Home / News / JAJI MATOGOLO AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI ILI KUJENGA TASWIRA CHANYA YA MAHAKAMA

JAJI MATOGOLO AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI ILI KUJENGA TASWIRA CHANYA YA MAHAKAMA

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Mhe. Firmin Matogolo akifungua kikao kazi cha Watumishi wa Divisheni yake ambacho pia kilihusisha Mafunzo ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16-2019/20) leo jijini Dar es salaam.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Mhe. Firmin Matogolo amewataka Watumishi wa Divisheni hiyo kufanya kazi kwa kufuata Maadili ili kujenga taswira chanya ya Mahakama ya Tanzania kwa wananchi.

Akifungua kikao kazi cha Watumishi wa Mahakama hiyo ambacho pia kilijumuisha Mafunzo kuhusu  Mpango Mkakati wa miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16 -2019/20) kwa watumishi hao, Jaji Matogolo aliwataka watumishi kuzingatia suala la maadili na kulipa kipaumbele kama ambavyo jamii inatarajia kutokana na umuhimu wa Divisheni hiyo.

“Kuweni makini mnapotekeleza majukumu yenu kutokana na umuhimu wa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwani Serikali pamoja na Wananchi wametuamini sisi, alisema”

Jaji Matogolo pia aliwaasa watumishi wa Mahakama hiyo kujifunza kwa bidii na kuufahamu Mpango Mkakati wa Mahakama ili waweze kuutekeleza ipasavyo na kuboresha huduma wanazotoa kwa wananchi.

Alisema pamoja na changamoto zinazoikabili Divisheni hiyo mpya za upungufu wa watumishi, Jaji Matogolo amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii wakati Mahakama ya Tanzania ikizitafutia majibu changamoto hizo ambapo alisema Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unalenga pia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Mahakama.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Mhe. Charles Magesa akizungumza na Watumishi wa Divisheni hiyo wakati wa kikao kazi.

Akiwasilisha Mada juu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Bwn. Benjamin Mlimbila pia alisisitiza suala la Maadili kwa watumishi na kuwataka kuzingatia kipembele katika nguzo ya Tatu ya Mkakati huo kinachowataka kuimarisha tabia, maadili na miiko ya watumishi wa Mahakama.

Wakati huo huo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Mhe. Charles Magesa pia aliwataka watumishi hao kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa kujituma pamoja na kutii Mamlaka katika maeneo yao ya kazi.