Home / News / Mafunzo ya Huduma kwa Wateja kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania yaendelea kwa awamu ya pili

Mafunzo ya Huduma kwa Wateja kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania yaendelea kwa awamu ya pili

Mafunzo maalumu ya siku mbili yahusuyo huduma kwa wateja na haki ya kupata taarifa kwa watumishi wa Mahakama, yameanza leo katika hoteli ya Flomi mkoani Morogoro ikiwa ni muendelezo wa mafunzo yaliyozinduliwa mwaka jana na Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma Mhe. Crecensia Makuru.

Lengo Kuu la mafunzo haya likiwa ni kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama kwa kuwapa mbinu na mikakati mbalimbali itakayowasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Mahakama ya Tanzania kwa sasa inaendelea na maboresho ya utendaji kazi wake kama sehemu ya kuhakikisha kuwa inatoa huduma iliyo bora na kwa wakati. Moja ya maeneo yaliyoonekana kuwa na udhaifu ni namna masijala za Mahakama zinavyopokea na kutunza nyaraka na hata zinavyohudumia wateja kwa ujumla.

Walengwa wa mafunzo haya ni  watumishi wa kada mbalimbali za mahakama wakitokea kanda ya Mashariki inayounganisha mikoa ya Pwani, Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro.

Miongoni mwa mada zinazowasilishwa ni “Nini maana ya uhuru wa Habari na habari ni Nini?, Huduma kwa wateja na ujuzi wa mawasiliano kwa watumishi wa Umma, Njia mbalimbali za upatikanaji wa taarifa katika Taasisi za Umma na Sheria ya utoaji wa  habari katika Mahakama”.

Mafunzo haya yameandaliwa na kufadhiliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) pamoja na Taasisi ya Friedrick Ebert Stiftung (FES) ofisi ya Tanzania.

 

edited