Home / News / Mahakama yamuaga Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mahakama yamuaga Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania

cj-r1

Pichani Mhe. Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania akimkabidhi Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tuzo ya utambuzi kwa kukuza demokrasia, kuheshimu na kuilinda Katiba na kuimarisha utawala bora wa sheria Hotuba ya mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania kwenye sherehe ya kumuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Asha- Rose Migiro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jaji Kiongozi wa Mahakama kuu ya Tanzania, Wahe Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wahe. Majaji Wakuu Wastaafu na Majaji Wengine Wastaafu, Mhe. Msajili Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Wahe. Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wasajili, Wakurugenzi na Watendaji wa Mahakama, Mahakimu, Mawakili na Watumishi wote wa Mahakama, Waandishi wa Habari, Wageni waalikwa, Mabibi na

Mabwana.

1. UTANGULIZI.

Mheshimiwa Rais, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema ya kuiona siku hii adhimu. Aidha nakushukuru sana Mhe Rais kwa kukubali mwaliko wetu wa kuwa nawe leo katika shughuli hii ya kipekee tuliyoiandaa kwa ajili yako. Ninajua kuwa kwa kipindi kifupi ulichobaki nacho katika uongozi wa Taifa letu una majukumu mengi na ratiba iliyojaa lakini kwa hisani kubwa umekubali kutenga muda huu ili tuwe nawe hii leo. Pia nawashukuru wageni waalikwa wote mliohudhuria kwa kukubali kushiriki nasi. Asanteni sana.

2. MADHUMUNI YA KUKUALIKA.

Mheshimiwa Rais, Madhumuni ya kwanza ya hafla hii ni kwa Mahakama kukuaga rasmi kwa matarajio ya kumaliza kipindi chako cha kuiongoza nchi yetu kwa mafanikio makubwa tangu tarehe 21 Disemba, 2005 ulipoapishwa kipindi cha kwanza kuwa Rais wa nchi yetu hadi hivi sasa. Madhumuni ya pili ni kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi na Serikali yako kwa ujumla kwa hatua dhabiti na mbalimbali mlizochukuwa kusaidia kuimarisha Mahakama kama Mhimili huru wa Dola na kuchangia kwenye kuboresha utendaji haki.

