Home / News / Mahakama Kuu Kanda ya Tabora yajipanga kuondoa mlundikano wa Mashauri

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora yajipanga kuondoa mlundikano wa Mashauri

Na Mary Gwera, Tabora

Uhairishwaji wa kesi wa mara kwa mara unaotolewa na baadhi ya Mawakili umeelezwa kuwa moja ya sababu zinazopelekea kutofikiwa kwa malengo ya umalizaji wa mashauri kwa wakati.

Hayo yalisemwa na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mhe. Sam Rumanyika katika kikao kilichoketi baina ya Mahakama katika Kanda hiyo na Wadau wake Oktoba 03, 2017 katika Ofisi ya Mhe. Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora.

“Lengo la kuwaita katika kikao hiki cha pamoja ni kukaa kama ndugu tukiwa na nia moja ya kumaliza mlundikano wa mashauri yaliyopangwa kusikilizwa katika mfululizo wa vikao saba (7) vya kuondoa mlundikano wa mashauri ambavyo vitaanza rasmi kesho, Oktoba 04, 2017” alisisitiza Mhe. Rumanyika.

Kikao hicho cha kabla ya kuanza kwa kikao maalum cha kusikiliza mashauri ‘pre session meeting’ kiliwahusisha wajumbe wafuatao; Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Naibu Msajili-Kanda ya Tabora, Mtendaji-Mahakama Kuu-Tabora, Wanasheria wa Serikali na wa Kujitegemea, Mkuu wa Gereza la Uyui na RCO.

Kwa upande wake Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mhe. Sharmillah Sarwatt alisema kuwa lengo la Kikao hicho na Wadau ni kujipanga kwa pamoja kuhakikisha mashauri yote ya mlundikano yaliyopangwa kusikilizwa katika vikao saba yanamalizika kufikia Desemba 15 mwaka huu.

“Lengo la Kanda yetu ya Tabora ni kuhakikisha kuwa tunamaliza mlundikano wa mashauri na Mkakati Mkuu tulionao kama Kanda ni kumaliza mashauri mengi kuliko yanayopokelewa; ili yanayobakia yawe machache,” alifafanua Mhe. Sarwatt.

Akiongelea juu ya kikao maalum cha kuondoa mashauri kinachoanza rasmi Oktoba 04, mwaka huu, Mhe. Sarwatt alisema kuwa jumla ya kesi 14 za mauaji (katika kikao cha kwanza) zimepangwa kwa ajili usikilizwaji wa awali (PH) na hatua awali za kuwahoji watuhumiwa ‘Plea taking’

Aidha; Naibu Msajili huyo aliongeza kuwa katika mfululizo wa vikao hivyo saba (7) vya kuondoa Mlundikano, jumla ya kesi 82 za aina tofauti za mlundikano zimepangwa kusikilizwa na kumalizwa ifikapo Disemba 15, 2017 na kuongeza kuwa kesi ya muda mrefu zaidi ambayo pia imepangwa kusikilizwa katika vikao hivyo,ni ya mwaka 2011 ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya kutoa hukumu.

Hata hivyo; Mhe. Sarwatt alisema kuwa mchakato cha kuondoa mlundikano wa mashauri kwa Kanda ya Tabora, ulianza kwa muda mrefu hata kabla ya kutolewa kwa maagizo kutoka Makao Makuu ya kumaliza mlundikano wa kesi hali ambayo imeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa.

Akitoa mfano wa uondoshaji wa mashauri kwa takwimu, Mhe. Sarwatt alisema kuwa kwa mwaka 2015 jumla ya mashauri 894 yalipokelewa Mahakamani na mashauri 1030 yalimalizika na kubaki mashauri 795, hali hii inayoonesha kuwa kesi zilizofunguliwa zilimalizika zote na baadhi ya kesi za mlundikano za kipindi cha nyuma kushughulikiwa.

“Kwa mwaka 2016, jumla ya kesi 1347 zilifunguliwa, zilizomalizwa ni kesi 1464 na zilizobaki ni kesi 621, na kwa mwaka huu 2017 hadi kufikia mwezi Septemba jumla ya kesi 1062 zilifunguliwa huku 878 kumalizwa na kubaki na jumla ya kesi 526,” alifafanua Naibu Msajili.

Akiongelea juu ya mkakati wa kupambana na mlundikano, Mhe. Sarwatt alisema kuwa wamejiwekea utaratibu kama Kanda wa kufanya ufuatiliaji wa takwimu za umri wa mashauri kwa wiki ‘weekly tracking’ ili Majaji na Mahakimu waweze kushughulikia/kuyapa kipaumbele mashauri yanayokaribia umri wa kuwa mlundikano ‘back stopping.’ Pamoja na kufanya mikutano ya wadau ya mara kwa mara ili kuongea lugha moja ya kutokuwa na mlundikano.

“Lengo letu Kanda ya Tabora ni kuondoa kesi zote za Mlundikano ili tuweze kubaki na kesi zilizofunguliwa kwa mwaka huu 2017 tu,” alisisitiza Mhe. Sarwatt.

Katika kuhakikisha kuwa Mahakama ya Tanzania inatekeleza wajibu wake wa utoaji haki kwa wananchi na vilevile inatekeleza ipasavyo nguzo namba mbili (2) ya Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa Mahakama (2015/2016-2019/2010) ya Upatikanaji na utoaji wa Haki kwa wakati,  Majaji Wafawidhi kupitia Mkutano wao uliofanyika tarehe 15 na 16, Septemba,2017 waliazimia kuwa Mahakama zote nchini zimalize mlundikano wa mashauri yote ya muda mrefu ifikapo Desemba 15, 2017.