Home / News / Jaji Mkuu awaasa Wahitimu wa Sheria kujiendeleza kitaaluma

Jaji Mkuu awaasa Wahitimu wa Sheria kujiendeleza kitaaluma

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma amewataka wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kujiendeleza katika fani ya Sheria kwa kuwa na hitaji  na hamu ya kujiendeleza zaidi toka kiwango kimoja cha elimu hadi cha juu zaidi.

Prof. Juma ameyasema hayo mjini Lushoto katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama ambapo wahitimu 150 walitunukiwa Stashahada ya Sheria na wengine 142 walitunukiwa  Astashahada ya Sheria.

Amesema kwamba wahitimu hao na wasomi wengine wa sheria nchini hawana budi kuzingatia kasi ya sasa ya maendeleo ya dunia na umuhimu wa elimu katika ulimwengu wa leo na kongeza kwa kutokana na hali hiyo ni lazima wajiendeleze zaidi katika fani hiyo.

“ Ninawaasa popote pale mtakapokuwa someni na kujiendeeleza na  jifunzeni  mambo mapya kila siku, karne hii ya 21 ni karne ya teknolojia na habari , ni karne inayowategemea wahitimu wanaojiendeleza  na kujifunza kila siku, jiendelezeni hadi kufikia viwango vya juu kulingana na kushindana na yeyote yule duniani , kumbukeni kuwa ajifunzae haachi kujua, naomba mtambue kuwa kujifunza ni kwekeza,” alisisitiza Jaji Mkuu

Mhe. Jaji Mkuu pia amewaasa wahitimu hao kuwa watakapopata kazi wahakikishe wanafanya kazi kwa bidii, uaminifu na kwa wakati ili kulinda maslahi ya Taifa na hivyo kuwa mabalozi wazuri wa Chuo.

Awali akimkaribisha Jaji Mkuu katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mhe. John Mrosso amesema ndani ya miaka miwili chuo kimepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kujielekeza katika masuala ya utafiti na ushauri ambapo inao wanataaluma 22 ambao wamejikita katika eneo hilo na kuwezasha wahitimu wa chuo hicho kupata ajira serikalini na kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ili kujiendesha.

Nae Mkuu wa Chuo hicha Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo alisema katika mwaka huu chuo kimefanikiwa kutoa wanafunzi 26 waliopata daraja la kwanza hali ambayo imetokana na kujitoa kwa wahadhiri na kujituma kawa wanachuo hao na hivyo kukiletea sifa chuo.

Amesema kama chuo wamepanga kuimarisha kitengo cha mafunzo, kuimarisha vyanzo vya mapato, kujenga uwezo wa watumishi ili kuhakikisha kinatekeleza kwa vitendo dhamira ya kuanzishwa kwa chuo ya kuboresha utendaji kazi  wa Mahakama kupitia mafunzo kwa Maafisa wa Mahakama pamoja na wasaidizi wao na wadau wote wa sekta ya sheria nchini.