Home / Latest News / JAJI MKUU AFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA MAJAJI WAPYA WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA NA ZANZIBAR

JAJI MKUU AFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA MAJAJI WAPYA WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA NA ZANZIBAR

Jaji Mkuu wa Tanzania , Mhe. Profesa Ibrahim Juma akifungua mafunzo endelevu ya wiki ya tatu kwa ajili ya majaji wapya yaliyoanza leo kwenye Kituo cha Mafunzo , kilichopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar e s Salaam.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewatsaka Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kufanya kazi kwa kiwango cha juu kwani wananchi wana matarajio makubwa na matokeo ya kazi zao.

Alisema hayo mapema Mei 07 alipokuwa akifungua Mafunzo Elekezi ya Waheshimiwa Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kituo cha Mafunzo kilichopo katika eneo la Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu-Dar es Salaam.

“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka, wakati ambao Mahakama ya Tanzania ipo katika maboresho mbalimbali, hivyo ni vyema ninyi Majaji kupitia utendaji kazi wenu mtumike kubadili taswira ya Mahakama,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa lengo la Mafunzo hayo kwa Waheshimiwa Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni kuwapa miongozo na taratibu mbalimbali katika ufanyaji kazi ya Ujaji.

“Mafunzo haya enedelevu yanayotolewa na Mahakama kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni muhimu katika utendaji kazi kwani baadhi ya Majaji walioteuliwa wametoka sehemu mbalimbali hivyo ni vyema kuwafunza ili kuwa na uelewa wa pamoja katika utendaji kazi,” alifafanua Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu pia amewataka Wahe. Majaji kufanya kazi kwa kuangalia pia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

Jaji Mkuu wa Tanzania , Mhe. Profesa Ibrahim Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo endelevu kwa ajili ya Majaji wapya yaliyoanza leo kwenye Kituo cha Mafunzo , kilichopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar e s Salaam.

Mafunzo hayo yalioshirikisha jumla ya Majaji wapya 14, 12 kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania na wawili (2) kutoka Mahakama Kuu-Zanzibar yatafanyika kwa muda ya Wiki tatu, na katika mafunzo hayo mada mbalimbali zitatolewa ikiwa ni pamoja na Matumizi ya TEHAMA Mahakamani, Makosa ya Kimtandao nk.

Mafunzo haya yanaendeshwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto chini ya ufadhili wa fedha za Mradi wa Benki ya Dunia.