3. UHUSIANO NA MAHAKAMA NA UTAWALA WA SHERIA

Mheshimiwa Rais, nadhani utakumbuka kuwa ni katika jengo hili hili la Mahakama Kuu ndiko ulikokuja kutiliwa sign na Mh. Jaji Damian Lubuva Form zako kwa ajili ya kugombea Urais mara ya Kwanza. Ulipokuja tena, tarehe 13 Februari, 2006, siku 53 baada ya kupaishwa tarehe 21 Disemba, 2005 kama Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, ulisema haya: “Unapopewa eneo jipya la “Command”, …..kitu muhimu ni kutafuta habari ya eneo lenyewe. Ili ukitulia…..upange mipango yako”. Wakati huo, ulituuliza na tukakupa taarifa juu ya mafanikio na changamoto zilizopo na dira na mipango yetu ya kuboresha Mahakama na utendaji haki. Tunashukuru sana kwamba kwa kipindi chote cha uongozi wako wa Taifa letu tumekua na fursa nyingine nyingi za kukupa taarifa zaidi juu ya mambo yote hayo. Umejumuika nasi na kutupa nasaha mara kadhaa kuhusu muundo wa Mahakama, utendaji bora na uadilifu kama Mgeni Rasmi, kwenye mikutano mingi ya mwaka ya Majaji. Umekuwa ukihudhuria uzinduzi wa Siku ya Sheria ya Mahakama, ambayo mpaka sasa umehudhuria mfululizo, mwaka hadi mwaka, kwa miaka 8, mara ya mwisho ikiwa tarehe 4 Februari, 2015. Tunashukuru sana kwa kuvunja rekodi. Mheshimiwa Rais, eneo moja la msingi baina ya mahusiano yako kama Mkuu wa Nchi na Kiongozi Mkuu wa mmoja ya mihimili mitatu ya Dola yaani Mamlaka ya Utendaji au Serikali na Mahakama ni lile la kuheshimu Katiba ya Nchi, Utawala Bora na Haki za Binadamu. Mheshimiwa Rais, wageni waalikwa Hayati Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa pia aliwahi kusema haya: “In shorthand, the Constitution itself must be based on the principles of the rule of law”. Mhe Rais, ulipofungua rasmi mara ya kwanza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 30 Disemba, 2005, ulitamka haya: “Tutaheshimu utawala wa sheria, na tutazingatia na kuheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya Mihimili ya Dola, yaani Utawala, Bunge na Mahakama. Tutaheshimu uhuru wa Mahakama”. Ulipokuja hapa Mahakama, hiyo tarehe 13 Februari 2005 ulituahidi haya pia: “Serikali ya Awamu ya Nne itazingatia na kuheshimu utawala wa sheria. Hatutawaingilia katika kutimiza utawala wa sheria………..mimi nawahakikishia kwamba sitafanya na nitahakikisha kwamba wenzangu pia hawatafanya na kama kuna mtu yoyote ana kishawishi hicho, niambieni na tutaona cha kufanya. Kwa kweli, tuwape uhuru wa kufanya maamuzi yenu mtuhakikishie kwamba haki inatendeka”. Kwa Jamii, utawala wa sheria unaimarisha demokrasia, unaleta uwajibikaji; unahakikisha heshima na uzingatiaji wa haki za binadamu, unaongeza upatikanaji wa haki sawa na kwa wakati kwa wote; unamnyima fursa za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Kwenye Utawala wa sheria Tanzania haijipimi tuu. Inapimwa vile vile. Kwenye kipimo cha World Justice Project (WJP) Rule of Law Index 2015 Tanzania imekua nchi ya 72 duniani. Tumepitwa na Botswana, Ghana na Afrika Kusini, lakini tumezipita Zambia, Kenya, Ethiopia, Nigeria, Cameroon na Zimbabwe na nchi nyingi nyingine. Mheshimiwa Rais na wageni waalikwa, Kwa niaba ya Mahakama na wanasheria wenzangu, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza kwa kuheshimu, tena sana, Katiba ya Nchi, utawala wa sheria na uhuru wa Mahakama. Kwa vitendo vyako umeimarisha misingi ya Demokrasia. Mahakama, Majaji, Wasajili na Mahakimu wamefanya kazi kwa amani, utulivu na bila ya kuingiliwa na Serikali kwenye uhuru wao. Kwenye hili, nadhani ni vizuri tuu niwahakikishie wananchi kuwa hakukua na haja ya kukustakia kiongozi yoyote wa Serikali aliyekiuka kauli yako nzito. Nguvu yetu ni kuwa Mahakama huamua migogoro ya kisheria kwa kuzingatia Katiba na sheria na kupitia sababu za kisheria zinazotolewa. Wanazuoni husema hatuna nguvu ya upanga; nguvu yetu ni kalamu tuu na imani ya wananchi. Mahakama ina deni kubwa la kukushukuru kwa yote uliyoyafanya haswa kuheshimu Katiba na kuimarisha utawala wa sheria.

4. HATUA ULIZOCHUKUWA WEWE RAIS NA SERIKALI YAKO.

Mheshimiwa Rais ulipofungua Bunge jipya tarehe 30 Disemba, 2005 ulitoa kauli hii: “Serikali ………………………………………..itatimiza ipasavyo wajibu wake na kuimarisha miundombinu ya kutoa haki kwa kuongeza idadi ya watumishi, kuwaendeleza kitaaluma, kukarabati majengo yaliyopo na kujenga mapya, na kupeleka huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi”. Ulipotutembelea tarehe 13 Februari 2006 tulikueleza changamoto kubwa na sugu zilizokua zinaikabili Mahakama: ufinyu wa bajeti ya kuendeshea Mahakama; uhaba wa raslimali watu na miundombinu chakavu ya Mahakama zetu. Bila ya kusita uliahidi kuzichukulia hatua changamoto hizo ambazo nyingi zilikuwa kikwazo si tu kwa Mahakama kutimiza wajibu wake wa Kikatiba na kisheria wa kutoa haki bali pia kwa wananchi kupata fursa ya kupata haki. Mheshimiwa Rais, niruhusu, kwa kifupi tuu nitilie mkazo mambo machache kama tathmini ya tulikotoka, tulipo na tunapotarajia kufika na mchango wako na Serikali ya Awamu ya Nne unaoiongoza.

5. RASILIMALI FEDHA. BAJETI

Mheshimiwa Rais, ulipoingia madarakani mwaka 2005 kiasi cha fedha tulichokuwa tumetengewa na Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2005/2006 kwa ajili ya uendeshaji wa Mahakama kilikuwa takriban shilingi bilioni thelathini na sita nukta sita (36.6 bilioni) kwa mwaka huo. Baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani mwaka 2005/2006 kiasi hicho kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia zaidi ya shilingi bilioni themanini na tisa nukta tisa (89.9 bilioni) kwa mwaka huu wa fedha 2015/2016. Ongezeko la asilimia 143% ndani ya kipindi cha miaka 10. Ni lazima Mahakama ijivunie, kwa ongezeko la Bajeti ya Uendeshaji kwenye kipindi chote hicho. Changamoto za upatikanaji wa fedha zote zilizopitishwa na Bunge ndani ya Bajeti ni za Kitaifa. Nishukuru tuu kuwa kwa sasa Mahakama tunapata wastani wa asilimia 75 ya bajeti yote ya Uendeshaji (O.C) na mishahara kwa asilimia 100. Ni lazima tukiri mbele yako na Umma wa Tanzania, kuwa shughuli za uendeshaji wa Mahakama, kwenye maeneo mengi zimeboreshwa kwa kiwango cha kuridhisha ukilinganisha na miaka 10 iliyopita. Mheshimiwa Rais, ni dhahiri kuwa hili linatokana na agizo lako kwa Serikali kufanya juhudi za maksudi dhidi ya Muhimili wa Mahakama ambayo kwa miaka nenda rudi ulikua muathirika wa “budget ceiling”. Mara nyingi umetusaidia kujenga hoja zaidi. Umekua hata wakili wetu kwenye suala hili endelevu la kuwa na bajeti inayokidhi na inayoiwezesha Mahakama kutenda kwa ubora zaidi wajibu wake. Tunashukuru sana kwa maagizo na usimamizi wako. Mfuko wa Mahakama Mheshimiwa Rais katika kipindi cha uongozi wako umeanzishwa Mfuko wa Mahakama chini Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (Judicial Administration Act No 4 of 2011) kama ilivyo kwa Mfuko wa Bunge. Miongoni mwa manufaa yaliyojitokeza ya Mfuko huu kwa Mahakama ni haya yafuatayo: Umesadia sana kuifanya Mahakama iwe na bajeti inayotabirika zaidi na kueleweka hivyo kuiwezesha kupanga na kutekeleza mipango yake kwa uhakika zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa huko nyuma. Aidha ujio wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, unatoa utaratibu mzuri wa upatikanaji wa fedha za Mahakama na Bunge toka Mfuko Mkuu wa Serikali kwa kila robo mwaka (miezi mitatu mitatu) na Bajeti ya Mahakama na Bunge kulindwa (Protected/Ring-fenced). Mheshimiwa Rais, kwa yote hayo tunaamini unaacha msingi na histora ya kukumbukwa ya uhakika wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza majukumu ya msingi ya Uendeshaji wa Mihimili mingine ya Utawala wa Nchi, yaani Mahakama na Bunge. • Fedha za Uendeshaji (O.C) Aidha kama nilivyoeleza hapo juu kiasi cha fedha kinachowekwa katika mfuko huo kimekuwa kikiongezeka tangu Mfuko huo uanzishwe kutoka shilingi billion 57.8 mwaka 2012/2013 hadi kufikia shilingi billion 88.9 kwa mwaka huu