Home / News / MAHAKAMA YAWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WAKE KUHUSU MASUALA YA HABARI

MAHAKAMA YAWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WAKE KUHUSU MASUALA YA HABARI

Na Lydia Churi-Dodoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mohamed Awadh leo amefungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo wawakilishi wa habari wa Mahakama walioko kwenye kanda za Mahakama Kuu na Mahakama za Mikoa na kuwataka kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kutoa taarifa za Mahakama zilizo sahihi zitakazowezesha kuboresha suala zima la utoaji wa haki kwa wananchi.

Akifungua mafunzo hayo mjini Dodoma, Jaji Awadh amesema Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2019/20) inakusudia kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama na kuimarisha ushirikano na wadau wake.

Alisema hatua ya Mahakama kuwapatia Mafunzo watumishi pamoja na wadau wake ni moja ya mikakati ya kurejesha imani yake kwa wananchi na kushirikisha wadau katika shughuli za Mahakama kama ambavyo nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015/16-2019/2020) wa Mahakama ya Tanzania inavyosema.

Alisema nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati huo inahusu Utawala Bora na usimamizi wa Rasilimali ambapo nguzo ya pili inahusu upatikanaji wa Haki kwa wananchi kwa wakati.

Aidha, mafunzo ya kuwajengea uwezo wawakilishi wa habari wa Mahakama walioko kwenye kanda za Mahakama Kuu na Mahakama za Mikoa yanawahusisha Watumishi wa Mahakama wakiwemo Maafisa Habari, Maafisa Utumishi, Maafisa Tawala, Maafisa Tehama pamoja na Wasaidizi wa Kumbukumbu.

Mafunzo hayo pia yanawahusisha Maafisa Habari wa Taasisi ambazo ni wadau wa Mahakama ya Tanzania zikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria, Wizara ya katiba na Sheria na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Akielezea malengo ya mafunzo hayo, Jaji Awadh alisema yatasaidia kuimarisha utoaji wa habari za mahakama kwa wananchi kwa kuwa Maafisa hao watajengewa uwezo utakaowawezesha kuandika taarifa za mahakama zitakazoongeza uelewa kwa wananchi juu ya maboresho yanayoendelea kufanyika na hatimaye kurejesha imani ya wananchi kwa Mhimili huo.

Jaji Awadh aliyataja malengo mengine ya mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kuwapatia ujuzi washiriki hao hasa katika ukusanyaji, uandaaji na utoaji wa taarifa zinazohusu mahakama ya Tanzania pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa hao kuhusu matumizi ya Teknolojia katika utoaji wa habari za Mahakama.

Mafunzo ya siku tano kwa watumishi hao wa Mahakama yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.