Home / News / JAJI MKUU WA TANZANIA ATEMBELEWA NA WAKILI MKUU WA SERIKALI

JAJI MKUU WA TANZANIA ATEMBELEWA NA WAKILI MKUU WA SERIKALI

Na Magreth Kinabo

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Profesa Ibrahim Hamis Juma, ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano  na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ili kuiwezesha kufanya majukumu ipasavyo.

Kauli hiyo imetolewa mapema Agosti 23,wakati Wakili Mkuu wa Serikali  Dkt. Julius Mashamba na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali ,Dkt. Ally Possi, akiwemo  Mwanasheria Mwandamizi wa Ofisi  ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mark  Mulwambo walipomtembelea Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.

“Kazi yenu nyingine  ni kuzifahamu sheria na kuangalia  na kuzifuatilia,” alisema  Jaji Mkuu.

Aliongeza kwamba Taasisi hii  ni muhimu, na itakuwa inafanya  kazi ya kushauri katika masuala yanayohusu  sheria, hivyo itasaidia kuweka nidhamu katika utendaji kazi unaozingatia misingi ya sheria.

Profesa  Juma alisema  watumiaji wa sheria ni wengi, hivyo suala la kurekebisha sheria linahitaji busara.

Awali Wakili Mkuu huyo wa Serikali, Mashamba alisema aliomba ushirikiano kati ya ofisi yake na Mahakama ya Tanzania  katika Mfumo  wa Kuhifadhi Takwimu  za Mashauri kwa njia ya Kielektroniki na mafunzo ili kuweza kusaidia kuimarisha ofisi hiyo.