Home / News / MAKAMU WA RAIS ASHAURI KUANZISHWA KWA MAHAKAMA MAALUM ZA MASHAURI YA JINSIA

MAKAMU WA RAIS ASHAURI KUANZISHWA KWA MAHAKAMA MAALUM ZA MASHAURI YA JINSIA

Na Mary Gwera na Lydia Churi-ARUSHA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezishauri Mahakama za Afrika kuanzisha Mahakama maalum zitakazoshughulikia mashauri ya Jinsia ili kuwezesha usawa na haki za kijinsia kupatikana kwa haraka.

Akifungua Mkutano wa Jinsia na Haki ulioandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia leo Jijini Arusha, Makamu wa Rais amesema kuwa Majaji Wakuu na Wanasheria Wakuu ni Watendaji muhimu  katika kuhakikisha kuwa mifumo ya haki inaimarishwa kwenye nchi zao.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya, katika Bara hili la Afrika na Dunia kwa ujumla licha ya changamoto mnazokutana nazo katika nchi zenu, Mahakama Afrika zimekuwa ni msimamizi wa haki kwa raia wake,” alisema Makamu wa Rais.

Alisema Wanawake na Watoto ni makundi yaliyosahaulika katika jamii ukilinganisha na wanaume. Wanawake wamekuwa nyuma katika masuala ya kielimu, umiliki wa ardhi, uongozi katika ngazi mbalimbali za maamuzi pamoja na umiliki wa mali za familia.

Alisema kuanzishwa kwa Mahakama za Kijinsia kutasaidia kuondokana na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Wanawake katika jamii.

Makamu wa Rais alisema, utafiti uliofanywa na Taasisi mojawapo nchini Tanzania ijulikanayo kama ‘Tanzania Demographic Health Survey’ (TDHS) mwaka 2010 unaonyesha kuwa asilimia 44 ya Wanawake walioolewa wenye umri wa kati ya miaka 15-49 wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia kutoka kwa Wenzi wao.

Katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake, Makamu wa Rais amesema Tanzania imejiwekea Mikakati ambayo mbalimbali ikiwemo maboresho katika Sekta ya Sheria yaliyosababisha kutungwa na kurekebishwa kwa baadhi ya Sheria zinazohusiana na masuala ya Jinsia na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vituo vya Polisi nchini.