Home / News / MAHAKAMA YA BIASHARA YAJIPANGA KUTEKELEZA MPANGO MKAKATI KWA VITENDO

MAHAKAMA YA BIASHARA YAJIPANGA KUTEKELEZA MPANGO MKAKATI KWA VITENDO

Na Mary Gwera

MTENDAJI, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bw. Willy Machumu amewataka Watumishi wa Divisheni hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali kufanya kazi kwa malengo kwa kutoa huduma nzuri zitakazowaridhisha wateja.

Bw. Machumu aliyasema hayo Agosti 10, alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo ya siku moja kuhusu Mahusiano kati ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama na Tathmini ya Utendaji kazi (OPRAS) katika Ukumbi wa Mahakama ya Biashara.

Mtendaji huyo alisema ili kufanya kazi kwa matokeo zaidi aliona ni vyema kuhuisha malengo ya Mfumo wa Utendaji (OPRAS) na malengo ya Mpango Mkakati unaotekelezwa na Mahakama kwa sasa.

“Lengo kuu la kufanya hivi ni kushirikisha Watumishi wa kila Kada ili kuona umuhimu wa kufanya kazi ili kwa pamoja kama Taasisi tuweze kufikia malengo  makuu mojawapoo ikiwa ni kuongezeka kwa kiwango cha wananchi kuridhika na huduma zitolewazo na Mahakama,” alieleza Bw. Machumu.

Kwa upande wake, Mchumi Mwandamizi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Geofrey Mashafi ambaye alishiriki katika Mafunzo hayo kuwakumbusha Watumishi kuhusu Mpango Mkakati alisema kuwa Mahakama ya Biashara inayo jukumu kubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

“Kama mnavyofahamu jukumu kuu la Mahakama hii ni kushughulika na utatuzi wa migogoro ya kibiashara ili kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji nchini kwa lengo la kuongeza nafasi za ajira na kukuza uchumi wa nchi,” alisema Bw. Mashafi wakati akitoa mada kwa Watumishi wa Mahakama hiyo.

Bw. Mashafi alisema kuwa mahusiano ya Mpango Mkakati na OPRAS hayawezi kutenganishwa kwani viashiria vilivyowekwa kupima utekelezaji wa Mpango Mkakati haviwezi kupimika kwa ujumla ila kwa kupima utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja.