Home / News / Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara yamaliza mlundikano wa Mashauri ya kwa asilimia 86.

Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara yamaliza mlundikano wa Mashauri ya kwa asilimia 86.

Na Nurdin Ndimbe

 Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara imefanikiwa kwa asilimia 86 kumaliza kesi zote zenye umri unaozidi miaka miwili Mahakamani katika Kanda hiyo.

Akizungumza hivi karibuni Mjini Mtwara Naibu Msajili-Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe.Hussein Mushi alisema kuwa, Kanda ya Mtwara ilianza zoezi la usikilizwaji wa  mashauri ya zamani mapema kabla ya mpango huu maalumu wa kumaliza mlundikano wa mashauri.

Zoezi la uondoshaji mashauri nchini ulianza rasmi katika kanda zote Aprili 24, mwaka huu. “Kwa upande wetu zoezi la kumaliza mlundikano wa mashauri kwa Kanda yetu tulianza mapema kabla ya mpango huu mkubwa , Machi 7 mwaka huu tayari tulikuwa na kesi 15 zilizokuwa zimepangwa kusikilizwa’’ alisema Bw.Mushi.

Kati ya kesi hizo kesi 7 zilizobaki zilingizwa kwenye mpango Maalum ya kumaliza mashauri ya zamani ambapo kesi 3 tayari zilikuwa zimeisha mpaka tarehe Mei, 23.

“Kwa ujumla mashauri yote yaliyofunguliwa katika Kanda ya Mtwara yalikuwa 32 ambayo ni ya jinai, madai pamoja na ardhi” alisisitiza Naibu Msajili huyo.   Ukilinganisha yale tuliyoanza  nayo pamoja na nyongeza ya mpango maaalum ‘Backlog Clearance’  utaona tuna wastani wa 86% ya umalizaji wa mashauri kwa kanda yetu na nakuhakikishia kwa upande wa jinai na madai tutaendelea nayo kwa pamoja mpaka tutamaliza kama sio yote kabla ya Mwezi wa Sita kwa kesi zote zenye umri wa miaka miwili’’ alisisitiza Bw.Mushi.

Hata hivyo alisema kuwa, changamoto kubwa kwa kesi za jinai katika kanda ya Mtwara ni kwa upande wa mashtaka kukata rufaa na kuzifanyia matangazo ili ziendelee. “Jumla ya kesi zilizokatiwa rufaa ni 23 hadi kufikia Mei 2017 kati ya hizo 13 ni zamani kuanzia Mwaka 2013 kesi 1, 2014 kesi 3 na 2015 kesi 9” alifafanua.

Kuhusu upatikanaji wa nakala za hukumu, Naibu Msajili huyo alisema licha ya changamoto zilizopo katika Mkoa wa Mtwara, na Kanda yake kwa ujumla imekuwa ikitoa nakala za hukumu pamoja na mienendo ya kesi kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa idadi ya Wahe.Majaji pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi, lakini kwa Mhakama za Wilaya bado kuna matatizo ya uhaba wa Mahakimu kwani kwa ujumla kanda ina Mahakimu Wakazi 24 tu ukilinganisha na mahitaji.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni kwa wananchi kujichukulia sheria mkononi kwani ikumbukwe wakati wa mchakato wa ujenzi wa bomba la mafuta toka Mtwara hadi Dar Es Salaam Mahakama mbili za Mikindani na Mtwara Mjini zilichomwa moto na wananchi wenye hasira kali.

Aidha changamoto nyingine ni uhaba wa majengo ya Mahakama kwani hata Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara inatumia jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mtwara.

Akizungumzia kuhusu mlundikano wa Mashauri kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi/Mkoa Mtwara, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe.Elizabeth Missana alisema kuwa,katika Mkoa huo mlundikano wa kesi sio mkubwa, hivyo wao kwa mwaka mzima kesi zilizo na zaidi wa miezi 12 ni kesi 10 tu na tayari kesi 6 zilishatolewa maamuzi na kubaki kesi nne (4).

“Kwa ujumla kuanzia Januari hadi Aprili 2017, jumla ya mashauri 511 yalifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi/Mkoa Mtwara na 454 yalimalizika hii ni sawa na wastani wa 75.6% ya mashauri yote yaliyofunguliwa” alieleza Mhe. Missana.

Mhe.Missana. aliongeza kuwa; kwa mwaka 2016, jumla ya mashauri 1397 yalifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa, hivyo wastani wa umalizwaji wa mashauri kwa mkoa huo ni 99.5% nje ya mpango huu maluum wa umalizwaji wa mashauri ya zamani ambapo kuna kesi 3 bado hazijatolewa maamuzi. Mahakama ya Mkoa wa Mtwara ina jumla ya  wafanyakazi 164 wa kada mbalimbali ikiwemo Mahakimu 24.

Mahakama ya Tanzania ipo katika maboresho ya maeneo kadhaa mojawapo ikiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki nchini ili wananchi waweze kuufanya Mhimili huu kama kimbilio la upatikanaji wa haki.

Katika kuhakikisha kuwa Mahakama inafikia malengo yake, hivi sasa Mhimili huu upo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake ambao kwa ujumla umejikita katika kuboresha huduma zitolewazo na Mahakama kwa ujumla hususani suala ya utoaji haki ambalo ndio Jukumu muhimu linalosimamiwa na Chombo hiki.

Kwa minajili hiyo, Kanda ya Mtwara ni moja ya Kanda 14 za Mahakama Kuu, na ngazi nyingine za Mahakama nchini ambayo inatekeleza agizo lililotolewa na Makao Makuu- Mahakama la kuhakikisha kuwa zinamaliza mlundikano wa mashauri Mahakamani na tatizo la msongamano wa kesi kuwa historia katika Mahakama zetu.