Home / News / JAJI KIONGOZI ATEMBELEA MAHAKAMA MOROGORO

JAJI KIONGOZI ATEMBELEA MAHAKAMA MOROGORO

Na Victor Kitauka, Mahakama ya Mkoa Morogoro

Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.Eliezer Feleshi amewataka Watumishi wa Mahakama ya Mkoa Morogoro kufanya kazi kwa umoja, bidii, ushirikiano na kupendana kwani wanatumia muda wao mwingi wakiwa kazini.

Jaji Kiongozi aliwakumbusha watumishi wa Mahakama hiyo alipotembelea Mahakama ya Mkoa huo kujionea hali ya utoaji haki huku akisisitiza kuwa jukumu kuu la Mahakama ni kutoa  haki kwa  kwa wakati hivyo amewata kuwahudumia wananchi kwa weledi na bidii  ili kuondoa malalamiko ya  wananchi dhidi ya mahakama.

Mnamo tarehe 16/8/2018, Mhe. Jaji Kiongozi alifanya ziara katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro na kuongea na Watumishi wa Mahakama hiyo.

Awali, Mh Jaji Kiongozi kabla ya kukutana na  kuongea na watumishi wa mahakama alipata wasaa wa kutembelea kiwanja cha Mahakama kilichopo eneo la Kihonda na kujionea eneo ambalo linatarajiwa kujengwa jengo la Mahakama Kuu Morogoro ambapo aliridhishwa na ukubwa wa kiwanja hicho na  eneo kilipo kiwanja hicho.

Aidha Mhe.Jaji Kiongozi  aliwaonya watumishi  wazembe kazini na wanaojiusisha na vitendo vya rushwa  kuwa Mahakama  haitomvumilia Mtumishi yeyote mzembe na anayejihusisha na  vitendo vya rushwa

Vilevile Mhe. Jaji Kiongozi, aliwataka  Hakimu Mkazi Mfawidhi na Mtendaji wa mahakama hiyo  kutosita kutoa taarifa na kuwachukulia hatua watumishi wote wazembe na wanaojiusisha na vitendo vya rushwa na itakapogundulika kuwa viongozi wameshindwa  kuwachukulia hatua watumishi basi  uongozi wa mahakama hautosita kuwachukulia hatua viongozi hao kwa kushindwa kuchukua  hatua dhidi ya   watumishi wa chini yao ambao ni wazembe na wala rushwa kwani wanachafua taswira ya Taasisi.

Kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi kuongea na watumishi, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Mh.Elizabeth J.Nyembele alielezea kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro imefanikiwa  mpaka sasa kusikiliza na kutolea maamuzi zaidi ya asilimia 75 ya mashauri yote yaliyopo mahakamani hapo.

Kwa upande wa  changamoto  zinazoikabili Mahakama Hakimu Mkazi Mfawidhi  alimueleza Jaji kiongozi kuwa upelelezi hasa katika kesi za uhujumu uchumi,kutokufanyika kwa vikao vya  mahakama kuu Morogoro kwa siku za hivi karibuni  imeipelekea msongamano wa mahabusu  katika gereza la mahabusu mkoa wa morogoro na  uhaba wa watumishi katika kada tofauti jambo linalopolekea kupunguza ufanisi katika utendaji wa kazi.

Mwisho, Jaji Kiongozi Mh Jaji dkt Feleshi aliwataka Hakimu Mkazi Mfawidhi na Mtendaji wa Mahakama ya Morogoro kuendelea kufanya kazi kwa  uwazi, ukaribu na kuwashirikisha watumishi wa chini ili kuondoa malalamiko na kero za watumishi na aliwaagiza kushughulikia kero na malalamiko ya watumishi zilizo ndani ya uwezo wao na zile ambazo zipo nje ya uwezo wao waziwasilishe ngazi za juu kwa utekelezaji.