· Awataka kutambua nafasi ya Mungu katika kazi zao
· Awasisitiza kufanya kazi nyingine halali za kujipatia kipato ikiwa ni pamoja na Kilimo, Ufugaji…
Na MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya huku akisema kuwa mafunzo hayo ambayo yatasheheni mada mbalimbali yatahudhuriwa na viongozi wa dini lengo likiwa ni kujenga uwajibikaji, uzoefu, kuimarisha ufanisi na kuongeza umahiri wa mahakimu wapya katika kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Masaju aliyasema hayo jana tarehe 07 Oktoba, 2025 wakati akifungua Mafunzo Elekezi yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi wapya 89 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“Nimeangalia ratiba yenu na mafunzo ambayo mtayapata kipindi hiki cha mafunzo elekezi, pamoja na mambo mengine yote yaliyoko pale nimevutiwa na siku ya pili ya mafunzo haya, pale kutakuwa na muda wa mazungumzo na Viongozi wetu wa dini wamealikwa kuja kuzungumza na ninyi na tumekuwa na utaratibu huu kwa sasa mwaka wa tatu kila tunapoapisha tunawaita hawa viongozi wa dini kuja kuzungumza na ninyi kuwatia moyo, kuwashauri,” alisema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju aliwaeleza Mahakimu hao kuwa, Mwenyezi Mungu ametoa maelekezo ya namna ya kuishi na namna ya kuhusiana na yeye na namna ya kuhusiana na watu wengine.
“Mimi niwashauri watakapokuja kuzungumza na sisi tuwasikilize kwa makini na kama kuna maswali waulizeni lakini wamekuja kutujenga sana, mwelekeo wetu kuanzia sasa tangu tulipokula kiapo imejikita namna tutazingatia miongozi ya Mwenyezi tunapotekeleza majukumu yetu ya utumishi wa umma na sheria zile za Mungu hazipingani sana na zile za kwetu, kwa mfano sheria za Mungu zinatuhimiza tupendane lakini pia zinatuhimiza tusile rushwa, zinatuhimiza sisi tulio na majukumu ya kutoa haki tusipendelee,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju aliongeza kwa kuwakumbusha Mahakimu kuheshimu siku za ibada za kila dini ambapo alisema, “Na sisi hao watu wa dini tunawapa kipaumbele sana na utakumbuka hapa kila mmoja ana dini yake na siku ya kufanya ibada, pengine wapo ambao wanafanya ibada siku ya Ijumaa, wengine siku za Jumamosi lakini pia wapo wanaofanya ibada siku za Jumapili na pengine wapo wanaofanya ibada siku nyingine pia lakini siku mahsusi ambazo zimetengwa kwa ajili ya ibada hatujakatazwa kufanya ibada kila siku, kimsingi ibada ni haki yako.”
Alisema, madhehebu ya dini yana mchango mkubwa katika katika Taifa kwa ajili ya usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii na umoja wa kitaifa.
Jaji Mkuu alibainisha kuwa, ‘Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema, ‘uhuru wa kuamini dini mtu atakayo’, Ibara ndogo ya 1 inasema kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake, Ibara ndogo ya 2 inasema kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiyari la mtu binafsi na shughuli za uendeshaji wa jumuiya ya dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi……’
Kadhalika, Mhe. Masaju alisisitiza juu ya suala la Uwajibikaji ambalo ni moja ya kipaumbele cha tatu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Aliongeza pia kufanya kazi kwa uaminifu.
"Suala la uwajibikaji, baadae mtakuja kusoma Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, moja ya kipaumbele kikubwa sana ni uwajibikaji, uwajibikaji ni kipaumbele cha tatu katika ile misingi mikuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uwajibikaji kwa watumishi wa Umma," alisisitiza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju aliongeza kwamba, suala la Uwajibikaji ni takwa la kisheria na kuwahimiza Mahakimu Wakazi kufanya kazi kwa kujituma na kwa uaminifu katika utekelezaji wa shughuli halali na uzalishaji mali pamoja na majukumu mengine kwa kuzingatia Dira ya Mahakama ya Utoaji haki sawa kwa wote mapema ipasavyo.
"Na hapo ndipo tunapopata sisi utekelezaji wa Dira yetu ya Mahakama inayosema, Haki sawa kwa wote mapema ipasavyo, tunaishi hiyo Dira hatutaki haki icheleweshwe na nyie wenyewe mnasema haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa, tumeweka utaratibu sasa tungependa zile kesi ziwe zinamalizika mapema sana isipokuwa kuwe na sababu za msingi," alisema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu aliwataka pia kutimiza nidhamu ya kazi na kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na kuvaa vizuri na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya mtu binafsi kama vile kilimo, ufugaji na yale malengo yaliyowekwa na Sheria.
“Utapimwa kwa maadili yako pia hata unavyovaa, wewe unategemewa kuwa kioo, na nimeona watu wengine wamevaa vizuri hapa na wamejistiri na vichwa vyao, hayo ni mavazi ya heshima, endeleeni kuvaa hivyohivyo msiseme wananipima wananiona mimi sijui mshamba,” alisisitiza.
Mhe. Masaju pia aliwataka kuzingatia vitendea kazi vya aina mbili ambavyo ni ‘hardware’ na software’, ambavyo ni pamoja na kompyuta, meza, vitabu vya sheria na vingine, “lakini mimi nataka kuwashirikisha vitendea kazi ‘software’ ambayo sasa ni fikra ‘mindset’, ninyi ambao mmeitwa sasa na mmekubali kuwa Mahakimu ili mtoe haki mkiwa mamlaka yenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, moja ya kitendea kazi chenu cha muhimu itakuwa ‘sensitivity to justice’, muwiwe kuona haki inatendeka, ameeleza kuwa haki maana yake ni uamuzi unaofanywa kwa mujibu na kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na Sheria za Nchi na kwa mujibu wa ushahidi ulioletwa Mahakamani.”
Aliongeza pia, kitendea kazi kingine ni uwajibikaji ambapo amesisitiza kufanya kwa kujituma na kwa uaminifu, uadilifu kama kitendea kazi kingine ambapo amewataka kuwa na uwezo endelevu wa kufanya kazi, kuwa wabunifu na wenye kuchukua hatua za mapema katika kufanya maamuzi na kutatua vikwazo na changamoto wakati wa kutimiza majukumu yao ili kuimarisha ufanisi pamoja na Uzalendo wa Taifa.