Home / News / MAJAJI WAWILI WAAGWA KITAALUMA BAADA YA KUSTAAFU RASMI

MAJAJI WAWILI WAAGWA KITAALUMA BAADA YA KUSTAAFU RASMI

MAJAJI  na Mahakimu wameshauriwa kuzingatia sheria  katika utoaji haki na wafuate miiko ya kazi zao na kuhakikisha hawafanyi wanayoyataka wao.

Ushauri huo ulitolewa mapema Julai 27, jijini Dar es Salaam na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Bernard Luanda katika hafla ya kuagwa kitaaluma yeye na Jaji mstaafu wa mahakama hiyo, Sauda Mjasiri iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Hafla hiyo ambayo iliongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma na kuhudhuriwa watu mbalimbali wakiwemo Majaji wa mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu,  Majaji wastaafu wa mahakama ya Rufani.

“Kazi ya kutoa haki ni ngumu, wanapokuja watu mahakamani kila mtu anavutia upande wake, hivyo lazima utumie busara zako na sheria inasemaje,”alisema Jaji Mstaafu, Mhe.Luanda.

“Majaji na Mahakimu wazingatie sheria, katika mahakama kila hatua ni sheria, lakini siyo sheria tu imani ya wananchi kwa mahakama ni nguzo ya mahakama,” alisema na kuongeza wananchi ni muhimu kwa na imani na mahakama.

Alisema wananchi wasipokuwa na imani na Mahakama ni hatari  kwa kuwa wanaweza kujichukulia sheria mkononi.

Jaji mstaafu Luanda alisema Majaji na Mahakimu wanapaswa kufanya kazi zao kwa kufuata miiko na wasijaribu kufanya wanavyotaka wao na wasifanye vitu vya ajabu ajabu.

Mbali na hayo, Jaji huyo Mstaafu ambaye ametumikia Mahakama kwa miaka 38, aliwaeleza Mahakimu na majaji kuzingatia miiko 10 ya kazi zao ikiwemo ya kutojaribu kukwepa majukumu yao katika kutoa uamuzi wa haki, kutojaribu kumtoa hatiani mtu kwa kufahamu mwenendo wake mbaya, isipokuwa uwe umejiridhisha ametenda kosa aliloshitakiwa nalo.

Pia, wasisite kumwachia mtu ambaye ushahidi wake haujakamilika hata kama katika uelewa wako inaonesha ametenda kosa, wasisite kumtoa hatiani mtu na kumwadhibu ipasavyo kama ushahidi unaonesha ana hatia,  bila kujali nafasi yake.

Jaji Mstaafu Luanda amewaasa Majaji na Mahakimu kutokwenda nje ya ushahidi wa kesi na kutotoa uamuzi kwa kufuata maoni ya ofisa wa mahakama, kutojadili kesi kabla haijakufikia na usiruhusu kujadiliwa ikiwa ipo tayari kwenye mikono na vizuri kujadili kesi ambayo imekuwa historia.

Jaji mstaafu Luanda ambaye amestaafu akiwa ametumikia mahakama ya Rufani kwa miaka 10  aliwashukuru majaji wenzake, mahakimu, wasajili, manaibu wasajili na wafanyakazi wengine kwa ushirikiano waliompatia katika utendaji wake wa kazi.

Naye Jaji mstaafu Mjasiri alisema ametumikia mahakama ya Rufani kwa miaka 15 ambapo kabla ya hapo amefanya kazi katika sehemu mbalimbali.

Jaji mstaafu Mjasiri alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wadaawa ambao hawana uwakilishi mahakamani kwenye mashauri mbalimbali katika Mahakama ya Rufani kuwa na uwakilishi wa mawakili kwa kuwa hiyo ndiyo mahakama kubwa hapa nchini.

Alisema kwa kuwa huyo ndiyo mahakama kubwa,  wadaawa wa kesi wanaofika mahakamani wanatakiwa wawakilishwe Ili kuhakikisha wanafuatilia kile kinachoendelea na kipo sawa kwa ajili ya haki
.
“Kwa kuwa mahakama ya Rufani ndiyo mahakama ya mwisho, ni muhimu wadaawa kuwakilishwa na mawakili anajua kuna hatua zinachukuliwa kufikia hatua hiyo, lakini zinahitajika za haraka.

Alisema kwa kuwa kuna wengine wakati wa usikilizwaji wa rufani wadaawa huamua kuachia kila kitu kwenye mikono ya mahakama, kutokana na kutokuwa na uelewe wa kile kinachoendea.

“Hivyo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kinatakiwa kuangalia hilo kwa namna mawakili wake  watawawakilisha wadaawa ambao hawana uwakilishi,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Profesa Juma alisema kwa kawaida baada ya majaji kustaafu wanaagana kitaaluma ambapo Jaji Luanda ametumikia kwa miaka 37 huku Jaji Mjasiri akiwa ametumikia sehemu mbalimbali na  kutumikia mahakama kwa miaka 15.

Jaji Mkuu Profesa Juma alisema hafla ya kuagwa kitaaluma, mbali ya kutoa ushauri inatoa nafasi kwa majaji wengine wastaafu kukutana.

” Umri  wa kuishi Tanzania umeongezeka na majaji hawa wanaondoka wakiwa na nguvu zao na wanaondoka wakiwa bado hazina,” alisema Jaji Mkuu Profesa Juma.

Alisema kinachotakiwa kuangaliwa ni namna gani wataendelea kuwatumia, hivyo vyuo vikuu vinaweza kuwatumia kuwafundisha mawakili.