kuwa katiba ya nchi inalazimisha ushirikiano baina ya mihimili yote.

Jaji Mkuu alisema, Mahakama imejiwekea utaratibu wa kuondoa uwezekano wa kutokea kwa migangano baina ya mihimili kwa kuzupa kipaumbele kesi zinazohusiana na kazi zinazofanywa na serikali kama vile ujenzi wa reli au barabara, migogoro ya wakulima na kesi ,mbalimbali za uhujumu uchumi.

Aidha, Prof. Juma alimshukuru Rais kwa kumteua kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na kuahidi kutimiza wajibu wake kikamilifu kwa kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati kwa kuwa hiyo ndiyo kazi moja kubwa ya Mahakama ya Tanzania.

Alisema Mahakama ya Tanzania inatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia nguzo tatu za Mpango Mkakati wake wa miaka mitano ambazo ni Utawala bora na usimamizi wa rasilimali, Upatikanaji wa Haki kwa wakati pamoja na urejeshaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama.

Alizitaja baadhi ya changamoto ndani ya Mahakama alizokabiliana nazo akiwa kaimu Jaji Mkuu na pia atakazokabiliana nazo kama Jaji Mkuu kuwa ni upungufu wa majengo ya Mahakama hasa Mahakama za Mwanzo nchini. Alisema Tanzania ina kata 4000 ambapo kati ya hizo, ni kata 976 pekee ndizo zenye Mahakama za Mwanzo.

Wakati huo huo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Jaji Mkuu katika majukumu yake ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata haki kwa wakati.

Aidha, Waziri huyo wa Katiba na Sheria pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Prof. Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuwa ni mchapa kazi, mtii na muadilifu.

Prof. Juma aliapishwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Januari 18, 2017 na kuteuliwa rasmi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Septemba 10, 2017 ambapo leo Septemba 11, 2017 ameapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. Prof. Juma anakuwa ni Jaji wa 8 tangu nchi ipate uhuru na Jaji wa 6 Mzalendo.

Majaji hao ni Raphs Windham (1961-1964), Telford Georges (1965-1970), Augustino Said- Jaji wa kwanza Mzalendo (1971-1977), Francis Lucas Nyalali (1977-2000), Barnabas Albert Samatta (2000-2007), Augustino Ramadhani (2007-2011), Mohamed Chande Othman (2011-2017) na Prof. Ibrahim Hamis Juma  wa sasa.

DSC08505

DSC08511

DSC08449