Home / News / RAIS AWAAPISHA MAJAJI NA KUWATAKA KUTANGULIZA MASLAHI YA TAIFA

RAIS AWAAPISHA MAJAJI NA KUWATAKA KUTANGULIZA MASLAHI YA TAIFA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo amewaapisha Majaji Kumi pamoja na viongozi wengine wa sekta ya sheria aliowateua hivi karibuni na kuwataka kutanguliza maslahi ya Taifa wanapotekeleza majukumu yao ili nchi iweze kusonga mbele.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha viongozi hao iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli pia amewataka Majaji aliowaapisha kumtanguliza Mungu ili waweze kutenda haki kwa kuwa kazi ya Jaji inahitaji mtu kumtanguliza Mungu hasa katika kufanya maamuzi.

“Ninaamini nimeteua watu wenye sifa zinazostahili pamoja na maadili hivyo fanyeni kazi zenu kwa kuzingatia maadili mema na kwa maslahi ya Tanzania ili tusonge mbele”, alisisitiza Mhe Rais.

Wakati huo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji walioapishwa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa bidii ili kumaliza kesi kwa wakati na pia kuendana na kasi ya mahakama ya kumaliza   mlundikano wa kesi Mahakamani.

“Naamini wote mlioteuliwa kwenye nafasi hii ya Jaji mna sifa zote za kufanya kazi hii, sasa kilichobaki kwenu ni kuthibitisha kwa vitendo”, alisema Jaji Mkuu na kuongeza kuwa maisha yote ya Jaji ni ya kupimwa na kwamba kazi yao tayari imeanza kupimwa leo.

Aidha, Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao kufuata maadili na kuacha tabia zisizofaa kama vile ulevi, kudai wasiyostahili, kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani kwa kuahirisha kesi bila sababu za msingi pamoja na mienendo yote isiyoendana na maadili ya kazi yao.

Akizungumzia hali ya kesi mahakamani, Jaji Mkuu aliwaambia Majaji walioapishwa kuwa kazi ya kuwa Jaji ina changamoto ya wingi wa kesi za mlundikano kwenye Mahakama mbalimbali nchini ambapo alisema hivi sasa mzigo wa mashauri kwa kila Jaji umepungua kutoka kesi 535 na kufikia kesi 460.

Alisema Mahakama ya Tanzania imejiwekea mkakati utakaowezesha kupungua na hatimaye kumalizika kwa mlundikano wa kesi mahakamani. Kufuatia mkakati huo, kila Jaji amepangiwa kusikiliza na kumaliza 220 kwa mwaka na kwamba kesi isikae mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili kwa Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa mkakati huo, katika Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za wilaya kesi haipaswi kukaa mahakamani kwa zaidi ya miezi 12 wakati katika Mahakama za Mwanzo kesi zinatakiwa kumalizika katika kipindi cha miezi sita. Aidha, kila hakimu anatakiwa kusikiliza na kumaliza kesi 250 katika kipindi cha mwaka moja.

Naye Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. Harold Nsekela aliwaasa Majaji walioapishwa leo kujiepusha na tabia zilizo kinyume na maadili kwa kuwa kazi waliyopewa inawapasa kuwa na maadili ya hali ya juu.

“Suala la maadili kwa Majaji ni la msingi sana hivyo ni vizuri mkaishi kwa kufuata na kuzingatia maadili”, aliongeza Jaji Nsekela.

Aprili 15 mwaka huu, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Majaji 10 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka , Wakili Mkuu wa serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Walioteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni Mhe. Ilvin Mugeta, Mhe. Elinaza Luvanda, Mhe. Yose Mlyambina, na Mhe. Immaculata Banzi. Wengine ni Mhe. Mustafa Siyani, Mhe. Paul Ngwembe, Mhe. Agnes Mgeyekwa, Mhe. Stephen Magoiga, Mhe. Thadeo Mwenempazi na Mhe. Butamo Philip.

Aidha, Rais alimteua Dkt. Evaristo Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Edson Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Dkt. Julius Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Ally Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Picha ya pamoja baada ya uapisho: katikati ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, wa tatu kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa tatu kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu- Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Sifuni Mchome, wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali na wa pili kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Adelardus Kilangi, katika uapisho walioapishwa ni pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.