· Aitisha Kikao cha Wadau kueleza mikakati ya Mahakama na kuweka mikakati ya pamoja
· Asema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kufikia Dira ya Mahakama sanjari na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
· Asema mashauri hayo yana mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa Nchi
· Awasihi Wadau wa Haki Madai kutoa ushirikiano na kila mmoja kutekeleza wajibu wake ipasavyo
· Wadau wakiwemo Tume ya Mipango, Benki Kuu, Mwanasheria waipongeza Mahakama kwa hatua hiyo
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Majaji na Mahakimu nchini kukamilisha mashauri yote ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Ardhi ifikapo tarehe 15 Desemba, 2025, huku akiwataka wadau wote wa haki madai kutoa ushirikiano wa dhati kwa kila mmoja kuwajibika ipasavyo ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Mahakama ya Utoaji Haki Sawa mapema ipasavyo ili kuchangia kukuza uchumi wa nchi na kuvutia mazingira ya uwekezaji.
Akizungumza jana tarehe 08 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano wa Wadau kuhusu Mikakati na Hatua zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki na Ushindani wa Kibiashara na Ardhi, Mhe. Masaju alisema mkakati huo unaenda sambasamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika eneo la kuboresha utoaji haki.
“Sisi Mahakama ni wadau muhimu katika hili eneo ambalo linagusa uchumi na tumejipanga, Mahakama tunatambua wajibu wetu kwenye utatuzi wa migogoro, ndio maana tumeitisha kikao hiki ili kuwashirikisha mikakati tunayochukua sisi na hatua tunazozichukua kuhakikisha kwamba mashauri haya ambayo yapo mahakamani yanaamuliwa mapema ipasavyo ili watu waendelee na shughuli zao, fedha ambazo zimefungiwa huku ziweze kufunguliwa ziingie kwenye mzunguko wa uchumi ili ziweze kuwanufaisha Watanzania,” alisema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju alieleza kuwa, azma hiyo itafanikiwa endapo Mahakama itapata ushirikiano wa wadaawa wanaokuja mahakamani ambapo alisema, “tunataka kama vile ambavyo Mahakama imejitoa hata kwa rasilimali kidogo sana na wakati fulani kulazimika kuchukua hela fulani kwenye matumizi fulani kuzileta huku, lakini ukweli ni kwamba sisi haya tunafanya kwa nia njema na hii ikifanikiwa itatusaidia sana kwenda mbele, hivyo tumejipanga tunataka twende, hatutaki kukwamishwa na mtu.”
Kadhalika, Jaji Mkuu alisema kwamba, pamoja na kuwashirikisha Wadau hao kuhusu mikakati ya Mahakama ya kushughulikia migogoro yote na kuimaliza mapema ipasavyo amewaeleza kuwa na Dira ya Mahakama isemayo; ‘Haki sawa kwa wote mapema ipasavyo’ nayo inataka kutoa haki mapema ipasavyo, lakini katika kutekeleza Dira hiyo, Mahakama inajifungamanisha na Dira ya Taifa ya Maendeleo, hivyo ni muhimu kwa Wadau kushirikiana ili kwa pamoja kufanikisha Dira hizo.
Mhe. Masaju aliongeza kuwa, katika jitihada za kuhakikisha huduma za haki zinawafikia wananchi kwa karibu zaidi, Mahakama imepanga kushusha huduma za Mahakama ya Rufani katika Kanda na kwa kuanzia itakuwa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mikoa mingine yenye mashauri mengi.
“Kwahiyo sasa katika kuwashirikisha hii mikakati yetu tutapata fursa na pengine na ninyi kujua kinachoendelea hapa, mtatusaidia na ninyi kuboresha wapi ambapo hatufanyi vizuri, muwe huru mseme ndio maana ya mkutano, muwe huru labda mtusaidie hata kuboresha mikakati yetu, lakini pia pale ambapo hatufanyi vizuri mtueleze kwa sababu kufanikiwa kwa Taasisi moja kwenye suala hili ambalo ni mtambuka Taasisi nyingine zikiwa hazikufanikiwa hatutakuwa tumepiga hatua. Kwa hiyo tumewaita ili tushirikishane, tusemane hapa kwa nia njema ya kwenda mbele, tumewaita wote hapa mkiwa wote ni wahusika wakuu kwa mfano tumewaita watu wa TLS, Mabenki, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gavana wa Benki Kuu na wadau wengine,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu alisema kwamba, kupitia mkutano huo watapata fursa ya kuambiana madhaifu ya kila Taasisi lengo likiwa ni kwenda mbele. Ameeleza kuwa, “sisi wakati tunaweka hii mikakati ya kutekeleza wajibu wetu wa kutoa haki sawa mapema ipasavyo na ninyi sasa ambao ni wadau wetu mtusaidie namna gani mtaungana na sisi katika kulifanikisha hili ili wote twende pamoja.”
“Kwa ujumla mapinduzi makubwa yanahitajika katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hususani katika kubadilisha Sekta ya Umma kutoka kuwa mdhibiti kwenda kuwa Mwezeshaji wa biashara na uwekezaji na katika hii ya mwisho ndio na sisi pia tunaingia pale na Mahakama ina mchango mkubwa kwenye hili suala,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Mhe. Masaju aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutambua umuhimu wa Mahakama na kuiwezesha kufanya kazi zake vizuri, huku akiwataka wadau wengine kama Umoja wa Mabenki Tanzania (TBS), Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama na wadau wengine kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu bila kuzalisha migogoro.
