Home / News / Makamu wa Rais wa Tanzania, azitaka Mahakama ya nchi za Madola kupambana na Rushwa

Makamu wa Rais wa Tanzania, azitaka Mahakama ya nchi za Madola kupambana na Rushwa

Na Lydia Churi- Mahakama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka Mahakama za nchi za Jumuiya ya Madola kupambana na rushwa ili kuzifanya Mahakama hizo kuwa huru zinapotekeleza jukumu lake la msingi la utoaji haki.

Akifungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola kilichoanza leo nchini, Makamu wa Rais alisema kuwepo kwa vitendo vya rushwa ndani ya Mahakama husababisha Mahakama kutokuwa huru na kukosekana kwa utawala wa sheria.

Alisema kila nchi inapaswa kuwa na Mahakama huru na inayowajibika ili kujenga msingi wa Demokrasia. Aliongeza kuwa kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha Mahakama yake inapambana na vitendo vya rushwa ili kuimarisha uhuru wake.

“Naamini kuwa nia ya kujenga Mahakama bora na yenye kuwajibika kwa Tanzania haiwezi kutenganishwa na juhudi za Serikali Katika kupambana kuondoa umaskini na rushwa”, alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais alisema amefurahishwa kuona Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola wanakutana ili kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia nchi zao kuendana na kauli mbiu ya Mkutano huo inayosema kujenga mahakama shirikishi, inayowajibika na thabiti kiutendaji.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza kwenye Mkutano huo alisema Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ndiyo njia ya kuifanya Mahakama kuwa shirikishi, inayowajibika na thabiti kiutendaji.

Alisema ni mwaka wa pili sasa tangu Mahakama ya Tanzania ianze kutekeleza Mpango Mkakati wake wa miaka mitano ambao msingi wake ni kujenga Imani ya wananchi kwa Mahakama na kuhakikisha upatikanaji na utoaji wa haki kwa wote na wakati.

“Nina uhakika kwa wiki hii moja tutaweza kubadilishana uzoefu juu ya umuhimu wa Mpango Mkakati katika kusaidia Mahakama zetu za Jumuiya ya Madola ili ziwe thabiti, zinazowajibika na shirikishi” alisema Jaji Mkuu wa Tanzania na kuongeza kuwa kwa kuwaondolea Majaji na Mahakimu majukumu ya kiutawala kumesaidia kuifanya Mahakama kuwa inayowajibika zaidi katika kutoa haki kwa wakati.

Prof. Juma alisema kupitia Mpango Mkakati huo, Mahakama, inakusudia kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga kuongeza idadi ya Majengo. Hadi kufikia mwaka 2020 jumla ya majengo 100 ya Mahakama za Mwanzo, 48 Mahakama za wilaya, 14 Mahakama za Hakimu Mkazi, 13 Mahakama kuu na jengo moja la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania yatajengwa.

Mkutano huo unahudhuriwa na jumla ya Majaji wakuu kumi na tatu (13) kutoka nchi za Papua New Guinea, Jersey, Guyana, Uganda, Malawi, Turks Caicos Islands, Swaziland, Lesotho, Zanzibar, Tanzania, Msumbiji, Kenya na Namibia.

Mkutano huo pia unahudhuriwa na watu mashuhuri sita ambao ni Marais na Majaji waandamizi wa Mahakama za juu na Rufaa kutoka nchi za Australia, Afrika Mashariki, Pakistan na Zambia. Washiriki wengine ni Mahakimu na Majaji kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola.

Aidha, mkutano huu ni wa kihistoria hapa nchini kwa kuwa Tanzania imekuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa umoja huo wa Majaji na Mahakimu mwaka 1970. Katika bara la Afrika mkutano huu unafanyika kwa mara ya pili.