Home / News / MAHAKAMA NA TLS KUENDELEZA USHIRIKIANO

MAHAKAMA NA TLS KUENDELEZA USHIRIKIANO

Na Magreth Kinabo

Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati  amesema   kuwa Mahakama itaendelea  kutoa ushirikiano  kwa  Chama  cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika  masuala  ya utendaji  kazi kwa kuwa vyombo hivyo vinafanya kazi kwa  kutegemeana.

Kauli hiyo imetolewa leo  na  Msajili Mkuu huyo, wakati  Rais wa TLS,  Fatma Karume   na  baadhi ya viongozi  wa chama hicho, walipotembelea  ofisi za Mahakama Rufani jijini Dar es Salaam.

“Ninashukuru kwa  ushirikiano wenu  mliouonesha kwa kuwa suala la kushirikisha wadau wetu ni miongoni mwa jambo  tunalolipa kipaumbele,” alisema  Revocati.

Aliongeza kwamba Mahakama na TLS ni  kama mtu na dada, hivyo mi muhimu kuendeleza ushirikiano  huo hasa katika Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/2020.

Msajili huyo, aliongeza kwamba suala la kuendeleza ushirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lipewe kipaumble na TLS ili kuweza kuendana na mabadiliko ya dunia, kama ilivyo Mahakama ya Tanzania inavyolipa msisitizo.

Kwa upande wake Rais wa TLS, Fatma, alisema   aliipongeza  mahakama ya Tanzania kwa kuwasaidia Watanzania kupata haki.

Alisema  TLS ni wadau wa ndani ya Mahakama, hivyo wataendelea kufanya kazi pamoja, kwa kuwa bila Mahakama hawawezi kufanya kazi.

Aidha   viongozi  hao, awali  walipata nafasi ya kumtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania. Pia walielezewa juu ya Mpango Mkakati  wa Miaka Mitano na malengo ya mpango huo na maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama na mfumo  wa kuhifadhi takwimu  kwa njia  ya kielektroniki (JSDS) .