wa fedha wa 2015/2016. Kwa upande wa fedha za Uendeshaji pekee (O.C) • Fedha za Maendeleo Mheshimiwa Rais, Bajeti ya Maendeleo iliongezeka na kufikia bilioni 40 mwaka 2014/15 kabla ya kushuka kufikia bilioni 12.1 kwa mwaka 2015/16. Aidha, malengo ya kuwa na jengo la Mahakama ya Tanzania (Makao Makuu/Mahakama za Juu) na majengo bora ya Mahakama Kuu kwenye Mikoa yote Tanzania Bara, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo zilizo bora na zenye kukidhi mahitaji na viwango vya karne ya Ishirini na Moja yalitekelezwa kwa kiwango kidogo kutokana na hali ngumu ya upatikanaji wa fedha za maendeleo. • Fedha za Maendelo za Benki ya Dunia Mheshimiwa Rais, faraja, kubwa tuliyoipata ni pale uliposimamia na kuhimiza Serikali yako ipate fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya Maboresho ya Mahakama. Tumefikia hatua nzuri. HAZINA tayari wametoa ridhaa na barua kwenda Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata fedha za kuanzia maandalizi ya mradi huu mkubwa, unaotajiria kuanza Desemba 2015/Januari, 2016. Mheshimiwa Rais, kama unavyofahamu maeneo muhimu yanayolengwa na mradi huu ni ujenzi wa miundo mbinu ya kisasa ya Mahakama, kujenga uwezo, mafunzo na nyenzo kwa Majaji, Mahakimu na Wataalamu wengine wa Mahakama na matumzi ya Teknolojia katika shughuli za uendeshaji pamoja na jukumu la utoaji haki. Tunajipanga vyema kutekeleza mpango huu kulingana na mahitaji yetu na viwango vinavyohitajika vya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Lengo letu ni kuwa haki ipatikane na ipatikane kwa wakati na kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa kutokana na juhudi, mipango na mikakati kadhaa tunayoendelea nayo.Washiriki wa maendeleo kadhaa wameonyesha nia ya kushirikiana na sisi. • Viwanja vya majengo ya Mahakama Mheshimiwa Rais, naomba upokee shukrani za pekee za kutupatia viwanja Na. 43 na 44 mtaa wa Chimala kwa ajili ya jengo la Mahakama ya Tanzania na pia kutupatia eneo la iliyokuwa Canadian Village huko Masaki kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Majaji, ambazo ni muhimu sana kwa Majaji zaidi ya 45 wenye makazi yao Dar es Salaam. Tunashukuru sana kwa mbegu hii uliyoipanda na ni matumaini yetu itaendelezwa na awamu ijayo Tunataraji katika kipindi cha siku 60 zijazo kujenga Mahakama za Wilaya, Mahakama za Mwanzo na nyumba za Mahakimu wa Wilaya Mkuranga, Kibaha na Longido katika mpango wa utafiti wa matumizi ya Teknolojia ya ujenzi wa haraka na gharama nafuu na ubora chini ya usimamizi na ushauri wa Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Baraza la Ushauri wa Ujenzi (National Construction Council). Mafanikio ya hatua hii itapunguza changamoto tuliyonayo ya miundo mbinu ya Mahakama za Wilaya na Mikoa yote na baadhi ya Mahakama za Mwanzo. Aidha, tatizo la nyumba za Mahakimu kwenye maeneo ya Wilaya na Vijiji pia litapatiwa ufumbuzi.

