Home / News / Jaji Mkuu awakubali na kuwaapisha jumla Mawakili Wapya 296 na Kufanya idadi yao kufikia 6,536 Nchini

Jaji Mkuu awakubali na kuwaapisha jumla Mawakili Wapya 296 na Kufanya idadi yao kufikia 6,536 Nchini

Na Lydia Churi, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili nchini kutokuwa sehemu ya rushwa na badala yake waisaidie Mahakama ya Tanzania katika kupambana na rushwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia Maadili ya taaluma hiyo.

Akizungumza wakati wa sherehe za 57 za kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya zilizofanyika leo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amewataka Mawakili kutokutumia vifungu vya sheria na kanuni ili kuchelewesha upatikanaji wa haki kwa kuwa suala la upatikanaji wa haki hutegemea Mawakili.

“Katika karne hii ya 21 ni muhimu kwa Mawakili kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa huduma za karne hii huvuka mipaka ya nchi”, alisema Jaji Mkuu.

Prof. Juma pia amewashauri Mawakili kusoma na kuzifahamu sheria za kimataifa ili wawe na upeo mkubwa katika kushughulikia kesi hasa zile zinazohusisha nchi zaidi ya moja. Baadhi ya kesi hizo ni zile zinazohusu mipaka ya nchi, makosa ya kimtandao (cyber Crimes) pamoja na zile zinazohusu Maliasili.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliyataka baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya Mawakili na wananchi kuwashitaki kuwa ni kutoa siri za wateja, kughushi nyaraka, kutayarisha mikataba zaidi ya moja kwa lengo la kudanganya, Wakili kuchukua kesi bila ya ruhusa ya mteja, kuwaibia wateja kwa kuwatoza fedha nyingi, kuwadanganya, kuchukua kesi yenye maslahi binafsi pamoja na uzembe.

Prof. Juma pia amewashauri Mawakili wapya kuhakikisha wanashirikiana na taaluma nyingine wanapofanya kazi zao ilikurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wateja wao.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amewataka Mawakili wapya kutosubiria kuajiriwa na Serikali na badala yake wajiajiri na kutoa huduma mikoani na siyo Dar es Salaam peke yake.

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Godwin Ngwilimi amewataka Mawakili nchini kutekeleza wajibu wao kwa kufuata misingi ya haki na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Jumla ya Mawakili wapya 296 wamekubaliwa na kuapishwa leo na kufanya idadi ya Mawakili nchini kufikia 6,536. Aidha, sherehe za kuapishwa na kukubaliwa kwa  Mawakili zimefanyika kwa mara ya 57 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo mwaka 1986.