Home / Latest News / MAHAKAMA YA MFANO INAWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO; JAJI MZUNA

MAHAKAMA YA MFANO INAWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO; JAJI MZUNA

Na Catherine Francis, Mahakama Kuu Arusha

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Jaji Mosses Mzuna amesema kuwa Mahakama Kanda ya Arusha inaweza kuwa Mahakama ya mfano ikiwa kila mtumishi wa Mahakama hiyo atatimiza wajibu wake kikamilifu.

Akizungumza katika kikao cha Watumishi wa Mahakama wa Arusha mwishoni mwa wiki, Jaji Mzuna alisisitiza kwa kuwaonya watumishi wenye tabia za uzembe kazini kuacha tabia hizo kwani husababisha kazi kutokutendeka kwa ufanisi.

Mhe. Jaji Mzuna aliwasihi pia Viongozi kuwa na uratibu mzuri wa matumizi ya fedha kwani matumizi mabaya ya fedha hukwamisha shughuli za Kimahakama.

“Wakati sasa umebadilika hivyo kila Mtumishi akae atafakari utendaji wake wa kazi na kubadilika kabla ya kuchukuliwa hatua kwa uzembe,” Alieleza Jaji Mfawidhi huyo.

Mhe. Jaji Mzuna aliendelea kusisitiza hilo kwa kunukuu usemi wa Jaji Mkuu Mstaafu , Mhe. Jaji Augustino Ramadhani usemao ‘Mjue Kamanda wako’ akimaanisha kuwa ni wajibu wa kila Mtumishi kujua ni aina gani ya kiongozi anayewaongoza kwani yeye hapendi uzembe na uvivu kazini hivyo yawapasa kubadilika kuendana na kasi yake ya kiutendaji.

Aidha Mhe. Jaji Mzuna aliwapongeza baadhi ya watumishi wa Mahakama wenye usikivu kwa viongozi wao na wanajituma kutelea wajibu wao kwa bidii huku akisisitiza hilo kwa kusema ‘Excellence is not an accident but it is a process’ akimaanisha kuwa ubora wa kazi hauji kama ajali bali ni mchakato.