6. RASLIMALI WATU.

Mheshimiwa Rais kwa upande wa rasilimali watu, wakati unaingia madarakani na hadi kufikia mwaka 2008 Mahakama ilikuwa na jumla ya watumishi wapatao 4,972. Hivi sasa unapoondoka madarakani idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia jumla ya watumishi 6,052. Ongezeko la watumishi 1,180 zaidi linaonekana zaidi katika kada zifuatazo:  Mwaka 2005 Majaji wa Mahakama ya Rufani walikuwa 9 tuu. Sasa hivi jumla ya Majaji wa Rufani ni 16. Katika kipindi cha uongozi wako umeteua Majaji wa Rufani 19, ikiwemo Majaji Wakuu 2.  Mwaka 2005 Majaji wa Mahakama Kuu walikuwa 35. Leo tunapokuaga unaiacha Mahakama Kuu ikiwa na Majaji 84. Katika kipindi cha uongozi wako umeteua jumla ya Majaji wa Mahakama Kuu 94. Kubwa zaidi, umetilia mkazo sana usawa wa Jinsia kwani hivi sasa takriban 41% ya Majaji ni wanawake. Pia idadi hiyo ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama kuu uliowateua ni kubwa kuliko jumla ya Majaji walioteuliwa katika awamu zote tatu za uongozi uliokutangulia.  Kwa upande wa Mahakimu Wakazi ulipoingia Madarakani walikuwa 151 tuu. Kwa sasa idadi yao iongezeke hadi kufikia 670 na Tume ya Utumishi ya Mahakama iko mbioni kuajiri wengine 142. Watakua 812 kabla ya October, 2015.  Aidha katika kipindi chako cha uongozi Mahakama imeweza kuajiri watumishi wa kada mpya ambazo hazikuwepo miaka ya awali za Wasaidizi wa Sheria wa Majaji ambao wapo 62 ,  Pia watumishi wa kada nyingine kama vile Maafisa Utumishi,Wachumi, Wataalam wa Mifumo ya Kompyuta, Wahasibu, Watunza Kumbukumbu, Makatibu Muhtasi, Madereva na Walinzi wameajiriwa wapya na kufanya idadi ya watumishi wote iongezeke hadi kufikia hiyo niliyoitaja hapo juu.

7. MUUNDO WA MAHAKAMA.

Mheshimiwa Rais, kama unavyofahamu baada ya kutungwa na kuanza kutumika kwa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama, Na. 4 ya 2011 Muundo wa Mahakama umebadilika kwa kuanzishwa kwa kada ya Watendaji wa Mahakama ambao wanasimamia masuala yote ya fedha na utawala wa Mahakama na kuwaacha Majaji, Wasajili na Mahakimu waliokuwa wanafanya kazi hizo washughulike na masuala ya mashauri yaliyoko Mahakamani. Hii leo tuna watendaji 32 Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Mahakama za Hakimu Mkazi na kuna watendaji wengine 162 kwenye Mahakama za Wilaya wote hawa wameajiriwa baada ya Sheria hiyo kuanza kufanya kazi. Muundo huu umeleta na unaendelea kuleta tija na mafanikio. Umesaidia kuimarisha uwezo na kuboresha utendaji wa Mahakama katika ngazi zote.

8. MAFUNZO KWA WATUMISHI.

Mheshimiwa Rais, katika kipindi hiki cha uongozi wako watumishi wengi wa Mahakama wamepata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu ndani na nje ya nchi. Katika kipindi hiki jumla ya watumishi 1245 wamepata shahada za uzamivu, uzamili na shahada za kawaida na wengine wamepata astashahada na wengine vyeti vya fani mbalimbali. Kwa mwaka huu wa fedha 2015/2016, Mahakama imepanga kuwapatia mafunzo ya muda mrefu watumishi wengine wapatao 584 na wakati huo huo mafunzo ya muda mfupi yakiendele kutolewa kila kunapapatikana fursa ya kufanya hivyo. Mahakama ina Wafanyakazi 104 wanasomea Shahada ya Uzamili; kuna wafanyakazi 131 wanaosoma Chuo Cha Sheria kwa Vitendo; kuna 281 wanaochukua Shahada ya kwanza Vyuo Vikuu; kuna 159 wanaosomea Diploma. Kila mmoja ana ari na shauku ya kujiendeleza. Mahakama imetoa na inaendelea kuoa fursa hizi ili kila mtumishi aweze kujiendeleza kitaaluma. Fursa hizo, Mh. Rais, zinatokana na juhudi za Serikali kutambua umuhimu wa kuwa na Mahakama yenye wafanyakazi wenye taaluma, ujuzi na inayotoa kwenye ngazi zake zote, za nchi pia, huduma bora kwa wananchi.

