Home / News / Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Watu Wa China akutana na Jaji Mkuu wa Tanzania

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Watu Wa China akutana na Jaji Mkuu wa Tanzania

Na Mary Gwera, Zanzibar

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma ashauri juu ya uwezekano wa kuwa na Kanuni za pamoja za Sheria ya Biashara na Uwekezaji ‘Trade Investment Regulations’ kati ya Tanzania na China zitakazowezesha ukuaji wa uchumi ambao utasaidia kuleta maendeleo baina ya nchi hizi mbili.

Aliyasema hayo, Desemba 1, katika maongezi maalum na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng, pindi alipotembelewa na Naibu Waziri huyo Mahakama Kuu-Zanzibar ambapo Mhe Jaji Mkuu anaendelea na Vikao maalum vya Mahakama ya Rufani ‘court session’

Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa; China ni nchi ambayo tayari imeshapiga hatua kubwa kiuchumi na kimaendeleo, hivyo kuwepo kwa Kanuni wezeshi za Biashara Uwekezaji  baina ya nchi hizi mbili (2) utasaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania pia.

“Ni vyema kuangalia juu ya uwezekano wa nchi zetu; Tanzania na China kuwa na kanuni zinazofanana zitakazotoa muelekeo wa jinsi ya kuwekeza kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng aliafiki ushauri huo uliotolewa na Mhe. Jaji Mkuu na kumtaka kuendelea na hatua za awali za uwasilishaji wa pendekezo hilo kwa taratibu zinazotakiwa kufanyika ili kufanikisha utekelezaji wa ushauri uliotolewa.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu pia alimueleza Naibu Waziri huyo juu ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati unaoendelea kufanyika ndani ya Mahakama kwa kutaja baadhi ya vipaumbele ambavyo Mahakama imejiwekea ikiwa ni pamoja na utoaji wa Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama, Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kadhalika.

Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania inakusudia pia kuwafikishia huduma ya Mahakama Watanzania wote kwa ngazi ya Kata.

“Kwa sasa changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni jinsi ya kuwafikishia huduma ya Mahakama wananchi wote, tuna zaidi ya Kata 3000, lakini Mahakama ya Tanzania ina majengo ya Mahakama za Mwanzo yasiyozidi 900, hivyo Mpango uliopo ni kufikisha huduma za Mahakama kwa wananchi wote ili kuwaondolea aza za umbali pindi wanapotafuta haki zao,” alifafanua Mhe. Jaji Mkuu.

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa China, Mhe. Zhao Dacheng ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama katika uendeshaji wa shughuli zake.

“China ni nchi inayoendelea kukua kiuchumi hivyo tunapaswa kutoa mchango kwa  Tanzania pia ili kuendelea kukua kimaendeleo,” alisema Mhe. Zhao Dacheng.

Naibu Waziri huyo aliyeambatana na Ujumbe wa Wakurugenzi na Maafia sita (6) kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Watu wa China walionana na Mhe. Jaji Mkuu lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili; Tanzania na China.