Home / News / Mahakama kuanzisha Kituo cha Mafunzo- Dar es Salaam

Mahakama kuanzisha Kituo cha Mafunzo- Dar es Salaam

Mahakama ya Tanzania inakusudia kuanzisha kituo cha Mafunzo kwa ajili ya watumishi wake pamoja na wadau ili kuwaongezea ujuzi utakaosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama.

Kituo hicho kinachojengwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam kitawaunganisha watumishi wa Mahakama na wadau katika mafunzo kwa njia ya video (video conferencing).

Akizungumzia Kituo hicho, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya Maboresho ya huduma za Mahakama ambacho pia wadau wa Mahakama watakuwa ni sehemu ya mafunzo yatakayokuwa yakitolewa.

Alisema badala ya Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau wa Mahakama kwenda kupata baadhi ya mafunzo kwenye chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), baadhi ya mafunzo watakuwa wakiyapata katika kituo hicho.

Naye Mratibu wa Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na maboresho ya Huduma za Mahakama Mhe. Zahara Maruma alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia nguzo ya pili ya Mpango huo, Majaji na Mahakimu hupatiwa mafunzo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

DSC08038

Akizungumzia nguzo ya tatu ya Mpango huo, Mhe. Maruma alisema nguzo hiyo inahusiana na urejeshaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama ambapo kupitia kituo hicho wadau wa Mahakama watahusishwa kwenye Mafunzo mbalimbali ili kurahisisha suala la upatikanaji wa Haki.

Kuhusu suala la matumizi ya Teknolojia ndani ya Mahakama, Mratibu huyo alisema hivi sasa Mahakama inao mpango wa kujenga vituo vya aina hiyo kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuunganisha Mahakama zote nchini kwa njia ya video (video conferencing).

Ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ulioanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 78. Aidha, Jengo la kituo hicho cha mafunzo linajengwa kwa kutumia teknolojia ya gharama nafuu iitwayo Moladi na linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki nane.

KJM4