9. USIKILIZAJI WA MASHAURI.

Mheshimiwa Rais, kiwango cha usikilizaji mashauri ambayo ndio kazi yetu ya msingi kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo:  Ngazi zote za Mahakama kufanya kazi kwa mipango, malengo vigezo na vipimo;  Kumaliza mashauri ya muda mrefu, yaani yale ya zaidi ya miaka 2 kwa Mahakama Kuu na muda mfupi zaidi kwa Mahakama za ngazi za chini yake;  Kufanya vikao maalum vya Mahakama Kuu ya usikilizwaji wa mashauri yenye vipaumbele; na  Kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa Mahakama za ngazi za chini. Mheshimiwa Rais, kama unavyofahamu hivi sasa Mahakama ina “BRN” (Matokeo Makubwa Sasa) wenyewe. Kama ulivyo eleza mara kadha, madhumuni ya mfumo wa BRN ya Taifa ni kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha kuwa kilichokusudiwa kinafanyika, tena kwa wakati. Uwezo wa Mahakama ni kusikiliza zaidi ya asilimia mia moja ya mashauri yote yanayofunguliwa Mahakamani kwa mwaka. Tunachopambana nacho sasa kwenye mikakati mipya inayotumia mpango wetu wa “BRN” ni kuondoa mashauri yaliyorundikana ya zamani kwenye badhi ya Mahakama. Mlima huo umeanza kuwa kichuguu! Kuna sehemu hauonekani. Naomba Mh. Rais, uridhike tuu kuwa utakapoondoka madarakani mikakati na mipango hiyo tutaendelea nayo mpaka tufanikiwe.

10. MATUMIZI YA TEHAMA

Mheshimiwa Rais, Dunia ya sasa ni ya TEHAMA. Mahakama haina uchaguzi mwengine zaidi ya kutumia TEHAMA. Tumeanza kutumia mfumo wa TEHAMA kwenye ngazi za Mahakama ya Rufani mpaka Wilaya, kukusanya Takwimu kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki/TEHAMA. Mpango uliopo ni matumizi ya TEHAMA, kwenye shughuli zote za Mahakama, pamoja na mashauri (Comprehensive case managements systems) kwa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama za Mikoa na Mahakama za Wilaya. Kupitia kwako, tunapenda kuishukuru Wizara ya Sayansi na Teknolojia hususani Waziri, Proff. Makame Mbarawa kwa kutoa maamuzi ya kuingiza Mahakama zote Nchini kwenye mpango wa kuunganishwa na Mkongo wa Taifa. Hatua hii itasaidia kuleta mabadiliko na ufanisi wa utendaji kazi na utoaji haki Nchini, kwa vile sasa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yatarahisisha kazi nyingi za Kiutawala na Mashauri.

11. WASHIRIKI WA MAHAKAMA

Mheshimiwa Rais, Mahakama ina washiriki muhimu. Kwenye kipindi chote hichi tumeshirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Kurekebisha Sheria na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Kwenye mashauri ya jinai tunaendelea kuimarisha utendaji kazi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka ambayo tunakuomba sana uifikirie ili iende sambamba na mikakati yetu ya kuharakisha umalizikaji wa mashauri, haswa ya jinai. Tunaongea lugha moja na Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza kuhusu umuhimu huu. Mmoja kati ya kiungo muhimu, Mawakili wa Kujitegemea, ambao pia wanawajibika kama maafisa wa Mahakama pia wamechangia vyema kwenye utendaji haki. Miongoni mwa washiriki pia nisisahau watoa Msaada wa Sheria. Tunakushukuru sana, Mh. Rais, kwa kuridhia kwako, tarehe 23 Juni, 2015 kanuni mpya za malipo za Mawakili-The Advocates Remuneration Order, 2015. Ninajua Mawakili Binafsi 5,073 ambao wako kwenye orodha ya Mawakili hivi sasa wamefurahi sana.