Aidha, Mhe. Masaju alisema, mashauri hayo ni eneo ambalo linagusa masuala ya uwekezaji na biashara, “Na mimi ninachoweza kusema ni kwamba tumeanza utekelezaji wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Dira hii mnafahamu ina msingi mkuu ambao msingi mkuu unahusu Utawala, Amani, Usalama na Utulivu lakini na vipaumbele vyake ambavyo viko vinne, cha kwanza kabisa ni Utawala Bora na Haki, halafu cha pili Serikali imara za Mitaa na Ufanisi lakini kipengele cha tatu ni Uwajibikaji utumishi wa Umma lakini kipengele cha nne ni Amani, Usalama, Utulivu hivyo ndio vipaumbele vya msingi mkuu wa Dira.”
Aidha, Jaji Mkuu alieleza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imebeba nguzo tatu ambapo nguzo ya kwanza inahusu uchumi imara, jumuishi na shindani.
“Na mkiangalia haya mashauri ambayo sisi tumewashirikisha, mkakati ambao tunachukua yana mchango mkubwa sana katika Uchumi na unaposoma ukurasa 21 wa Dira hiyo inasema Uchumi imara, jumuishi na shindani ni moja ya nguzo kuu ya kujenga Taifa lenye ustawi kwani nguzo hii inafungua fursa za kiuchumi na hivyo kuweka mazingira ya kupunguza umaskini na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote, Uchumi imara utahakikisha kwamba maendeleo ya kiuchumi yanakua na taswira chanya kwa jamii na kuwanufaisha wananchi wote,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amesema katika moja ya vipengele vya nguzo hii ya Uchumi imara ni mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ambapo ukurasa wa 25 wa Dira; ‘Uchumi imara na endelevu unategemea kuwepo kwa mazingira mazuri ya kufanya biashara.’
Aidha, aliongeza kwamba, mwaka 2018, Tanzania ilizindua Mpango Mkakati wa Mageuzi ya Sheria ya kuboresha mazingira ya biashara nchini ambao ulilenga kuimarisha ufanisi katika mifumo ya kisheria, kurahisisha michakato ya usajili na usimamizi wa biashara na kuongeza uwazi na uwajibikaji ambapo vipengele vikuu ilikuwa ni kupitia upya sheria na kanuni, kupunguza kodi na ada zisizo na ufanisi na kuboresha uwezo wa Taasisi za kudhibiti ili kuzifanya zijielekeze zaidi katika kuchangia ukuaji wa Sekta ya Biashara badala ya kuweka mkazo katika makusanyo ya mapato pekee.
“Pamoja na juhudi hizo, changamoto mbalimbali zimeendelea kuyagubika mazingira ya biashara nchini ikiwemo gharama na muda mkubwa wa usajili na ukosefu wa mitaji, kikwazo kingine ni urasimu katika utendaji jambo linaloongeza muda ambao Wawekezaji wanachukua kukamilisha taratibu za awali za kuidhinisha biashara na uwekezaji,” amesema Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu amebainisha kuwa, uendeshaji wa biashara umeendelea kuwa na uthibiti uliokithiri ukiathiri utaratibu wa kodi na mapato kwa bidhaa zenye thamani kubwa, migongano ya Sera, Sheria na Kanuni na kuwepo kwa miingiliano ya majukumu ya Taasisi za Udhibiti, ambapo ameeleza kuwa, “suala hili limezifanya biashara kubeba mzigo mkubwa wa kodi, ada na ongezeko la gharama kutokana na masharti mengi ya leseni na vibali.”
Ameongeza kwamba, ili kushughulikia changamoto hizo ni lazima kujenga mazingira wezeshi ya kibiashara yatakayochochea ukuaji wa Uchumi na kuvutia uwekezaji na kwamba mageuzi hayo yanapaswa kurahisisha taratibu, kupunguza vikwazo vya kisheria, kuondoa tozo zisizo na tija na kufungamanisha Sera na Taasisi ili kuimarisha mazingira ya biashara yenye ushindani na ufanisi.
Kadhalika, Jaji Mkuu pia alisisitiza suala la uwajibikaji na uadilifu kwa Mahakama na wadau wote wa Haki Madai kuwajibika na kujituma ipasavyo, na kuweka wazi kuwa suala la kuwajibika ni suala la kikatiba hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika huku akitimiza malengo yake binafsi na yale ya pamoja.
"Kwetu sisi wenyewe huku Mahakamani tumekuwa na mafunzo na tunawajibishana, sasa na ninyi, wakati Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inazungumza juu ya uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hili suala ni la kikatiba, Ibara ya 25 ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hivi, 'kazi pekee ndio uzao tajiri wa mali katika jamii ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu na kila mtu ana wajibu wa (a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali na (b) kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria.'
Kupitia Mkutano huo Wadau hao wa Haki Madai walipata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na changamoto zilizopo na kuweka mikakati thabiti ya kuondokana na changamoto hizo na hatimaye kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Wadau mbalimbali waliohudhuria katika Mkutano huo ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msajili wa Hazina, Tume ya Taifa ya Mipango, Baraza la Ushindani, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Fedha, Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo maalum ya Kiuchumi (TISEZA), NBC, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Baraza la Rufani za Kodi, Chama cha Madalali Tanzania, na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.