Home / Latest News / MAJAJI WASTAAFU MAHAKAMA KUU-DIVISHENI YA ARDHI WAAGWA KITAALUMA-JAJI KIONGOZI AONGOZA HAFLA HIYO

MAJAJI WASTAAFU MAHAKAMA KUU-DIVISHENI YA ARDHI WAAGWA KITAALUMA-JAJI KIONGOZI AONGOZA HAFLA HIYO

Na Mary Gwera, Mahakama

Mahakama ya Tanzania inathamini mchango wa Majaji na Watumishi wengine wa Mhimili huo wanaomaliza muda wao wa Utumishi kwa mujibu wa Sheria.

Akizungumza na Vyombo vya Habari baada ya kuwaaga rasmi Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, mapema Oktoba 19,Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisema kwa kuzingatia umuhimu huo Mahakama ina utaratibu maalum wa kuwaaga kitaaluma.

“Mahakama ya Tanzania inaendelea kujenga umoja, kwa kutambua hili tunatambua kazi nzuri waliofanya Wastaafu na kuthamini mchango wao katika jukumu zima la utoaji haki nchini,” alisema Mhe. Jaji Kiongozi.

Aidha; Mhe. Jaji Kiongozi aliongeza kwa kutoa wito kwa Wananchi kuiamini Mahakama kwani ipo kuhakikisha inawahudumia kwa kutoa haki kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, mmoja wa Majaji Wastaafu, Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agathon Nchimbi aliwaasa Majaji na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunipa nafasi ya kuitumikia Mahakama katika jukumu zito na nyeti la utoaji haki, wito wangu kwa Watumishi wenzangu waliobaki ni kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu,” alisisitiza, Mhe. Jaji Mstaafu Nchimbi.

Mbali na Mhe. Nchimbi, Jaji Mstaafu mwingine aliyeagwa katika hafla hiyo ni Mhe. Jaji Gad Mjemmas, Majaji wengine ambao wamestaafu kutoka Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi ni pamoja na Mhe. Jaji Projest Rugazia na Mhe. Jaji Fredrica Mgaya.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ilihudhuriwa na wageni kadhaa ikiwa ni pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Manaibu Wasajili, Watendaji na baadhi ya Watumishi wa Mahakama.