Home / News / MAFUNZO KWA MAHAKIMU, WAJUMBE WA MABARAZA YA KATA YATOLEWA MKOANI TABORA

MAFUNZO KWA MAHAKIMU, WAJUMBE WA MABARAZA YA KATA YATOLEWA MKOANI TABORA

Na Aisha Abdallah, Mahakama Kuu Tabora

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Mhe. Salvatory Bongole amefungua rasmi Mafunzo ya Mahakimu na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata mkoani humo yanayolenga kuwajengea uwezo wa kuyasimamia mabaraza ya kata katika utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa sheria.

Akifungua Mafunzo hayo mapema Oktoba 08, katika Ukumbi wa Katibu Tawala, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Bongole aliwaelezea washiriki wa mafunzo hayo kuwa ni muhimu kwa sababu yataleta uelewa wa pamoja kati ya Mahakama na Mabaraza ya Kata juu ya mamlaka ya Mahakama na Mabaraza katika utoaji haki.

Aidha katika hotuba yake ya ufunguzi,Mhe. Jaji Mfawidhi huyo pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa kumsikiliza mtu kabla ya kutoa maamuzi na kuwaasa wanasemina kuyatekeleza mambo yote watakayojifunza katika semina hiyo.

“Kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama suala la ushirikishwaji wa Wadau limepewa kipaumbele ili tuweze kufanikisha huduma ya utoaji haki”, alisema Mhe. Jaji Bongole.

Katika semina hiyo, Mahakama imewashirikisha Wanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora na Halmashauri ya Manispaa-Tabora kama viongozi wa Mabaraza ya Kata.

Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Washiriki ni Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kutoka Tabora Mjini, Urambo, Nzega na Igunga pamoja na wajumbe wa Mabaraza ya Kata na Wanasheria wa Halmashauri ya Manispaa na wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.