Home / Latest News / MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA KAZI YAKUTANA NA WADAU WAKE KUJADILI NAMNA BORA YA KUTATUA MIGOGORO YA KAZI

MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA KAZI YAKUTANA NA WADAU WAKE KUJADILI NAMNA BORA YA KUTATUA MIGOGORO YA KAZI

Mahakama ya Tanzania ipo katika jitihada mbalimbali za kuhakikika kuwa inamaliza mlundikano wa  mashauri ya Migogoro ya kazi  ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano ya karibu na Wadau wake ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Akifungua Warsha ya siku tatu ya Wadau wa masuala ya Kazi kujadili juu ya Utatuzi na Usuluhishi wa Migogoro ya Kazi mapema Mei 14, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere alifungua alisema lengo ni kuwa  na uelewa wa pamoja jinsi ya kutatua migogoro ya kazi.

“Tumewaita Wadau wetu ambao tunafanya nao kazi kwa karibu ili kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya kazi ili wote twende pamoja katika kutatua migogoro hiyo,” alisema Mhe. Jaji Nyerere.

Jaji Mfawidhi aliendelea kusema kuwa kuna changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo katika uondoshaji wa mashauri ya kazi mojawapo ikitokana na upande wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo kuna changamoto ya rasilimali fedha, rasilimali watu na kadhalika zinazopelekea kuchelewa kwa mashauri hayo.

Mbali na changamoto hizo kwa upande wa CMA, Mhe. Jaji Nyerere alibainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea malalamiko ya Mahakama ya Kazi ni kutokana pia na uchache wa Majaji katika Divisheni hiyo.

Hata hivyo, Mhe. Jaji Nyerere alisema kuwa ili kukabiliana na upungufu wa Majaji wa Divisheni hiyo, Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania kupitia tamko la Aprili 30, 2018 ameelekeza kuwa kila Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania atasikiliza mashauri ya masuala ya kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa katika Warsha hiyo Wadau hao watafundishwa juu ya Sheria mbalimbali za masuala ya kazi.

“Katika Warsha hii pamoja na Wadau tutapata wasaa wa kuwa na uelewa wa pamoja juu ya Sheria mpya mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sheria ya Mahusiano kazi ya mwaka 2004,” alieleza Mhe. Kihwelo.

Warsha hii ya Siku tatu inayofanyika katika Kituo cha Mafunzo kilichopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshirikisha baadhi ya Wadau mbalimbali wakiwemo Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Chama cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO).

Katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020) Mahakama ya Tanzania imejielekeza kuboresha huduma zake kupitia ushirikishaji wa Wadau mbalimbali.

Warsha hii imeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto chini ya Ufadhili wa Fedha za Mradi wa Benki ya Dunia.