12. MAHAKAMA NA HUDUMA BORA

Mheshimiwa Rais, Tunafahamu kuwa kwenye uongozi wako wa Taifa letu unaguswa sana na kero za wananchi. Umewahi kutukumbusha umuhimu wa kuzingatia kwa kumaliza mashauri kwa wakati. Kukidhi yote hayo Mahakama imeboresha na imeanzisha njia mpya na za kisasa za kupata maoni na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji wetu na hata miendo ya wafanyakazi wa Mahakama. Ulivyokuwa unalivunja Bunge la Kumi na kuagana na Wabunge tarehe 9 Julai, 2015, Dodoma ulieleza kuwa mwaka 2014 watu milioni 9.3 walikuwa wanatumia Intaneti na kulikua na laini za simu milioni 28. Kwa mazingira ya sasa, sehemu nyingi za Mahakama masanduku ya maoni yamepitiwa na wakati. Kupitia mtandao wa simu na intaneti Mahakama inapokea maoni na malalamiko ya wananchi. Yanashughulikiwa papo kwa papo. Kwa mfano kuanzia 6 Disemba, 2014 hadi 5 Agosti, 2015 tumepokea Simu za Ujumbe Mfupi (SMS) 399 na Whatsup 58 za malalamiko kutoka mikoa na wilaya nyingi za Tanzania (Sumbawanga, Muleba, Kahama n.k.). Yote yametolewa majibu kwa 99%. Sasa hivi tunafanya utafiki kujua kama wateja wetu wanaridhika na huduma kwenye Wilaya 20 (Masasi, Misungwi, Nzega, Babati, Kibondo, Masasi, Tandahimba). Kwa ushauri wako Mh. Rais, Mahakama unayoiwacha ni sikivu, na itaendelea kulenga utatuzi wa kero za watanzania, haswa wateja wetu.

13. HITIMISHO.

Mheshimiwa Rais naomba kumalizia kwa kukushukuru tena kwa kutusikiliza muda wote wa uongozi wako na kwa kutekeleza ahadi zako za kuisaidia Mahakama iwe ubora zaidi. Nasaha zako zimechangia kufanikisha dira na malengo yetu. Tutaendelea kuzienzi. Mheshimiwa Rais, Tuwakumbushe Viongozi wa sasa, wajao na Watanzania wenzetu uimara na ustawi wa Mhimili huu wa Mahakama kuwa ndiyo nguzo muhimu juu ya Amani na Utulivu wa Nchi yetu Mahakama ndiyo kimbilio la sisi sote. Hivyo, hatuna budi tuimarishe Mahakama kama ulivyotufundisha wewe na waliokutangulia. Paul B. Wice, kwenye kitabu chake, Presidents in Retirement: Alone and Out of Office, Lexington Books, 2009 – alifanya utafiti wa mwenendo baada ya kustaafu wa Marais 34 wa Marekani. Aligundua kwamba kustaafu Rais kunampa uhuru binafsi mkubwa (personal freedom) kujishughulisha na mambo mengine na kutimiza ndoto zake nyingine za maisha. Tunamwomba Mwenyenzi Mungu akubariki, akujaalie afya njema na hekima zaidi na akulinde wewe na familia yako. Tunakutakia kila la kheri na mafaniko kwenye cheo chako kipya cha senior citizen. Una haki ya kuvuna ulichopanda! Baada ya kusema haya machache kwa niaba ya Mahakama naomba Mh. Rais, ukubali kupokea Tuzo tuliyoiandaa kama utambuzi wetu kwako kwa kukuza demokrasia ya Tanzania, kuheshimu na kuilinda Katiba, kuimarisha utawala bora na kuliongezea kasi gurudumu la utendaji haki. Iwe kumbukumbu ya rekodi uliyoiweka ya mahusiano yako mema na Mahakama na yanayotakiwa kuigwa na wamu zijazo. Baada ya hapo, Mh. Rais, kwa heshima kubwa nitakuomba utupe nasaha zako, kwa mara nyingine tena. Asanteni kwa kunisikiliza.